• HABARI MPYA

  Monday, October 08, 2018

  MENEJA WA AZAM FC, PHILIPO ALANDO ATUHUMIWA KUMFANYIA FUJO REFA MECHI NA LIPULI

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  KAMATI ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imemtia hatiani Meneja wa Azam FC, Philippo Alando kumfanyia fujo refa wa akiba katika mechi namba 65 dhidi ya Lipuli FC ya Iringa iliyomalizika kwa sare ya 0-0.
  Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), Boniface Wambura Mgoyo amesema Alando atapelekwa Kamati ya Nidhamu ya TFF kwa kosa la kumzonga Mwamuzi wa Akiba akilalamikia maamuzi yake katika mechi hiyo iliyochezwa Septemba 27 Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.
  Wambura Mgoyo amesema hayo yamefikiwa katika kikao cha Bodi Oktoba 5, mwaka huu kupitia taarifa na matukio katika mechi za Ligi Kuu, Ligi Daraja la Kwanza (FDL) zinazoendelea hivi sasa na taarifa mbalimbali. 
  Meneja wa Azam FC, Philippo Alando (kushoto) atapandishwa Kamati ya Nidhamu kujibu tuhuma zake

  Aidha, Wambura amesema kwamba Kocha Msaidizi wa Mbao FC, Augustino Joseph Malindi pia atapelekwa Kamati ya Nidhamu kwa kumfuata Mwamuzi na kumsakama kwa maneno na kumtolea vitisho vya kumroga katika mechi namba 76 dhidi ya wenyeji, Ruvu Shooting walioshinda 1-0. Wambura amesema naye refa Fikiri Yusuf Saleh amepewa onyo kwa kushindwa kufanya maamuzi sahihi katika baadhi ya matukio yaliyojitokeza katika mechi hiyo iliyochezwa Oktoba 1 Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani.
  Singida United wao wamepewa onyo kali kwa kuchelewa kwa dakika nane kwenye kikao cha maandalizi ya mechi namba 62 dhidi ya Mbeya City FC  Septemba 26 Uwanja wa Namfua mjini Singida, wenyeji wakishinda 3-0. Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 14(3) ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.
  Mchezaji wa Ruvu Shooting, Ayoub Kitala amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya Sh. 500,000 baada ya kutolewa nje kwa kadi nyekundu kwa kosa la kumpiga kiwiko mchezaji wa Mbeya City katika mechi namba 42 Septemba 19, 2018 Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya na adhabu imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 38(9) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti wa Wachezaji.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MENEJA WA AZAM FC, PHILIPO ALANDO ATUHUMIWA KUMFANYIA FUJO REFA MECHI NA LIPULI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top