• HABARI MPYA

  Friday, September 14, 2018

  REFA WA NAMIBIA ADAI RWANDA WALITAKA KUMHONGA AWABEBE MECHI NA IVORY COAST

  Na Mwandishi Wetu, KIGALI
  VIONGOZI wawili wa soka wa Rwanda wamewekwa rumande kwa tuhuma za kutaka kumhonga refa Jackson Pavaza wa Namibia aisaidie timu ya taifa ya nchi hiyo, Amavubi kushinda dhidi ya Ivory Coast.
  Shirika la Uchunguzi la Rwanda (RIB) Alhamisi jana lilisema kwamba lilikuwa linawashikilia viongozi wa Shirikisho la Soka la nchi hiyo (FERWAFA), Katibu Mkuu Francois Regis Uwayezu na Kamishna wa Mashindano Eric Ruhamiriza kwa tuhuma hizo.
  Wanadaiwa kutaka kumhonga fedha refa Pavaza aisaidie Amavubi kushinda dhidi ya Tembo wa Ivory Coast mechi ya Kundi H kuwania tiketi ya Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika iliyofanyika Jumapili iliyopita Uwanja wa Nyamirambo mjini Kigali.

  Refa wa Jackson Pavaza (katikati) akiwaongoza wachezaji wa Rwanda na Ivory Coast kuingia uwanjani Jumapili mjini Kigali

  Ivory Coast ilishinda 2-1, mabao yake yakifungwa na Jonathan Kodjia dakika ya 45 na Max-Alain Gradel dakika ya 49, wakati la Rwanda lilifungwa na mshambuliaji wa Simba SC, Meddie Kagere dakika ya 66.
  “Tunawahoji. RIB ina uwezo wa kuchunguza uhalifu wowote uliojitokeza katika jamii
  ,”amesema Msemaji wa RIB, Modeste Mbabazi.
  Vyombo vya Habari vya Namibian Jumanne viliandika kwamba Pavaza ametuma taarifa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) akiwashitaki viongozi hao walijaribu kumpa hongo ili aisaidie Amavubi.
  “Fedha zilikuwa kwenye bahasha. Sikujaribu hata kuhesabu au kuziona zilikuwa kiasi gani. Niliwaambia kwamba sipokei zawadi yoyote kutoka kwa mtu yeyote kwa mujibu wa taratibu za CAF,” amenukuliwa Pavaza akisema.
  Lakini FERWAFA imekana madai hayo. “Tumeshitushwa na madai yaliyotolewa na refa wa Namibia, Jackson Pavaza akisema kwamba alitaka kuhongwa aisaidie Rwanda katika mechi ya kufuzu 2019 baina ya Rwanda na Ivory Coast uliofanyika Septemba 9, 2018 Uwanja wa Kigali,” imesema Ferwafa katika taarifa yake ya Jumatano.
  FERWAFA imesema kwamba ililipa dola 247 pekee kwa gharama za Pavaza na wenzake watatukwa mujibu wa kanuni za AFCON.
  Pamoja na hayo, marefa hao walisema kulikuwa kuna gharama zaidi za kulipiwa katikam safari yao ya kwenda Kigali. Hakuna refa mwingine alieibuka au kujitokeza kukataa au kuthibitisha maelezo ya Pavaza.
  Bado CAF haijatoa tamko lolote juu ya hilo ingawa ikithibitika kweli maofisa hao walitaka kumhonga refa, Rwanda inaweza kupigwa faini au kuondolewa kwenye mbio za kuwania tiketi ya Afcon ya mwakani Cameroon.
  Kipigo cha Jumapili kinaifanya Amavubi icheze mechi mbili bila ushindi katika Kundu H, ambako Guinea inaongoza.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: REFA WA NAMIBIA ADAI RWANDA WALITAKA KUMHONGA AWABEBE MECHI NA IVORY COAST Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top