• HABARI MPYA

  Tuesday, September 04, 2018

  SIMBA SC KUMENYANA NA AFC LEOPARDS YA KENYA MECHI YA KIRAFIKI JUMAMOSI UWANJA WA TAIFA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  SIMBA SC itamenyana na AFC Leopards ya Kenya katika mchezo wa kirafiki Jumamosi Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
  Huo utakuwa mchezo wa kwanza kuzikutanisha timu hizo baada ya miaka miwili na ushei, kwani mara ya mwisho zilikutana kwenye tamasha la Simba Day, Agosti 8 mwaka 2016 Uwanja wa Taifa pia.
  Katika mchezo huo, Simba SC iliyokuwa ikisherehekea kutimiza miaka 80 iliifunga AFC Leopards 4-0, mshambuliaji Ibrahim Ajibu akifunga mabao mawili, Mrundi Laudit Mavugo na Shizza Kichuya wakifunga bao moja kila mmoja.

  Jons Mkude (katikati) ni miongoni mwa wachezaji wa Simba SC walioondolewa kwenye kikosi cha Taifa Stars

  Kocha wa Simba SC, Mbelgiji Patrick J Aussems anataka kutumia mchezo huo kuwaweka vyema wachezaji wake kufuatia kusimama kwa Ligi Kuu kupisha mechi za kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika wikiendi hii.
  Wachezaji wawili wa Simba SC, beki Juuko Murshid na mshambuliaji Emmanuel Okwi wapo timu ya taifa ya Uganda itakayomenyana na Tanzania Jumamosi na wengine wawili, kiungo Haruna Niyonzima na mshambuliaji Meddie Kagere wapo Rwanda itayomenyana na Ivory Coast mjini Kigali, wakati kipa Aishi Manula yupo Taifa Stars. 
  Simba SC ingekuwa na wachezaji 11 kwenye timu za taifa, kama si kocha Mkuu wa Taifa Stars, Mnigeria, Emmanuel Amunike kuwafukuza wachezaji sita, mabeki; Shomari Kapombe, Erasto Nyoni, Jonas Mkude, Hassan Dilunga, Shiza Kichuya na John Bocco wa Wekundu hao wa Msimbazi kwa utovu wa nidhamu.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SIMBA SC KUMENYANA NA AFC LEOPARDS YA KENYA MECHI YA KIRAFIKI JUMAMOSI UWANJA WA TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top