• HABARI MPYA

    Thursday, October 04, 2018

    KIMBE NA MNGUTO ‘WATUNISHIANA MISULI’ UENYEKITI WA BODI YA LIGI TANZANIA…KAMATI YA KUULI KUKUTANA LEO

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    MTENDAJI Mkuu wa Mbeya City, Emmanuel Kimbe na Mwenyekiti wa Coastal Union ya Tanga, Stephen Mnguto ndiyo wagombea pekee waliochukua fomu za kuwania Uenyekiti wa Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB).
    Wawili hao ni miongoni mwa viongozi wakuu wa klabu hiyo wenye heshima kubwa nchini baada ya kuziongoza kwa ufanisi klabu zao kwa miaka ya karibuni.
    Na wakati huu ambao Ligi Kuu inafanyika bila udhamini – inaaminika wanahitajika viongozi weledi, shupavu na jasiri watakaokwenda kufanya kazi nzuri TPLB. 
    Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Revocatus Kuuli amesema kwamba jioni ya leo watakuwa na kikao na baada ya hapo ndipo watatoa mustakabali mzima wa uchaguzi huo. 

    Emmanuel Kimbe (kushoto) atachuana na Stephen Mnguto kuwania Uenyekiti wa Bodi ya Ligi Novemba 17 Dar es Salaam

    Uchaguzi mdogo wa Kamati ya Uongozi (Management Committee) ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara kujaza nafasi zilizo wazi utafanyika Jumamosi Novemba 17, mwaka huu mjini Dar es Salaam na zoezi la kuchukua na kurudisha fomu lililoanza Septemba 21 lilikamilika Septemba 25, mwaka huu.
    Pamoja na nafasi ya Mwenyekiti, nafasi nyingine ni Mjumbe mmoja wa kuwakilisha Klabu za Ligi Kuu (PL), Mjumbe mmoja kuwakilisha Klabu za Ligi Daraja la Kwanza (FDL) na Mjumbe mmoja wa kuwakilisha Klabu za Ligi Daraja la Pili (SDL).
    Ada ya fomu kwa nafasi za Mwenyekiti ni Sh. 200,000 (Shilingi laki mbili)mbili wakati nafasi nyingine zilizobaki ni sh.100,000 (Shilingi laki moja) na Uchaguzi utaendeshwa kwa mujibu wa kanuni za Uchaguzi za TFF toleo la 2013.
    Wagombea kwa mujibu wa Kanuni za Uendeshaji za Bodi ya Ligi Kuu Tanzania ni marais au Wenyeviti wa Klabu husika, Hivyo, Wagombea wanatakiwa kuwa Wenyeviti au Marais wa Klabu husika. 
    Nafasi ya Mwenyekiti wa TPLB inagombewa na Klabu za Ligi Kuu pekee. Ikumbukwe, aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi, Clement Sanga alipoteza sifa baada ya kujiuzulu uongozi wa klabu yake, Yanga SC.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KIMBE NA MNGUTO ‘WATUNISHIANA MISULI’ UENYEKITI WA BODI YA LIGI TANZANIA…KAMATI YA KUULI KUKUTANA LEO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top