• HABARI MPYA

    Sunday, October 14, 2018

    MIAKA 19 BILA RAIS WA KWANZA WA NCHI MPENDA MICHEZO, MWALIMU JULIUS KAMBARAGE NYERERE

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    KADI namba moja ya uanachama wa klabu ya Yanga SC ya Dar es Salaam, inadaiwa alipewa hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ambaye leo anatimiza miaka 19 tangu kifo chake, Oktoba 14, mwaka 1999.
    Wakati Mwalimu Nyerere anafariki dunia, mimi nilikuwa mwandishi mchanga sana- wakati huo nipo kampuni ya Habari Corporation Limited, chini ya wamiliki wake wa awali akina Jenerali Twaha Ulimwengu.
    Aliyekuwa bosi wangu wakati huo, Kenny Manara, aliyekuwa Mhariri wa gazeti DIMBA alinipa kazi ya kwenda Uwanja wa Taifa, sasa Uhuru ulipowekwa mwili wa marehemu kwa ajili ya kuagwa ili kuandika habari juu ya wanamichezo waliojitokeza kuuaga mwili wa marehemu na kuchukua maoni yao.

    Mwalimu Julius Kambarage Nyerere akiwasabahi wachezaji wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars miaka ya 1970

    Hakika nilijifunza mengi sana kupitia msiba huo kwa kusikia, kuambiwa na kujionea. Miongoni mwa niliyoambiwa ni kwamba, Mwalimu Nyerere ndiye alikuwa ana kadi namba moja ya Yanga SC na kadi namba mbili, alikuwa nayo hayati Abeid Amaan Karume, rais wa zamani wa Zanzibar.
    Sijabahatika kuiona ‘leja’ ya Yanga hadi leo tangu nisikie habari hizo, kwa hivyo siwezi kusadiki, lakini kulingana na historia ya klabu ya Yanga katika harakati za ukombozi wa taifa letu, siwezi kupinga hilo.
    Nashukuru Mungu nikiwa Mwandishi wa Habari, nimewahi kufanya kazi za kuandika habari katika tukio ambalo Mwalimu Nyerere alikuwepo.
    Ilikuwa ni Aprili mwaka 1998 katika mechi ya mpira wa kikapu, iliyoandaliwa maalum kusherehekea kuzaliwa kwake, Mwalimu Nyerere Uwanja wa Ndani wa Taifa, kati ya Pazi na Don Bosco.
    Nakumbuka siku hiyo, mtangazaji mwenzangu wa Azam TV, Patrick Nyembele alikuwa bado anacheza mpira wa kikapu na ndiye alikuwa Nahodha wa Pazi ambayo ilishinda na kukabidhiwa na Kombe.
    Mechi hiyo iliandaliwa na Chama cha Mpira wa Kikapu Dar es Salaam (DABA), likiwa wazo la aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa DABA, Fakhrudin Amijee.
    Vyama vyote vya michezo vilialikwa kushiriki sherehe hiyo na vilitoa zawadi mbalimbali kwa Mwalimu.
    Bendi ya Varda Arts ilikuwepo kutumbuiza na ilimpigia wimbo mzuri Mwalimu wa Happy Birth Day. Rais wa awamu wa nne, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete, akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani na Ushirikiano wa Kimataifa wakati huo, alikuwepo na ndiye aliyekuwa amekaa meza kuu pamoja na marehemu Nyerere.
    Nilifarijika sana siku hiyo kufanya kazi mbele ya baba wa taifa na kwa kuwa pia nimefanya kazi mara kibao mbele ya marais waliomfuatia, Alhaj Ally Hassan Mwinyi, Benjamin William Mkapa, Jakaya Mrisho Kikwete na Dk. John Pombe Joseph Magufuli, najivunia sana hayo.
    Na kabla ya hapo, Mwalimu Nyerere alihudhuria matukio mengi ya michezo - enzi za utawala wake nchi ilikuwa ina sera nzuri kwa ajili ya michezo zilizosaidia kupatikana vipaji vingi na mafanikio ya kujivunia kwa ushindi wa wanamichezo wake kwenye mashindano makubwa. 
    Nilimpenda Mwalimu Nyerere tangu nasoma shule ya msingi pale Mgulani, Dar es Salaam na ninavutiwa sana na sera na misimamo yake enzi za uhai wake.
    Sijui, nasema sijui kama bila ya Nyerere Tanzania ingekuwepo na hata hiyo Tanganyika ingekuwaje. Sijui! Leo tunaishuhudia Tanzania ambayo mambo mengi yaliyoonekana ya ajabu wakati wa Nyerere yamekuwa ya kawaida.
    Rushwa, ukatili, unafiki, ulafi wa madaraka, ubifansi, ukabila, udini, ufisadi na uzandiki haya si ya ajabu tena katika Tanzania ya leo. Tena watu hawana aibu wala woga, wamekuwa jasiri wa uovu na hawamuogopi hata Mungu.
    Tuna kila sababu ya kumlilia Mwalimue Nyerere na kumkumbuka sana leo akitimiza miaka 19, tangu kifo chake.  
    Pongezi kwa Rais wa awamu wa tano, Dk. John Pombe Joseph Magufuli kwa kupambana kuirudisha nchi katika mstari. 
       
