• HABARI MPYA

  Sunday, October 07, 2018

  JONGO ALIYETANGAZA MECHI TAIFA STARS IKIFUZU KOMBE LA MATAIFA YA AFRIKA 1980 AFARIKI DUNIA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  RAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Wallace Karia ametuma salamu za rambirambi kwa familia ya mtangazaji wa zamani wa michezo Ahmed Jongo aliyefariki leo hospitali ya Temeke mjini Dar es Salaam.
  Jongo alistaafu utangazaji wa Redio Tanzania, kwa sasa TBC 2005 na kwa muda sasa amekuwa akisumbuliwa na matatizo ya kiafya.
  Kwa mujibu wa familia ya marehemu, mwili wa Jongo unatarajiwa kupumzishwa kesho Saa 7:00 mchana katika makaburi ya Tandika mjini Dar es Salaam.

  Ahmed Jongo katika siku za mwisho za uhai wake, akiwa kwenye mahojiano na Azam TV 

  Na kwa niaba ya TFF, Karia ametoa pole kwa wafiwa, familia, ndugu, jamaa na marafiki kwa msiba huo.
  “Nimepokea kwa majonzi makubwa taarifa ya kifo cha Ahmed Jongo,kwa niaba ya TFF natoa pole kwa ndugu,jamaa na marafiki,hakika tutamkumbuka kwa umahiri wake wa kutangaza mpira wa miguu”.
  Rais wa TFF, Karia amesema Jongo enzi za uhai wake alipokuwa Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD) alikuwa chachu ya Watanzania wengi kufuatilia mpira wa miguu kutokana na umahiri wake wa kutangaza mpira kupitia matangazo ya moja kwa moja kwenye Radio.
  Amesema aina ya utangazaji wa mpira wa Jongo ulishawishi wengi kufuatilia mpira wa miguu na kuhudhuria kutazama mechi mbalimbali.
  Jongo ametangaza mechi nyingi akiwa RTD, lakini mchezo maarufu zaidi ni wa marudiano kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka 1979 mjini Ndola, baina ya wenyeji Zambia na Tanzania.
  "Tunakwenda Lagos...Tunakwenda Lagos...Tunakwenda Lagos" ilikuwa ni sauti ya Jongo baadaya filimbi ya mwisho kuwaarifu Watazania kupitia RTD baada ya filimbi ya mwisho Taifa Stars ikitoa sare ya 1-1 na KK 11 na kufuzu CAN (sasa AFCON) kwa ushindi wa jumla wa 2-1 kufuatia ushindi wa 1-0 kwenye mchezo wa kwanza Dar es Salaam.
  Shujaa wa Tanzania siku hiyo alikuwa mshambuliaji Peter Tino aliyefunga bao la kusawazishia dakika za mwishoni na kuipa Taifa Stars nafasi pekee ya kucheza AFCON hadi leo. 
  Mungu ampumzishe kwa amani marehemu Ahmed Jongo. Amin.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: JONGO ALIYETANGAZA MECHI TAIFA STARS IKIFUZU KOMBE LA MATAIFA YA AFRIKA 1980 AFARIKI DUNIA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top