• HABARI MPYA

  Wednesday, October 10, 2018

  ETO’O AWASILI DAR NA KUMKUMBUSHIA IVO MAPUNDA MACHUNGU YA YOUNDE 2008 STARS NA CAMEROON

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  MWANASOKA Bora wa zamani Afrika, Mcameroon Samuel Eto'o leo amekumbushia machungu ya uwanjani kipa wa zamani wa kimataifa wa Tanzania, Ivo Mapunda walipokutana mjini Dar es Salaam.  
  Eto’o ambaye kwa sasa anamalizia soka yake katika klabu ya Qatar SC, amewasili nchini jioni ya leo kwa shughuli za uzinduzi wa Uwanja wa soka eneo la Coco Beach mjini Dar es Salaam, kabla ya kukutana na Mapunda.
  Eto’o alitua mchana wa leo Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) mjini Dar es Salaam na kupokewa na mwenyeji wake, Meneja wa Castle Lager, Pamera Kikuli kabla ya kupelekwa katika hoteli ya Ramada, eneo la Kunduchi mjini hapa.
  Gwiji wa Cameroon, Samuel Eto'o (kulia) akiwa na kipa wa zamani wa Taifa Stars, Ivo Mapunda baada ya kukutana tena leo Dar es Salaam

  Samuel Eto'o na Ivo Mapunda wakiwa na Meneja wa Castle Lager, Pamera Kikuli (katikati) katika Hotel ya Ramada mjini Dar es Salaam jioni ya leo

  Na huko ndiko Eto’o mwenye umri wa miaka 37 alipokutana na Mapunda na kuzungumza naye wakikumbushana mara ya mwisho walipokutana uwanjani Juni 21, mwaka 2008 mjini katika mchezo wa Kundi la Kwanza kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2010 nchini Angola.
  Siku hiyo, Eto’o alimfunga mabao mawili rahisi Mapunda na Simba Wasiofungika wakaibuka na ushindi wa 2-1 nyumbani, bao la Taifa Stars likifungwa na Danny Mrwanda na kuzima ndoto za Tanzania kwenda AFCON kwa mara ya pili baada ya mwaka 1980. 
  Katika michuano hiyo, Tanzania ilimaliza nafasi ya tatu kwa pointi zake nane, nyuma ya Cameroon pointi 16, Cape Verde pointi tisa huku Mauritius wakishika mkia kwa pointi yao moja. 
  Mapunda, kipa wa zamani wa Tukuyu Stars, Tanzania Prisons za Mbeya, Yanga, African Lyon, Simba SC, Azam FC za Dar es Salaam, Gor Mahia ya Kenya na St George ya Ethiopia tayari amestaafu soka wakati Eto’o ambaye ni Balozi wa Bia ya Castle Afrika anamalizia soka yake Qatar.
  Na hiyo ni baada ya kuzitumikia Real Madrid, Leganes, Espanyol, Mallorca, Barcelona zote za Hispania, Inter Milan ya Italia, Anzhi Makhachkala ya Urusi, Chelsea, Everton za England, Sampdoria ya Italia, Antalyaspor, Konyaspor za Uturuki na sasa Qatar SC.
  Eto’o, Mwanasoka Bora wa Afrika mara nne katika miaka ya 2003, 2004, 2005 na 2010 kesho anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika zoezi la uzinduzi wa Uwanja mpya wa soka eneo la Coco Beach.

  Samuel Eto'o na (katikati) akiwa na Meneja wa Castle Lager, Pamera Kikuli (kushoto) baada ya kuwasili Uwanja wa Ndege wa JNIA
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: ETO’O AWASILI DAR NA KUMKUMBUSHIA IVO MAPUNDA MACHUNGU YA YOUNDE 2008 STARS NA CAMEROON Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top