    HUYU NDIYE NYERERE
    Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alikuwa rais wa kwanza wa Tanzania. Alizaliwa Butiama, mkoani Mara pembezoni mwa Ziwa Nyanza Aprili, 13, mwaka 1922. Alifariki dunia Oktoba 14, mwaka 1999. Aliiongoza Tanzania tangu mwaka 1961 hadi mwaka 1985.
    Yeye ni mwasisi wa itikadi ya ujamaa na kujitegemea. Kabla ya kuingia kwenye siasa alikuwa ni mwalimu. Kazi hii ndiyo ilimpatia jina ambalo lilimkaa maisha yake yote la ‘Mwalimu’.
    Mwalimu Nyerere ni kati ya viongozi wachache wa Afrika ambao wameacha madaraka kwa hiyari baada ya kutawala kwa muda mrefu.
    Alipostaafu urais mwaka 1985 alirudi kijijini kwake Butiama ambako aliendesha shughuli za kilimo. Aliendelea kuwa na athari kubwa katika siasa ya Tanzania hadi kifo chake.
    Julius Kambarage Nyerere alizaliwa mwaka 1922 katika kijiji cha Butiama, wilaya ya Musoma, mkoa wa Mara, Tanzania (wakati ule: Tanganyika).
    Alikuwa miongoni mwa watoto 26 wa Nyerere Burito, chifu wa kabila la Wazanaki. Alipokuwa mtoto Nyerere alichunga mifugo ya baba yake na alipofikisha umri wa miaka 12 aliingia shule akitembea kilomita 30 hadi Musoma.
    Baada ya kumaliza shule ya msingi aliendelea kusoma shule ya Wamisionari Wakatoliki huko Tabora. Katika umri wa miaka 20 alibatizwa akawa mkristo Mkatoliki hadi mwisho wa maisha yake.
    Mapadri wakaona akili yake wakamsaidia kusomea Ualimu katika Chuo Kikuu cha Uganda, Makerere kilichopo Kampala, kuanzia mwaka 1943 hadi 1945.
    Akiwa Makerere, Mwalimu akaanzisha tawi la Umoja wa Wanafunzi Watanganyika pia amejihusisha na tawi la Tanganyika African Association (TAA). Baada ya kumaliza masomo ya ualimu alirudi Tabora akifundisha shule ya St.Mary´s. Mwaka 1949 alipata skolashipu ya kwenda kusoma kwenye Chuo Kikuu cha Edinburgh huko, Scotland ambako alisoma M.A. ya historia na uchumi, akiweka rekodi ya kuwa Mtanzania wa kwanza kusoma katika chuo kikuu cha Uingereza na Mtanzania wa pili kupata shahada ya elimu ya juu nje ya Tanzania.
    Aliporejea Tanganyika kutoka masomoni, Nyerere alifundisha Historia, Kingereza na Kiswahili katika shule ya St. Francis iliyo karibu na Dar es Salaam.
    Mwaka 1953 alichaguliwa kuwa rais wa chama cha Tanganyika African Association (TAA), chama ambacho alikisaidia kukijenga alipokuwa mwanafunzi katika chuo kikuu cha Makerere.
    Mwaka 1954 alikibadilisha chama cha TAA kwenda katika chama cha Tanganyika African National Union (TANU) ambacho kilikuwa cha kisiasa zaidi kuliko TAA.
    Ndani ya mwaka mmoja chama cha TANU kilikuwa tayari chama cha siasa kinachoongoza Tanganyika.
    Uwezo wa Mwalimu Nyerere uliwashitua viongozi wa kikoloni na kumlazimisha Nyerere kuchagua kati ya siasa na kazi ya ualimu. Nyerere alisikika akisema kuwa alikuwa mwalimu kwa kuchagua na mwanasiasa kwa bahati mbaya.
    Alijiuzuru ualimu na kuzunguka nchini Tanganyika kuzungumza na watu wa kawaida na machifu ili kuleta muungano katika mapigano ya uhuru.
    Pia alizungumza kwa niaba ya TANU katika Trusteeship council na Fourth committee ya Umoja wa Mataifa (UN) huko New York. Uwezo wake wa kimaongezi na kuunganisha watu ulimwezesha kufanikisha Tanganyika kupata uhuru bila umwagaji wa damu. Ushirikiano mzuri aliouonyesha aliyekuwa gavana wa wakati huo bwana Richard Turnbull ulisaidia pia kuharakisha upatikanaji wa uhuru.
    Nyerere aliingia katika bunge la kikoloni mwaka 1958 na kuchaguliwa kuwa Waziri Mkuu mwaka 1960. Mwaka 1961 Tanganyika ilipata uhuru wake na Desemba 9, 1961 na Nyerere alichaguliwa kuwa Waziri Mkuu wa Tanganyika huru na mwaka mmoja baadae Nyerere alikuwa raisi wa kwanza wa Jamhuri ya Tanganyika.
    Nyerere alikuwa kiungo muhimu katika muungano wa Tanganyika na Zanzibar kutengeneza Tanzania baada ya mapinduzi ya Zanzibar mwaka 1964 yaliyomtoa madarakani sultani wa Zanzibar Jamshid bin Abdullah.
    Februari 5, mwaka 1977 aliongoza chama cha TANU katika tendo la kuungana na chama tawala cha Zanzibar ASP na kuanzisha chama kipya cha CCM (Chama cha Mapinduzi) akiwa Mwenyekiti wake.
    Nyerere aliendelea kuongoza Taifa hadi 1985 alipomwachia nafasi rais wa pili Ali Hassan Mwinyi. Aliendelea kuongoza Chama cha CCM hadi 1990 na kuwa na hadhi kubwa katika siasa ya Tanzania hadi kifo chake.
    Inasadikika kuwa Nyerere alishawishi uteuzi wa Benjamini W.Mkapa kama mgombea wa rais wa mwaka 1995 na ambaye aliteuliwa kuwa rais kwenye uchaguzi wa mwaka 1995.
    Nyerere alikaa muda mwingi kwake Butiama akilima shamba lake. Pamoja na haya alianzisha taasisi yenye jina lake; mwaka 1996 alionekana akiwa mpatanishi wa pande mbalimbali wa vita vya wenyewe kwa wenyewe huko Burundi.

