• HABARI MPYA

    Monday, September 10, 2018

    MANENO YA PELE YAMETIMIA MAPEMA KABISA, AKADEMI YA AZAM FC SASA NDIYO GHALA LA VIPAJI VYA WANASOKA TEGEMEO TANZANIA

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    AKIWA katika viunga vya Azam Complex, Chamazi mjini Dar es Salaam Novemba 5, mwaka 2012, Mwanasoka bora wa zamani Afrika, Abedi Ayew Pele alisema; “Kama una akademi nzuri kama hii, kwa nini uchukue mchezaji kutoka Ghana, hii nchi yenu ina watu zaidi ya Milioni 40, mnaweza kutengeneza wachezaji wengi wazuri na nyinyi mkauza Ulaya,”.
    Pele alisema hayo alipokuwa katika ziara ya kutembelea akademi ya Azam FC akiongozwa na aliyekuwa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Leodegar Tenga, mchezaji mwenzake wa zamani wa kimataifa.
    Pele aliisifia mno Akademi ya Azam na akasema italeta matunda makubwa katika soka ya Tanzania baadaye na akaitabiria Azam FC itakuwa klabu kubwa yenye hadhi sawa na Manchester United ya England kutokana na uwekezaji wake huo mzuri.
    Nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta aliyeinua mkono akiwa na wachezaji zao la akademi ya Azam FC Gardiel Michael na Simon Msuva (kulia) na Himid Mao (kushoto) 

    Akasema akademi ya Azam ni nzuri na bora kuliko hata akademi yake. “Kwetu tuna akademi nyingi, lakini nyingi ni za wawekezaji wa nje (klabu za Ulaya), lakini hii ni ya Azam, safi sana. Akademi yangu ni ndogo tu, haiifikii hii kwa ubora, nami nina ndoto za kufanya kitu kama hiki, nadhani nitajifunza mengi kutoka kwa Azam,”alisema Pele.  
    Novemba 5, mwaka huu itatimia miaka sita tangu Pele azuru nchini na kusema maneno hayo – lakini mwishoni mwa wiki maneno ya mshambuliaji huyo wa zamani wa kimataifa wa Ghana na klabu ya Olympique Marseille ya Ufaransa yalijidhihirisha.
    Ilikuwa ni katika mchezo wa Kundi L kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwakani nchini Cameroon kati ya Tanzaniia na wenyeji, Uganda Jumamosi Uwanja wa Mandela, Namboole mjini Kampala uliomalizika kwa sare ya 0-0.
    Katika wachezaji 18 wa Tanzania walioshriki mchezo huo, tisa wametokea akademi ya Azam FC ambao ni kipa Aishi Manula, beki Gardiel Michael, viungo Mudathir Yahya, Simon Msuva, Farid Mussa, Himid Mao na washambuliaji Shaaban Iddi Chilunda, Rashid Mandawa na Yahya Zayid.
    Na kwa ujumla kwenye kikosi cha Taifa Stars kilicholazimisha sare ya 0-0 na Uganda mjini Kampala kulikuwa kuna wachezaji 12 walitokea na kupita Azam FC.

    Gwiji wa soka Afrika, Abedi Pele akiwa na wachezaji wa Akademi ya Azam FC Novemba 5, mwaka 2012 Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam

    Ukiondoa tisa hawa Manula, Gardiel, Mudathir, Msuva, Farid, Himid, Chilunda, Mandawa na Zayid ambao hakuna shaka ni zao la Azam Akademi, kulikuwa kuna wachezaji wengine watatu wa kikosi cha sasa Azam FC ambao wamedumu klabuni kwa muda mrefu – hao ni mabeki Aggrey Morris, David Mwantika na kiungo Frank Domayo. 
    Na kama kocha Mnigeria, Emmanuel Amunike asingewaondoa nyota sita wa Simba SC kwa utovu wa nidhamu – idadi ya wachezaji waliotokea Azam FC ingeongezeka kwa wachezaji watatu zaidi ambao ni mabeki Shomari Kapombe, Erasto Nyoni na mshambuliaji John Bocco.
    Leodegar Tenga, beki wa zamani wa kimataifa wa Tanzania aliona mbali alipompeleka Pele kutembelea akademi ya Azam pale Chamazi, kwani miaka sita baadaye matunda ya akademi hiyo ni faida kubwa kwa soka ya Tanzania.
    Inasikitisha viongozi wa sasa wa TFF chini ya Rais, Wallace Karia wakati Rais wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Ahmad alipokuwa nchini waliweza kumpeleka hadi kwenye tafrija za usiku, lakini hawakumfikisha kwenye ghala la kuzalisha vipaji vya wanasoka tegemeo Tanzania.
    Ni maono tu ya kwao yapo tofauti na ya Tenga – lakini faida za akademi ya Azam ni pana mno na zinavuka na kuingia hadi kwenye soka ya nchi hii kwa ujumla, kwani kwa sasa ni nadra katika klabu ya Ligi Kuu kati ya zote 20 kukosekana mchezaji aliyeibuliwa Chamazi. 
    Hiyo ni hadi kwa vigogo Simba ambao ndiyo wanao hao akina Manula na Yanga ambao wanao akina Gardiel Michael, kipa Ramadhan Kabwili na mshambuliaji Yohanna Nkomola.
    Bado akademi ya Azam FC inategemewa mno kwa kwa wachezaji wa timu za vijana kuanzia chini ya umri wa miaka kuendele U15, U17, U20. 
    Na hapo tayari vijana wawili, Farid na Chilunda wapo Ulaya katika klabu ya CD Tenerife ya Daraja la Kwanza Hispania, Rashid Mandawa yupo BDF XI ya Botswana, Himid Mao yupo Petrojet ya Ligi Kuu ya Misri na Simon Msuva yupo Difaa Hassan El-Jadidi ya Morocco baada ya kutamba na mabingwa wa kihistoria wa Tanzania, Yanga SC.  
    Mapema kabisa maneno ya gwiji wa soka barani, Abeid Pele yametimia kuhusu akademi ya Azam FC na sasa imekuwa ghala la kuzalisha vipaji vya wanasoka tegemeo nchini ambao tayari wameanza kuvuka mipaka ya Tanzania na kufika hadi Ulaya.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MANENO YA PELE YAMETIMIA MAPEMA KABISA, AKADEMI YA AZAM FC SASA NDIYO GHALA LA VIPAJI VYA WANASOKA TEGEMEO TANZANIA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top