• HABARI MPYA

    Wednesday, October 10, 2018

    PETER TINO AONGOZA MSAFARA WA TAIFA STARS KWENDA PRAIA KUIVAA CAPE VERDE IJUMAA KUFUZU AFCON 2019

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    GWIJI wa soka Tanzania, Augustino Peter Magali ‘Peter Tino’ amesafiri na kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars kwenda mjini Praia nchini Cape Verde kwa ajili ya mchezo na weneyeji wao hao Ijumaa.
    Taifa Stars imeondoka Alfajiri ya leo kwenda Praia ambako Ijumaa watakuwa wageni wa Cape Verde katika mchezo wa Kundi L kufuzu AFCON kabla ya kurejea Dar es Salaam kwa mchezo wa marudiano na wapinzani wao hao Oktoba 16.
    Tino ni mfungaji wa bao lililoipa Tanzania tiketi ya Fainali pekee za AFCON mwaka 1980 zilizofanyika mjini Lagos nchini Nigeria.
    Tino, mchezaji wa zamani wa African Sports ya Tanga, Pan African, Yanga za Dar es Salaam na Maji Maji ya Songea, alifunga bao la kusawazisha dakika ya 84 Uwanja wa Ndola katika sare ya 1-1 na Zambia kufuatia Alex Chola kuanza kuanza kuwafungia wenyeji dakika ya 43  Agosti 26 mwaka 1979.

    Wachezaji wa Taifa Stars wakiondoka mjini Dar es Salaam Alfajiri ya leo kwenda Praia 

    Na Taifa Stars ikafuzu kwa ushindi wa jumla wa 2-1, kufuatia ushindi wa 1-0 kwenye mchezo wa kwanza Agosti 11 mwaka huo huo, 1979 Uwanja wa Taifa (sasa Uhuru) mjini Dar es Salaam, bao pekee la Mohammed Rishard ‘Adolph’.
    Kocha Mnigeria, Emmanuel Amunike amewaengua beki Andrew Vincent ‘Dante’ na viungo Jonas Mkude na Frank Domayo kwa sababu wote ni majeruhi, wakati kiungo Salum Kihimbwa na mshambuliaji Kelvin Sabato wameachwa kwa sababu za kiufundi.
    Viungo wengine, Simon Msuva wa Difaa Hassan El-Jadidi ya Morocco, Farid Mussa na washambuliaji Shaaban Iddi Chilunda wote wa CD Tenerife ya Hispania na Nahodha Mbwana Ally Samatta wa KRC Genk ya Ubelgiji wap watajiunga na timu moja kwa moja mjini Praia baadaye leo.
    Wachezaji wengine wote wanaocheza nje, mabeki; Hassan Kessy wa Nkana FC ya Zambia, Abdi Banda wa Baroka FC ya Afrika Kusini, kiungo Himid Mao wa Petrojet ya Misri na washambuliaji Thomas Ulimwengu wa Al Hilal ya Sudan na Rashid Mandawa wa BDF XI ya Botswana wameondoka pamoja na wengine wanaocheza nchini leo.
    Peter Tino akiwa Uwanja wa Ndege 
    wa Kimataifa wa Julius Nyerere kwa 
    safari ya Praia Alfajiri ya leo
    Taifa Stars iliyokuwa imeweka kambi katika hoteli ya Sea Scape iliyopo Kunduchi mjini Dar es Salaam ilikuwa ikifanya mazoezi Uwanja wa JMK Centre, eneo la Gerezani katikati ya Jiji chini ya Kocha Mkuu, Amunike, anayesaidiwa na Mnigeria mwenzake, Emeka Amadi, na wazalendo Hemed Suleiman ‘Morocco’, Meneja Danny Msangi, Mtunza Vifaa ni Ally Ruvu na Madaktari Richard Yomba na Gilbert Kigadya.
    Tanzania inashika nafasi ya tatu katika Kundi L ikiwa na pointi mbili tu baada ya sare zote katika mechi zake mbili za mwanzo, 1-1 na Lesotho nyumbani mwaka jana na 0-0 na Uganda ugenini mapema mwezi huu.
    Uganda wanaendelea kuongoza Kundi hilo kwa pointi zao nne, wakifuatiwa na Lesotho mbili sawa na Tanzania na mabao mawili ya kufunga, wakati Cape Verde wanashika mkia kwa pointi yao moja. 
    Kihistoria Tanzania imecheza fainali moja tu za AFCON, mwaka 1980 nchini Nigeria, tena enzi hizo bado zinajulikana kama Fainali za kombe la Mataifa Huru ya Afrika.

    Kipa Aishi Manula akiwaongoza wenzake kuteremka kwenye basi kwenda kupanda ndege kwa safari ya Praia 

    Kikosi kizima cha Stars kinachotarajiwa kuwasili Praia leo kinaundwa na makipa; Aishi Manula (Simba SC), Beno Kakolanya (Yanga SC), Aaron Kalambo (Tanzania Prisons) na Benedicto Tinocco (Mtibwa Sugar Tanzania).
    Mabeki; Hassan Kessy (Nkana FC/Zambia), Shomari Kapombe (Simba SC), Salum Kimenya (Tanzania Prisons), Gardiel Michael (Yanga SC), Paulo Ngalema (Lipuli FC), Ally Sonso (Lipuli FC), Aggrey Morris (Azam FC), David Mwantika (Azam FC), Abdallah Kheri (Azam FC), Kelvin Yondani (Yanga SC) na Abdi Banda (Baroka FC).
    Viungo ni Himid Mao (Petrojet/Misri), Simon Msuva (Difaa Hassan El –Jadida/Morocco), Mudathir Yahya (Azam FC), Feisal Salum (Yanga SC) na Farid Mussa (CD Tenerife/Hispania).
    Washambuliaji; Mbwana Samatta (Nahodha, KRC Genk/Ubelgiji), Thomas Ulimwemgu (Al Hilal/Sudan), John Bocco (Simba SC), Yahya Zayed (Azam), Kelvin Sabato (Mtibwa Sugar), Rashid Mandawa (BDF XI/Botswana) na Shaaban Iddi Chilunda (CD Tenerife/Hispania).
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: PETER TINO AONGOZA MSAFARA WA TAIFA STARS KWENDA PRAIA KUIVAA CAPE VERDE IJUMAA KUFUZU AFCON 2019 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top