• HABARI MPYA

    Monday, October 08, 2018

    RASMI, KUANZIA LEO OKTOBA 8, 2018 MASOUD JUMA IRAMBONA SI KOCHA WA SIMBA SC TENA

    Na Sada Salmin, DAR ES SALAAM
    HATIMAYE klabu ya Simba SC leo imetoa tamko rasmi la kuachana na Kocha Msaidizi, Mrundi Masoud Juma Irambona baada ya takriban mwaka mmoja wa kuwa klabu.
    Kaimu Rais wa Simba, Salum Abdallah ‘Try Again’ amesema kwamba uamuzi huo ni kwa faida ya klabu na kwa maslahi ya pande zote mbili na kumshukuru kocha huyo kwa kazi nzuri aliyoifanya kwa kipindi chote alichofanya kazi Msimbazi na kumtakia kheri katika maisha yake mapya nje ya klabu hiyo.
    “Tumekaa naye vizuri, ametusaidia sana, lakini kila jambo lina mwisho wake, kwa faida ya klabu yetu tumefikia makubaliano kwa faida ya pande zote mbili kuuvunja mkataba huu, ili tuweze kuendelea. Tumemfungulia mlango Masoud kwa roho safi, na huenda hii ikawa ni bahati yake huko mbele ya safari kwa sababu tunaamini ni mwalimu mzuri,” amesema taarifa hiyo. 
    Lakini Abdallah amesema kwamba japo anaamoini Juma atapata klabu nyingine kubwa zaidi, lakini Mungu akipenda anaweza kurudi Tanzania kufundisha Simba SC.
    Kwa upande wake, Masoud ameushukuru uongozi wa Simba kwa kumuamini na kumpa nafasi hiyo, huku akiwatakia mafanikio mema kwenye mashindano yote yaliyo mbele yake.

    Kuanzia leo Oktoba 8, 2018 Masoud Juma Irambona si kocha wa Simba SC tena

    “Kazi ilikuwa inakwenda vizuri lakini kila jambo lina mwanzo na mwisho. Tumefikia makubaliano na klabu juu ya maslahi mazuri ya Simba kwenye ligi na kwenye mashindano mengine. Leo imefikia mwisho lakini siyo mwisho maana kwa nguvu za Mungu saa nyingine mtaniona tena,” amesema kocha huyo.
    Juzi Try Again alisema kwamba kutokana na Juma kushindwa kuelewana na kocha mkuu, Mbelgiji Patrick Aussems wamelazimika kuamua moja kwa manufaa ya klabu.
    Salim amesema uongozi wa Simba umekuwa ukijitahidi kusuluhisha na kuwaweka sawa makocha hao, lakini imeshindikana, hivyo ndani ya siku chache zijazo utatangaza rasmi kuachana na kocha huyo raia wa Burundi.
    Juma aliwasili nchini Oktoba 19, mwaka mwaka jana akitokea Rwanda alipokuwa anafundisha timu ya Rayon Sport, kuchukua nafasi ya aliyekuwa kocha Msaidizi wa Simba, Mganda Jackson Mayanja aliyeng’atuka.
    Alianza kazi chini ya Mcameroon, Joseph Omog lakini akafukuzwa, akaletewa Mfaransa, Pierre Lechantre aliyemalizia msimu na timu ikatwaa ubingwa kabla ya kufukuzwa – na Mbelgiji, Patrick J Aussems anakuwa kocha wa tatu mkuu wa Mrundi huyo.
    Lakini wakati Lechantre anaondoka alimtupia lawama Juma akidai alimsaliti na inaelezwa alitafuta nafasi ya kuzungumza na Aussems kumueleza juu ya kocha huyo wa Burundi. 
    Masoud alikuwa Msaidizi wa Omog katika mechi 10 tu, timu ikishinda mechi sita, sare tatu na kufungwa moja kwa penalti 4-3 na Green Warriors Mwenge katika hatua za awali za Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Azam Sports Federation Cup (ASFC) Uwanja wa Azam Complex, Chamazi mjini Dar es Salaam.
    Baada ya kutolewa na Green Warriors katika Kombe la TFF, Omog akafukuzwa na Masoud akakaimu Ukoha Mkuu, timu ikicheza mechi saba, kushinda nne, sare moja na kufungwa mbili kabla ya ujio wa Kocha mpya Mkuu, Mfaransa Pierre Lechantre.
    Na wakati wa Lechantre Simba ilicheza mechi 22 na kushinda 14, sare saba na kufungwa moja kabla ya Mfaransa huyo kuondolewa na Masoud tena kuwa Kaimu Kocha Mkuu akiiongoza timu katika mechi nane na kushinda tano, kufungwa mbili na sare moja.
    Na chini ya Aussems, pamoja na zile mechi tatu ambazo hakusafiri, Simba imecheza jumla ya mechi 14, ikishinda nane, sare tano na kufungwa moja. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: RASMI, KUANZIA LEO OKTOBA 8, 2018 MASOUD JUMA IRAMBONA SI KOCHA WA SIMBA SC TENA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top