• HABARI MPYA

  Wednesday, September 12, 2018

  SIMBA SC KUONDOKA KESHO MAPEMA TU KUIFUATA NDANDA MTWARA, MECHI JUMAMOSI NANGWANDA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  KIKOSI cha mabingwa wa Tanzania Bara, Simba kinatarajiwa kuondoka kesho kwenda Mtwara kwa ajili ya mchezo wake wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya wenyeji, Ndanda FC.
  Wachezaji wote wanne kati ya watano walioruhusuiwa kwenda kuchezea timu zao za taifa kwenye mechi za Kimataifa wikiendi iliyopita wamerejea kasoro mmoja tu, kiungo Mzambia Cletus Chama ambaye anatarajiwa kuwasili kesho mapema na kuungana na wenzake kwa safari ya Mtwara.
  Lakini Waganda beki Juuko Murshid, mshambuliaji Emmanuel Okwi na Wanyarwanda kiungo Haruna Niyonzima na mshambuliaji Meddie Kagere wamerejea na jana jioni wamefanya mazoezi.
  Kocha Mbelgiji Patrick J Aussems atachukua wachezaji 20 kati ya wote kwa safari ya Mtwara, ambako timu inakwenda kucheza mechi ya kwanza ya ugenini na ya tatu kwa ujumla ya msimu baada ya kushinda mbili za awali nyumbani dhidi ya timu za Mbeya, Tanzania Prisons 1-0 na City 2-0.

  Lakini kiungo Muzamil Yassin aliyeoa wiki iliyopita hatarajiwi kuwa miongoni mwa wachezaji hao kwa sababu yeye ni majeruhi.
  Kwa ujumla, baada ya mapumziko ya kupisha mechi za kimataifa, Ligi Kuu ya Tanzania Bara inarejea wikiendi hii Ijumaa kutakuwa michezo miwili, Mwadui FC na Azam FC Uwanja wa Mwadui Complex, Shinyanga Saa 8:00 mchana na African Lyon na Coastal Union Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam Saa 10:00 jioni.
  Ligi itaendelea Jumamosi Lipuli wakiikaribisha Mtibwa Sugar Uwanja wa Samora mjini Iringa Saa 8:00 mchana, Ndanda na Simba SC Uwanja wa Nangwanda SIjaona Mtwara Saa 10:00 jioni, Tanzania Prisons na Ruvu Shooting Saa 10:00 jioni Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya, Mbao FC na JKT Tanzania Saa 10:00 jioni Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza, KMC na Singida United Saa 10:00 jioni Uwanja wa Taifa na Biashara United na Kagera Sugar Saa 10:00 jioni Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Musoma mkoani Mara.
  Mabingwa wa kihistoria, Yanga SC wao watateremka Uwanja wa Taifa Jumapili Saa 10:00 jioni kumenyana na Stand United, huo ukiwa mchezo wao wa pili tu baada ya ushindi wa 2-1 kwenye mechi ya kwanza dhidi ya Mtibwa Sugar.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SIMBA SC KUONDOKA KESHO MAPEMA TU KUIFUATA NDANDA MTWARA, MECHI JUMAMOSI NANGWANDA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top