• HABARI MPYA

    Monday, September 10, 2018

    MENEJA WA SIMBA SC AFUNGIWA MWAKA NA FAINI MILIONI 4 AKIDAIWA KUSABABISHA AKINA KICHUYA WASIINGIE KAMBINI STARS

    Na Lulu Ringo, DAR ES SALAAM
    KAMATI ya Maadili ya Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) imemfungia Meneja wa Simba SC, Richard Robert kujihusisha na soka kwa mwaka mmoja na faini ya Sh. Milioni 4.
    Hiyo ni baada ya Kamati hiyo chini ya Mwanyekiti wake, Hamidu Mbwezeleni kumkuta na makosa mawili ya kuihujumu timu ya taifa na kushindwa kutii agizo la TFF – lakini atatumikia kifungo cha miezi sita kutokana na adhabu zake kwenda sambamba. 
    Mbwezeleni amesema katika mkutano na Waandishi wa Habari leo kwamba adhabu ya kuhujumu ni kwa mujibu wa kifungu 5 (2), kifungu cha 6 (c) na (h) vya Kanuni za Maadili za TFF toleo la 2013 na adhabu ya kutotii maagizo ya TFF ni kwa mujibu wa kifungu cha 41 (8) cha kanuni za ligi kuu toleo la 2013.

    Meneja wa Simba SC, Richard Robert (kushoto) amefungiwa mwaka mmoja kujihusisha na soka 

    Robert anadaiwa kuwa sababu ya wachezaji wa Simba SC, mabeki Shomari Kapombe, Erasto Nyoni, viungo Jonas Mkude, Hassan Dilunga, Shiza Kichuya na mshambuliaji John Bocco wa Simba kutojiunga na kambi ya timu ya taifa, Taifa Stars wiki iliyopita kwa ajili ya mchezo dhidi ya Uganda Jumamosi.
    Kocha mpya wa Tafa Stars, Mnigeria, Emmanuel Amunike aliwaondoa wachezaji hao sita wa klabu bingwa ya Tanzania pamoja na kiungo wa Yanga, Feisal Salum baada ya kukaidi kuripoti mwanzoni mwa wiki iliyopita.
    Lakini baada ua uchunguzi wake TFF juu ya sakata hilo, imemshushia rungu Meneja huyo wa Simba SC, siku mbili tu baada ya Taifa Stars kulazimisha sare ya 0-0 na Uganda mjini Kampala.
    Baada ya sare hiyo, The Cranes inabaki juu kwenye msimamo wa Kundi L ikifikisha pointi nne baada ya kucheza mechi mbili wakati Taifa Stars inaokota pointi ya pili tu katika mechi yake ya pili, wote wakiwa wamecheza nyumbani na ugenini.
    Na kufuatia sare ya 1-1 baina ya wenyeji, Lesotho na Cape Verde jana Uwanja wa Setsoto mjini Maseru jana, Tanzania inabaki nafasi ya tatu katika kundi hilo.
    Taifa Stars itateremka tena dimbani Oktoba 10, mwaka huu nchini Cape Verde katika mchezo wake wa tatu na wa mwisho wa mzunguko wa kwanza katika kuwania tiketi ya AFCON ya mwakani nchini Cameroon, siku ambayo The Cranes wataialika Lesotho mjini Kampala.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MENEJA WA SIMBA SC AFUNGIWA MWAKA NA FAINI MILIONI 4 AKIDAIWA KUSABABISHA AKINA KICHUYA WASIINGIE KAMBINI STARS Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top