• HABARI MPYA

    Monday, September 10, 2018

    SAMATTA: SI KITU KIZURI KWA MSHAMBULIAJI KUPOTEZA NAFASI NZURI KAMA ILE

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    NAHODHA wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta amewaomba radhi Watanzania kwa kukosa bao la wazi katika mchezo wa Kundi L kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwakani nchini Cameroon Taifa Stars ikitoa sare ya 0-0 na Uganda Jumamosi Uwanja wa Mandela, Namboole mjini Kampala akisema kwamba hakuwa na bahati.
    Akizungumza jana mjini Dar es Salaam baada ya kikosi cha Taifa Stars kurejea kutoka Kampala, Samatta alisema kwamba amekuwa akifunga mabao katika mazingira magumu mno, lakini  juzi akashindwa kutumia nafasi nyepesi jambo lilimuumiza sana.
     “Mimi ninafikiri huwa nakuwa sina shaka na ubora wangu hususan za ufungaji. Na kitu ambacho nilikuwa nacho pale ni kwamba naenda kufunga, hiyo ilikuwa haina shaka kwamba naweza kufunga. Na ilikuwa ni nafasi nyepesi ukilinganisha na nafasi nyingine ambazo huwa ninafunga,”.
    Mbwana Samatta amewaomba radhi Watanzania kwa kukosa bao la wazi Taifa Stars ikitoa sare ya 0-0 na Uganda Jumamosi  


    “Kwa hiyo naweza kusema sikuwa na bahati labda, inaweza kuwa hivyo ilitokea (juzi) bahati mbaya sijafunga, lakini ninadhani ni kitu ambacho kiliniumiza sana kwa sababu ni nafasi ambayo nilikuwa nikiitafuta katika mchezo mzima niweze kuipata, lakini baada ya kuipata nikashindwa kuitumia,”.
    Samatta amesema kwamba si kitu kizuri kwa mshambuliaji kupoteza nafasi nzuri za aina ile na ndiyo maana usiku wa kuamkia jana hakupata usingizi akikesha anafikiria nafasi ile na kujutia kwa kuipoteza.
    “Siyo kitu kizuri kwa mshambuliaji, ni kitu ambacho kwa kweli kilinifanya nisipate usingizi usikuwa jana (juzi) nikijaribu kuikumbuka ile nafasi nikijaribu kuitafuta kuiangalia, kuirudia rudia nione ni wapi nilishindwa na kwa nini ilikuwa vile,”alisema mshambuliaji huyo wa KRC Genk ya Ligi Kuu ya Ubelgiji.  
    Baada ya sare hiyo, The Cranes inabaki juu kwenye msimamo wa Kundi L ikifikisha pointi nne baada ya kucheza mechi mbili wakati Taifa Stars inaokota pointi ya pili tu katika mechi yake ya pili, wote wakiwa wamecheza nyumbani na ugenini.
    Na kufuatia sare ya 1-1 baina ya wenyeji, Lesotho na Cape Verde jana Uwanja wa Setsoto mjini Maseru, Tanzania sasa ni ya tatu katika kundi hilo.
    Taifa Stars itateremka tena dimbani Oktoba 10, mwaka huu nchini Cape Verde katika mchezo wake wa tatu na wa mwisho wa mzunguko wa kwanza katika kuwania tiketi ya AFCON ya mwakani nchini Cameroon, siku ambayo The Cranes wataialika Lesotho mjini Kampala.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SAMATTA: SI KITU KIZURI KWA MSHAMBULIAJI KUPOTEZA NAFASI NZURI KAMA ILE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top