• HABARI MPYA

    Monday, October 08, 2018

    KAKOLANYA NA DANTE WOTE WAPO FITI KABISA NA LEO WAMEFANYA MAZOEZI TAIFA STRAS

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    PAMOJA na kushindwa kumalizia mechi jana kufuatia kuumia na kutolewa kwa machela, kipa wa Yanga Beno Kakolanya na beki Andrew Vincent ‘Dante’ leo asubuhi wote wamefanya mazoezi ya timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars.
    Yanga SC jana ilijisogeza hadi nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Mbao FC ya Mwanza Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam, lakini Kakolanya na Dante walitolewa kipindi cha pili baada ya kuumia.
    Meneja wa Taifa Stars, Danny Msangi ameiambia Bin Zubeiry Sports – Online kwamba wawili hao walipatiwa tiba nzuri jana baada ya mechi na hapana shaka wako tayari kuitetea nchi yao.  

    Kipa Beno Kakolanya (katikati) na beki Andrew Vincent ‘Dante’ (kulia) wote wamefanya mazoezi Taifa Stars leo

    “Beno na Dante wote wamefanya mazoezi leo asubuhi, kwa sababu baada ya mechi ya jana walipatiwa matibabu na wote wameamka vizuri,” amesema Msangi.
    Taifa Stars watakuwa wageni wa Cape Verde katika mchezo wa Kundi L kufuzu AFCON Oktoba 12 mjini Praia kabla ya kurejea Dar es Salaa kwa mchezo wa marudiano na wapinzani wao hao Oktoba 16.
    Kakolanya alifanya kazi nzuri ya kuokoa michomo ya hatari mfululizo langoni mwake na kabla ya kuumia dakika ya 55 na kushindwa kuendelea na mchezo, nafasi yake ikichukuliwa na Mkongo, Klaus Kindoki, wakati Dante alimpisha Abdallah Shaibu ‘Ninja’ dakika ya 74 baada ya kuumia pia.
    Wachezaji wote wanaocheza nyumbani wapo kambini katika hoteli ya Sea Scape iliyopo Kunduchi mjini Dar es Salaam pamoja na mmoja anayecheza nje, Thomas Ulimwengu wa El Hilal ya Sudan wakiwa wanaendelea na mazoezi chini ya Kocha Mkuu Emmanuel Amunike, anayesaidiwa na Mnigeria mwenzake, Emeka Amadi, na wazalendo Hemed Suleiman ‘Morocco’, Meneja Danny Msangi, Mtunza Vifaa ni Ally Ruvu na Madaktari Richard Yomba na Gilbert Kigadya.
    Ambao hawajaripoti ni mabeki Hassan Kessy wa Nkana FC ya Zambia na Abdi Banda Baroka FC ya Afrika Kusini, viungo Himid Mao wa Petrojet ya Misri, Simon Msuva wa Difaa Hassan El –Jadida ya Morocco na Farid Mussa wa CD Tenerife ya Hispania na washambuliaji Nahodha Mbwana Samatta wa KRC Genk ya Ubelgiji, Rashid Mandawa wa BDF XI ya Botswana na Shaaban Iddi Chilunda wa CD Tenerife ya Hispania.
    Tanzania inashika nafasi ya tatu katika Kundi L ikiwa na pointi mbili tu baada ya sare zote katika mechi zake mbili za mwanzo, 1-1 na Lesotho nyumbani mwaka jana na 0-0 na Uganda ugenini mapema mwezi huu.
    Uganda wanaendelea kuongoza Kundi hilo kwa pointi zao nne, wakifuatiwa na Lesotho mbili sawa na Tanzania na mabao mawili ya kufunga, wakati Cape Verde wanashika mkia kwa pointi yao moja. 
    Kihistoria Tanzania imecheza fainali moja tu za AFCON, mwaka 1980 nchini Nigeria, tena enzi hizo bado zinajulikana kama Fainali za kombe la Mataifa Huru ya Afrika.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KAKOLANYA NA DANTE WOTE WAPO FITI KABISA NA LEO WAMEFANYA MAZOEZI TAIFA STRAS Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top