• HABARI MPYA

    Saturday, September 15, 2018

    PLUIJM ASIKITIKIA SARE YA JANA MWADUI, ASEMA; "TULISTAHILI KUIBUKA NA USHINDI"

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KOCHA Mkuu wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Hans van der Pluijm, ameweka wazi kuwa walistahili kushinda kwenye mchezo uliomalizika kwa sare ya bao 1-0 jana dhidi ya Mwadui.
    Mchezo huo uliofanyika Uwanja wa Mwadui, ilishuhudiwa Azam FC ikijipatia bao lake kupitia kwa kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’ na kujipatia pointi moja ugenini iliyoifanya kukaa kileleni mwa msimamo wa ligi ikifikisha pointi saba sawa na Mbao.
    Pluijm amesema kwamba walistahili ushindi kutokana na timu yake kucheza vema huku akidai walijisahau dakika moja na wapinzani wao kutumia nafasi hiyo kusawazisha bao na kufanya mchezo kuisha kwa sare.

    Hans van der Pluijm (kulia) akiwa na Msaidizi wake, Juma Mwambusi (kushoto) jana Mwadui

    “Tulicheza vizuri sana, kwangu mimi kwa dakika 90 unatakiwa kucheza kwa umakini na nidhamu ya mbinu na tulijisahau dakika moja, nidhamu yetu na namna tulivyopaswa kucheza na wakapata bao ambapo kwa maoni yangu hatukurudi nyuma haraka na kipa alifanya uamuzi kwa kuchelewa, hiyo ikawapa nafasi ya kutufunga.
    “Mbali na hayo, walikataa bao lililofungwa na Danny Lyanga lakini kwa sisi wote lilikuwa ni bao halali na kawaida huwa sitakagi kuzungumza sana kuhusu waamuzi kwa sababu yote ni baada ya mchezo na imeshatokea,” alisema.
    Pluijm alikisifia kikosi chake kwa kucheza vizuri kwa kueleza kuwa; “Tulicheza vizuri sana kwa kumiliki mchezo wote na tukio la mara moja walitumia kufunga na tumesikitishwa sana kwa upande wetu kuacha pointi mbili ugenini.”
    Azam FC inatarajia kubakia ugenini kucheza na Biashara United Jumatano ijayo mkoani Mara, akizungumzia mchezo huo Mholanzi huyo amesema wanaenda na nguvu zote kuhakikisha wanavuna pointi tatu.
    “Jambo la muhimu sana ni kucheza kwa ari na haraka sana na kujaribu kwenda kufunga na kama ukifunga bao moja zaidi mpinzani wako utashinda mechi zako na hilo ndilo tunatakiwa kulifanya, tunatakiwa kutumia nafasi zetu nadhani tunauzoefu zaidi ya mpinzani wetu tunawapa heshima zote, lakini tunaenda huko na nguvu kwa ajili ya pointi tatu,” alisema.
    Kikosi cha Azam FC kinatarajia kuondoka mjini Shinyanga kesho saa 12 asubuhi kuelekea mkoani Mara, tayari kujiandaa kuvaana na timu hiyo inayotumia Uwanja wa Karume mjini Musoma.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: PLUIJM ASIKITIKIA SARE YA JANA MWADUI, ASEMA; "TULISTAHILI KUIBUKA NA USHINDI" Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top