• HABARI MPYA

  Sunday, October 07, 2018

  AJIB AFUNGA ‘BONGE LA BAO’ YANGA YAIKANDAMIZA MBAO FC 2-0 TAIFA NA KURUDI JUU LIGI KUU

  Na Sada Salmin, DAR ES SALAAM
  TIMU ya Yanga SC imejisogeza hadi nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Mbao FC ya Mwanza usiku wa leo Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
  Kwa ushindi huo, Yanga SC inafikisha pointi 16 baada ya kucheza mechi sita, sawa na Singida United yenye wastani mdogo wa mabao na mechi tatu zaidi za kucheza - wakizidiwa pointi moja na Mtibwa Sugar wanaoongoza Ligi Kuu kwa pointi zao 17 za mechi tisa.
  Mabingwa watetezi, Simba SC wao wapo nafasi ya nne kwa pointi zao 14 baada ya kucheza mechi saba, wakizidiwa pointi moja na Azam FC iliyocheza mechi saba pia.
  Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Hans Mabena wa Tanga aliyesaidiwa na Jesse Erasmo na Makame Mdogo, hadi mapumziko Yanga SC walikuwa mbele kwa bao 1-0.
  Ibrahim Ajib (katikati) akishangilia baada ya kuifungia Yanga SC bao la pili  Bao hilo lilifungwa na kiungo Raphael Daudi Alpha dakika ya 16 kwa kichwa akimalizia mpira wa adhabu uliopigwa na kiungo Ibrahim Ajib kutoka upande wa kulia wa Uwanja.
  Kipa Beno Kakolanya alifanya kazi nzuri ya kuokoa michomo ya hatari mfululizo langoni mwake na kabla ya kuumia dakika ya 55 na kushindwa kuendelea na mchezo, nafasi yake ikichukuliwa na Mkongo, Klaus Kindoki.
  Kindoki aliwaweka roho juu mashabiki wa Yanga SC baada ya kufanya makosa kadhaa, lakini safu ya ulinzi ikiongozwa na mkongwe Kelvin Yondan ikasimama imara kumlinda.
  Yanga SC ikapata pigo lingine dakika ya 74 baada ya beki wake, Andrew Vincent ‘Dante’ kuumia kufuatia kuchezewa rafu na David Mwasa wa Mbao FC na kushindwa kuendelea na mchezo, nafasi yake ikichukuliwa na Abdallah Shaibu ‘Ninja’.
  Ajib akafunga bao zuri mno kwa tik tak maridadi dakika ya pili ya muda wa nyongeza baada ya kutimia dakika 90 za kawaida za mchezo kufuatia kukutana na mpira uliookolewa na beki Amos Charles wa Mbao FC.
  Mbao walikuwa wakicheza rafu mno na mabeki wengine wa Yanga, Gardiel Michael na Paulo Godfrey walimalizia mechi wanachecheema kutokana na kuumizwa.
  Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Beno Kakolanya/Klaus Kindoki dk55, Paulo Godfrey, Gardiel Michael, Andrew Vincent ‘Dante’/Abdallah Shaibu ‘Ninja’ dk74, Kelvin Yondan, Feisal Salum ‘Fei Toto’, Deus Kaseke, Raphael Daudi, Matheo Anthony/Matheo Anthony dk57, Ibrahim Ajib na Heritier Makambo.  
  Mbao FC; Hashim Mussa, Vincent Philipo, David Mwasa, Peter Mwangosi, Amos Charles/Abubakar Ngalema dk41/Emmanuel Mtumbuka dk82, Ally Mussa, Said Khamis/Rayson Okello dk77, Hussein Kasanga, Hamim Abdulkarim, Pastory Athanas na Robert Ndaki.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: AJIB AFUNGA ‘BONGE LA BAO’ YANGA YAIKANDAMIZA MBAO FC 2-0 TAIFA NA KURUDI JUU LIGI KUU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top