• HABARI MPYA

  Saturday, September 08, 2018

  TAIFA STARS YALAZIMISHA SARE 0-0 NA UGANDA KAMPALA, SAMATTA AKOSA BAO LA WAZI NAMBOOLE

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  TANZANIA imelazimisha sare ya 0-0 na wenyeji, Uganda katika mchezo wa Kundi L kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwakani nchini Cameroon jioni ya leo Uwanja wa Mandela, Namboole mjini Kampala.
  The Cranes inabaki juu kwenye msimamo wa Kundi L ikifikisha pointi nne baada ya kucheza mechi mbili wakati Taifa Stars inaokota pointi ya pili tu katika mechi yake ya pili, wote wakiwa wamecheza nyumbani na ugenini.
  Katika mchezo huo uliochezeshwa na Eric Arnaud Otogo Castane aliyesaidiwa na washika vibendera Moussounda Montel wote wa Gabon na Issa Yaya wa Chad, Uganda walio chini ya kocha Mfaransa, Sebastien Desabre walitawala kipindi cha kwanza kabla ya Tanzania inayofundishwa na Mnigeria, Emmanuel Amunike kuzinduka kipindi cha pili.
  Nahodha Mbwana Samatta amekosa bao la wazi dakika ya 70 leo Uwanja wa Mandela               PICHA YA MAKTABA

  Pamoja na kwamba Uganda walitawala mchezo kipindi cha kwanza, lakini shambulizi la ‘kurusha roho’ lilikuwa moja tu, pale Joseph Ochaya alipopiga nje akiwa amebaki na kipa Aishi Manula kufuatia krosi ya Nicholas Wadada kutoka upande wa kulia.
  Mpango wa kuchezesha mabeki watatu wa kati, Aggrey Morris, David Mwantika na Abdi Banda ulionekana kumsaidia kocha Amunike, kwani walinzi hao waliwadhibiti vizuri washambuliaji hatari wa The Cranes akina Emmanuel Okwi, Farouk Miya na Ochaya.  
  Na kutokana na mchezo wa kujihami zaidi kipindi cha kwanza, haikuwa ajabu washambuliaji wa Tanzania nao wakiongozwa na Nahodha wao, Mbwana Samatta, Emmanuel Ulimwengu na Simon Msuva wakishindwa kupiga shuti moja kwenye lango la Uganda.
  Amunike alibadili mambo kipindi cha pili na akawaruhusu vijana wake kulielekea lango la wenyeji na hapo ndipo iliposhuhudiwa kipa Dennis Onyango akifanya kazi yake kwa kuokoa mara kwa mara.
  Ni Nahodha, Samatta aliyepoteza nafasi nzuri kwenye mchezo huo dakika ya 70 baada ya kupewa pasi nzuri na Ulimwengu, lakini akiwa akiwa amebaki na kipa Onyango akashindwa kufunga. Mpira wa kwanza aliopiga ulimbabatiza kipa huyo lakini ukamrudia na badala ya kutoa pasi kwa wenzake waliokuwa kwenye nafasi, akajaribu kumpiga chenga Onyango akaunasa.
  Kutoka hapo, timu hizo ziliendelea kushambuliana kwa zamu na mchezo ukazidi kupendeza kutokana na kila upande kupeleka mashambulizi kusaka bao. Mchezo mwingine wa kundi hilo kati ya Lesotho na Cape Verde utafuatia kesho mjini Maseru.
  Kikosi cha Uganda kilikuwa; Denis Onyango, Nico Wakiro Wadada, Godfrey Walusimbi, Juuko Murushid, Hassan Wasswa Mawanda, Khalid Aucho, Denis Iguma, Moses Waiswa, Faruku Miya/ Edrisa Lubega dk87, Emmanuel Arnold Okwi/William Luwagga Kizito dk79 na Joseph Ochaya/Patrick Henry Kaddu dk66.
  Tanzania; Aishi Manula, Hassan Kessy, Gardiel Michael/Farid Mussa dk71, Aggrey Morris, David Mwantika, Abdi Banda, Simon Msuva, Mudathir Yahya, Mbwana Samatta, Frank Domayo/Himid Mao dk77 na Thomas Ulimwengu/Shaaban Iddi dk90.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: TAIFA STARS YALAZIMISHA SARE 0-0 NA UGANDA KAMPALA, SAMATTA AKOSA BAO LA WAZI NAMBOOLE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top