• HABARI MPYA

    Thursday, October 04, 2018

    LIPULI FC YAAMUA KUIVAA STAND UNITED KESHO SAMORA BILA WAKALI WAKE WAWILI WA TAIFA STARS

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    TIMU ya Lipuli FC ya Iringa itawakosa wachezaji wake wawili tegemeo, mabeki Paulo Ngalema na Ally Sonso katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara dhidi ya Stand United Uwanja wa Samora mjini Iringa. 
    Wawili hao wapo katika kambi ya timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars inayojiandaa na michezo miwili ya nyumbani na ugenini Kundi L kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) dhidi ya Cape Verde.
    Na pamoja na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutoa fursa kwa klabu kuchukua wachezaji wake siku moja kabla ya mechi yake ya Ligi Kuu, lakini Lipuli FC imeamua kuendelea na mechi ya kesho dhidi ya Stand bila Ngalema na Sonso.
    Lipuli FC itamkosa beki wake, Paulo Ngalema kesho katika mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Stand United 

     
    Ligi Kuu inatarajiwa kuendelea kesho kwa mchezo mmoja kati ya Lipuli ya kocha Suleiman Matola na Stand United, wakati keshokutwa mechi tano zitafuatia kwenye viwanja tofauti.
    Uwanja wa Namfua mjini Singida, wenyeji Singida United watawakaribisha Ndanda FC, Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam, wenyeji Simba SC watamenyana na African Lyon, Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba, Kagera Sugar watawakaribisha Ruvu Shooting, Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya kutakuwa na mechi ya mahasimu wa Jiji la Mbeya, Tanzania Prisons na Mbeya City wakati Uwanja wa Manungu, Turiani mkoani Morogoro, Mtibwa Sugar watamenyana na KMC.
    Jumapili kutakuwa na mechi nyingine tatu, Yanga SC wakimenyana na Mbao FC Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam, Uwanja wa Meja Isamuhyo huko Mbweni, JKT Tanzania watamenyana na Alliance FC na Uwanja wa Karume mjini Musoma, Biashara United watakuwa wenyeji wa Mwadui FC, wakati JUmatatu Azam FC watawakaribisha Coastal Union.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: LIPULI FC YAAMUA KUIVAA STAND UNITED KESHO SAMORA BILA WAKALI WAKE WAWILI WA TAIFA STARS Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top