• HABARI MPYA

    Friday, September 07, 2018

    KUZIONA SIMBA NA AFC LEOPARDS KESHO JIONI UWANJA WA TAIFA NI SH. 5,000 HADI 15,000 VIP A

    Na Lulu Ringo, DAR ES SALAAM
    KIINGILIO cha chini katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa wa klabu ya wenyeji, Simba SC na AFC Leopards ya Kenya utakaofanyika Jumamosi kitakuwa Sh. 5,000 kwa majukwaa ya mzunguko.
    Hayo yamesemwa na Msemaji wa Simba SC, Hajji Sunday Manara katika mkutano na Waandishi wa Habari leo makao makuu ya klabu, Mtaa wa Msimbazi mjini  Dar es Salaam.
    Manara ametaja viingilio vingine katika mchezo huo utakaoanza Saa 12:00 jioni vitakuwa Sh. 15,000 kwa jukwaa la VIP A na Sh. 10,000 kwa jukwaa la VIP B.
    Huo utakuwa mchezo wa kwanza kuzikutanisha timu hizo baada ya miaka miwili na ushei, kwani mara ya mwisho zilikutana kwenye tamasha la Simba Day, Agosti 8 mwaka 2016 Uwanja wa Taifa pia.

    Katika mchezo huo, Simba SC iliyokuwa ikisherehekea kutimiza miaka 80 iliifunga AFC Leopard 4-0, mshambuliaji Ibrahim Ajibu akifunga mabao mawili, Mrundi Laudit Mavugo na Shizza Kichuya wakifunga bao moja kila mmoja.
    Kocha wa Simba SC, Mbelgiji Patrick J Aussems anataka kutumia mchezo huo kuwaweka vyema wachezaji wake kufuatia kusimama kwa Ligi Kuu kupisha mechi za kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika wikiendi hii.
    Wachezaji wawili wa Simba SC, beki Juuko Murshid na mshambuliaji Emmanuel Okwi wapo timu ya taifa ya Uganda itakayomenyana na Tanzania Jumamosi na wengine wawili, kiungo Haruna Niyonzima na mshambuliaji Meddie Kagere wapo Rwanda itayomenyana na Ivory Coast mjini Kigali, wakati kipa Aishi Manula yupo Taifa Stars. 
    Simba SC ingekuwa na wachezaji 11 kwenye timu za taifa, kama si kocha Mkuu wa Taifa Stars, Mnigeria, Emmanuel Amunike kuwafukuza wachezaji sita, mabeki; Shomari Kapombe, Erasto Nyoni, Jonas Mkude, Hassan Dilunga, Shiza Kichuya na John Bocco wa Wekundu hao wa Msimbazi kwa utovu wa nidhamu.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KUZIONA SIMBA NA AFC LEOPARDS KESHO JIONI UWANJA WA TAIFA NI SH. 5,000 HADI 15,000 VIP A Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top