• HABARI MPYA

    Sunday, September 09, 2018

    YALIYOPITA SI NDWELE, STARS BADO INA NAFASI YA KWENDA CAMEROON

    MATUNDA ya kucheza kwa nidhamu na kukumbuka maelekezo ya kocha wakati wote yameonekana jana Tanzania ikilazimisha sare ya 0-0 na wenyeji, Uganda katika mchezo wa Kundi L kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwakani nchini Cameroon leo Uwanja wa Mandela, Namboole mjini Kampala.
    Safu ya ulinzi ya Taifa Stars haikuwa na makosa mengi jana na wachezaji wa safu ya kiungo walisaidia ulinzi kikamilifu badala ya kufikiria kushambulia pekee. Simon Msuva na Thomas Ulimwengu pamoja na kuchezeshwa kama viungo washambuliaji, lakini muda mwingi walikuwa katikati ya Uwanja kusaidia udhibiti.

    Nahodha na nyota mkubwa wa timu, Mbwana Ally Samatta alikuwa anakaba jana hadi akaonyeshwa kadi ya njano – na kwa sababu hiyo haikuwa ajabu Uganda jana walibanwa kwao. 
    Na kama si Samatta kukosa bao la wazi jana dakika ya 70 baada ya kupatwa na ‘kigugumizi cha miguu’ hadi kipa Dennis Onyango akaokoa kufuatia pasi nzuri ya Ulimwengu, Uganda wangefungwa kwao jana.
    Sare ya jana ya ugenini dhidi ya timu ngumu kama Uganda, inamaanisha mwanzo mzuri kwa kocha mpya wa Tanzania, Emmanuel Amunike kutoka Nigeria aliyeanza kazi Agosti 6 akimpokea mzalendo, Salum Mayanga.
    The Cranes inabaki juu kwenye msimamo wa Kundi L ikifikisha pointi nne baada ya kucheza mechi mbili wakati Taifa Stars inaokota pointi ya pili tu katika mechi yake ya pili, wote wakiwa wamecheza nyumbani na ugenini.
    Na hiyo ni kabla ya mwingine wa kundi hilo kati ya Lesotho na Cape Verde kesho mjini Maseru. Kwa sasa, Lesotho wana pointi moja baada ya sare ya na Tanzania kwenye mechi ya kwanza na Cape Verde hawana pointi kufuatia kufungwa na Uganda nyumbani mwaka jana.
    Amunike aliingia kwenye mechi ya jana bila wachezaji sita wazoefu, mabeki Shomari Kapombe, Erasto Nyoni, viungo Jonas Mkude, Hassan Dilunga, Shiza Kichuya na mshambuliaji John Bocco wote wa Simba pamoja na kiungo chipukizi wa Yanga, Feisal Salum.
    Hiyo ni baada ya kuwaondoa kambini kufuatia wachezaji hao kukaidi wito wa kuripoti kambini kwa wakati waliotakiwa. Lakini baada ya mazungumzo na wachezaji hao, Amunike alisema amewasamehe na atawapa tena nafasi wakiendelea kuonyesha uwezo kwenye klabu zao.
    Pamoja na kulazimisha sare ya ugenini jana, lakini umuhimu wa wachezaji walioenguliwa kwa utovu wa nidhamu ulionekana jana – hususan mabeki wanaoweza kucheza kama viungo pia, Erasto Nyoni na Shomari Kapombe, pamoja na viungo Shiza Kichuya na Hassan Dilunga.
    Nazungumzia mchezo wa jana, kuna wakati nilikuwa ninawaza kabisa kama wanne hao wangekuwepo uwanjani Kampala ingekuwa kimya jana. Lakini kuna mambo lazima yatokee katika kuelekea hatua za kimafanikio na mara nyingine huwa ya aina hii pia.
    Baada ya sare ya 1-1 nyumbani na Lesotho Juni 10, mwaka jana tulijutia kupeleka mechi kwenye Uwanja mdogo wa Azam Complex, Chamazi mjini Dar es Salaam na kujikuta tunanasa kwenye mitego ya wageni kwa urahisi.
    Na baada ya sare ya hii ya pili ugenini tunasemaje? Tunaweza kufurahia sare tu kwa sababu ni ya ugenini, wakati wapinzani wana rekodi ya ushindi wa ugenini dhidi ya Cape Verde – au tunaanza kutafuta mchawi mwingine?
    Huu si wakati wa kulaumiana bali kujipanga kwa michezo ijayo, benchi la Ufundi litazame mapungufu yaliyojitokeza na kuyafanyia marakebisho kuelekea mchezo ujao dhidi ya Cape Verde Oktoba 10 Uwanja wa Taifa wa Cape Verde mjini Praia kukamilisha mechi zake za mzunguko wa kwanza kufuzu AFCON.
    Taifa Stars bado ina nafasi ya kufuzu AFCON ya mwakani iwapo itafanya vyema kwenye mechi zake zilizosalia – ni juu ya viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzanjia (TFF) na benchi la Ufundi kuweka mikakati ya maandalizi kuelekea michezo hayo. 
    Wahenga walinena; “Yaliyopita si ndwele, tugange yajayo”, basi ni muhimu kuelekeza nguvu kwenye mechi zijazo, nafasi ya kwenda Cameroon bado ipo. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YALIYOPITA SI NDWELE, STARS BADO INA NAFASI YA KWENDA CAMEROON Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top