• HABARI MPYA

  Wednesday, September 19, 2018

  MBEYA CITY YAISHINDILIA RUVU SHOOTING 4-2, NDANDA YAIBWAGA MTIBWA NANGWANDA, AZAM FC SARE TENA ‘MIKOANI’

  Na Mwandishi Wetu, MBEYA
  TIMU ya Mbeya City imefanya mauwaji katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya kuichapa Ruvu Shooting ya Pwani mabao 4-2 katika mchezo wa jioni ya leo Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.
  Eliud Ambokile alifunga mabao mawili ndani ya dakika tatu, ya 20 na 23 na Mbeya City ikaenda kupumzika inaongoza 2-0, kabla ya Khamis Mcha kuifungia Ruvu Shooting dakika ya 52.
  Iddi Suleiman ‘Nado’ akafunga dakika ya 60 na Peter Mapunda akaongeza lingine dakika ya 75 Mbeya City wakifikisha mabao manne, kabla ya Said Dilunga kuifungia tena Ruvu dakika ya 90.
  Mechi nyingine ya leo, Ndanda FC imedhihirisha msimu huu imeimarika baada ya kuichapa Mtibwa Sugar mabao 2-1 katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara.

  Mbeya City imeichapa Ruvu Shooting ya Pwani 4-1 Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya leo

  Haukuwa ushindi mwepesi kwa wenyeji hao, kwani walilazimika kutoka nyuma kwa bao la mapema la mshambuliaji mwenye mwili mkubwa, Stahmili Mbonde dakika ya 23 ili kubeba pointi tatu za mchezo huo.
  Na shujaa wa Ndanda FC leo alikuwa ni mshambuliaji mpya, Vitalis Mayanga aliyewika Stand United ya Shinyanga msimu uliopita, ambaye leo amefunga mabao yote ya timu ya Mtwara dakika za 40  na 73.
  Ndanda FC sasa inafikisha pointi saba baada ya kucheza mechi tano, wakati Mtibwa Sugar wanabaki na pointi zao saba wakifikisha mechi tano.
  Mechi nyingine za Ligi Kuu leo, Biashara United imelazimishwa sare ya pili mfululizo nyumbani, baada ya kumaliza dakika 90 bila kufungana na Azam FC Uwanja wa Karume, Musoma mkoani Mara, wakitoka kutoa 1-1 na Kagera Sugar mwishoni mwa wiki.
  Azam FC nayo hiyo inakuwa sare ya pili mfululizo kwake, na zote ugenini kwani mechi iliyopita ilitoka 1-1 na Mwadui FC huko Kishapu mkoani Shinyanga.    
  Mwadui FC imelazimisha sare ya 1-1 na JKT Tanzania Uwanja wa Mwadui Complex mjini Shinyanga. Revocatus Richard alianza kuifugia Mwadui FC dakika ya 66, kabla ya Hassan Matelema kuisawazishia JKT dakika ya 87.
  Mwadui FC inafikisha pointi mbili baada ya kucheza mechi nne, wakati JKT inafikisha pointi tisa katika mechi yake ya tano.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MBEYA CITY YAISHINDILIA RUVU SHOOTING 4-2, NDANDA YAIBWAGA MTIBWA NANGWANDA, AZAM FC SARE TENA ‘MIKOANI’ Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top