    Katikati ni Mwalimu Nyerere akiwa na Katibu wa DABA wa enzi hizo, Jackson Kalikumtima. kulia na aliyekuwa Waziri wa mambo ya Nje, Jakaya Kikwete kushoto, rais wa awamu ya nne ya Jamhiri ya Muungano Tanzania Aprili mwaka 1998 Uwanja wa Ndani wa Taifa 

    SIASA ZA UJAMAA NA KUJITEGEMEA…

    Baada ya kuona kuwa uchumi wa Tanzania hautaweza kusimama kwa siasa za kijamaa na kutoweza kuvumilia kuendesha nchi kwa siasa ambazo yeye hakuwa muumini, Nyerere kwa maamuzi yake mwenyewe aliamua kustaafu nafasi ya urais baada ya uchaguzi wa mwaka 1985 na kumwachia usukani Ali Hassan Mwinyi aliyetawala kwa siasa za uchumi wa soko huria.
    Katika hali ya kukubali ukweli, Nyerere alitamka katika tafrija ya kumuaga juu ya siasa yake kiuchumi “Nimefeli. Tukubali hivyo.”
    Wapo ambao wanamlaumu Mwalimu Nyerere kwa siasa zake za ujamaa kwa madai zilichelewesha maendeleo ya kiuchumi wa Tanzania.
    Mwalimu bado anakumbukwa na Watanzania hasa wa hali ya chini kutokana na sera zake za kujali utu na ubinadamu na pia ataendelea kukumbukwa na Waafrika kote barani hasa kwa mchango wake mkubwa wakati wa harakati za kupigania uhuru katika nchi mbali mbali barani Afrika.
    Ni mmoja wa viongozi wachache wanaokumbukwa kwa kutojilimbikizia mali pamoja na kutawala kwa miaka zaidi ya 24.
    Mwishoni mwa maisha yake Nyerere aliishi kama mkulima wa kawaida kijijini kwake Butiama, ingawa wakati mwingine alikuwa akija kwenye nyumba yake ya Msasani, Dar es Salaam.
    Alipatwa na kansa ya damu (leukemia) na kufariki dunia nchini Uingereza wakati wa kutibiwa katika mji wa London Oktoba 14, 1999. Alizikwa mahali pale alipozaliwa, kijiji cha Butiama.
    Ni miaka 19 leo tangu, taifa limpoteze Rais wake wa kwanza mpenda michezo, aliyekuwa ana kadi ya Yanga, Watanzania bado tunamkumbuka na kumlilia kipenzi chao. Mungu ampumzishe kwa amani milele. Amin.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MIAKA 19 BILA RAIS WA KWANZA WA NCHI MPENDA MICHEZO, MWALIMU JULIUS KAMBARAGE NYERERE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top