• HABARI MPYA

  Saturday, October 06, 2018

  MBEYA CITY YAICHAPA PRISONS 2-1, SINGIDA UNITED WAIPIGA 3-1 NDANDA, KMC YAIVIMBIA MTIBWA MANUNGU

  Na Mwandishi Wetu, MBEYA
  TIMU ya Mbeya ya City imewazima mahasimu wao wa jiji la Mbeya, Tanzania Prisons kwa kuwachapa mabao 2-1 katika mchezo uliofanyika Uwanja wa Sokoine jioni ya leo.
  Shujaa wa MCC leo ni Nahodha wake, Erick Kyaruzi aliyefunga bao la ushindi dakika ya 87 katika mchezo huo mkali wa mahasimu wa jiji la Mbeya.
  Na hiyo ni baada ya Peter Mapunda kutangulia kuwafungia Mbeya City dakika ya saba na Jeremiah Juma Mgunda kuwasawazishia Tanzania Prisons dakika ya 41.
  Kwa matokeo hayo Mbeya City ya kocha Mrundi, Ramadhani Nswazurimo inafikisha pointi 13 baada ya kucheza mechi tisa, wakati Tanzania Prisons inayomilikiwa na Jeshi la Magereza nchini inabaki na pointi zake sita baada ya kucheza mechi tisa.

  Mbeya ya City imewazima mahasimu wao wa jiji la Mbeya, Tanzania Prisons leo Uwanja wa Sokoine

  Baada ya kufanikiwa kutwaa tuzo ya kocha Bora wa msimu uliopita wa Ligi Kuu Tanzania Bara Kocha, Mohamed Abdallah ‘Bares’ amejikuta katika mwanzo mgumu msimu huu, leo akipoteza mechi ya tano, nyingine nne akitoa sare tatu na kushinda moja.
  Mechi nyingine za Ligi Kuu leo, Singida United imeutumia vyema Uwanja wa nyumbani, Namfua mjini Singida kwa ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Ndanda FC. Mabao ya Singida yamefungwa na Habib Kiyombo mawili, dakika za 34 na 36 kwa penalti na Eliuter Mpepo dakika ya 86, wakati la Ndanda FC limefungwa na Vitalis Mayanga dakika ya 75.

  Singida United imeichapa 3-1 Ndanda FC leo Uwanja wa Namfua

  Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba, Kagera Sugar imelazimishwa sare ya 0-0 na Ruvu Shooting wakati Uwanja wa Manungu, Turiani mkoani Morogoro, Mtibwa Sugar imelazimishwa sare ya 1-1 na KMC ya Kinondoni, wenyeji wakitangulia kwa bao la Dickson Daudi dakika ya tatu kabla ya Emmanuel Mvuyekure kuwasawazishia wageni dakika ya 29.
  Mchezo wa mwisho wa Ligi Kuu leo kati ya mabingwa watetezi, Simba SC na African Lyon unaendelea hivi sasa Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MBEYA CITY YAICHAPA PRISONS 2-1, SINGIDA UNITED WAIPIGA 3-1 NDANDA, KMC YAIVIMBIA MTIBWA MANUNGU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top