• HABARI MPYA

  Sunday, September 16, 2018

  KATIKA MAMILIONI YA MFUKO WA JIMBO, WABUNGE WANATUMIA KIASI GANI KUSAIDIA MICHEZO NA WANAMICHEZO?

  MIAKA ya nyuma, kiki ilikuwa ina maana shuti katika mchezo wa soka – lakini kwa sasa kiki ina maana nyingine kabisa kwa kifupi umaarufu.
  Vijana wa kizazi cha sasa wanaelekwa kiki kama umaarufu tu- ambao huja kwa namna yoyote, kutokana na kazi nzuri, au wakati mwingine mtu kuutafuta kwa kufanya vitu, au mambo yatakayoteka hisia za watu, yawe mabaya mazuri.
  Wakati mwingine mtu hutafuta kiki kwa kuchokoza, kutukana, hata kujiingiza kwenye matatizo ya vyombo vya doka ili achukuliwe hatua tu apambe vichwa vya habari na kupata umaarufu.
  Lakini Jumamosi iliyopita, bondia Hassan Mwakinyo kutoka Tanga alimshinda kwa Technical Knockout (TKO) Muingereza, Sam Eggington Uwanja wa Arena Birmingham, zamani Barclaycard Arena mjini Birmingham, England.

  Mwakinyo aliushitua ulimwengu baada ya kummaliza Eggington kwa TKO katika raundi ya pili kuelekea pambano kuu jana kati ya Muingereza, Amir Khan na Samuel Vargas Colombia anayeishi Canada. Khan alishinda kwa pointi za majaji wote.
  Bondia huyo aliondoka nchini katika mazingira magumu kwenda Uingereza na kutokana na kukosa fedha za kulipia visa, alilazimika kumkopa mwanafunzi fedha yake ada.
  Na hiyo ni kutokana na kupewa taarifa siku chache kabla ya pambano hilo, kufuatia bondia wa awali aliyepangiwa kupigana na Eggington kujitoa.
  Ushindi huo uliokuja katika kipindi ambacho mchezo wa ngumi umesinzia kidogo, umeyarejeshea umaarufu wake masumbwi nchini na haikuwa ajabu Mwakinyo alipofikia Bungeni Dodoma juzi akitokea Uingereza, badala ya kwenda moja kwa moja Tanga.
  Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa alimpongeza Mwakinyo kwa ushindi huo na kumtakia mafanikio zaidi katika mapambano yake yajayo. 
  “Nimpongeze pia mwanamasumbiwi wa Kitanzania, Hassan Mwakinyo kwa kumchapa bondia Muingereza, Sam Eggington kwenye raundi ya pili ya pambano lao la masumbwi lililofanyika huko Birmingham nchini Unigereza. Hongereni sana wanamichezo wetu na endelezeni moyo huo wa kizalendo mliouonyesha katika kulitangaza taifa letu,”alisema Waziri Mkuu.
  Baada ya maelezo hayo, Spika wa Bunge Job Ndugai akamtambulisha Mwakinyo aliyealikwa Bungeni kwa ajili ya pongezi na Wabunge wote wakakubali kumchangia Sh. 20,000 kila mmoja kwa ajili ya pongezi.
  Spika Ndugai alisema alikuwa hajui kama Tanga kuna mabondia, wakati ukweli ni kwamba mkoa huo ni kati ya sehemu ambazo zinaoongoza kwa kutoa mabondia bora kihistoria tangu enzi za akina Matumla Ally, baba yao akiwa Rashid, Ally (marehemu), Hajji, Hassan, Mbwana, Mkwanda na Karim.
  Mabondia wengine maarufu kuwahia kutokea Tanga ni Charles Mhilu ‘Spinks’, Mambeya Bakari pamoja na bingwa wa zamani wa dunia wa WBU, Magoma Shaaban, ambaye sasa ni marehemu pia.
  Baaada ya ushindi huo, Mwakinyo atapanda tena ulingoni Oktoba 20, kuzipiga na mwenyeji Wanik Awdijan ukumbi wa Alex Sportcentrum mjini Nuremberg, Ujerumani katika pambano la kuwania taji la vijana la IBF uzito wa Middle.
  Litakuwa pambano lake la nne kupigana nje ya Tanzania, kwani kabla ya kumpiga Eggington alimshinda pia kwa TKO Anthony Jarmann wa Namibia Agosti 8, mwaka jana ukumbi wa Grand Palm Hotel mjini Gaborone nchini Botswana kabla ya Desemba 2, mwaka jana Mwakinyo kupoteza kwa pointi mbele ya mwenyeji, Lendrush Akopian ukumbi wa Krylia Sovetov mjini Moscow, Urusi. 
  Hapana shaka ushindi wa Mwakinyo unatudhihirishia huyo ni bondia bora anayeweza kupata mafanikio zaidi iwapo atapewa sapoti.
  Imekuwa kawaida ya wanasiasa wa nchi hii kupandia mafanikio ya wanamichezo yaliyotokana na juhuzi zao binafsi na kupitia katika mazingira magumu kama ilivyo kwa Mwakinyo.
  Lakini wamekuwa wazito kuwasaidia wanamichezo wasiojiweza katika maeneo yao kutimiza ndoto zao za kupata mafanikio na kuitangaza nchi yao kupitia michezo.
  Amini kuna akina Mwakinyo wengi katika nchi hii, lakini kutokana na kukosa sapoti hawafiki popote na wengine wanaishia kufanya uhalifu, kubeba dawa za kulevya, kuwa wezi, majambazi tu kwa kukosa wa kuwaendeleza kuwasaidia kutimiza ndoto zao kupitia michezo.
  Kila Mbunge kati ya waliokuwepo Bungeni Dodoma wakati Mwakinyo anapongezwa na kuchanga Sh. 20,000 ajiulize anafanya nini katika jimbo lake kusaidia wanamichezo na michezo zaidi ya kufanya mashindano ya ujanja ujanja ya kampeni, au kugawa vifaa vya michezo kikampeni. 
  Inafahamika kuna fedha za Mfuko wa Jimbo ambao kila Mbunge hupatiwa kwa shughuli za maendeleo ya jimbo lake wastani wa Sh. Milioni 30 hadi 60 kulingana na ukubwa wa jimbo, lakini kila Mbunge anatenga kiasi gani kwa maendeleo ya michezo pekee?
  Au ni hadi kampeni zikikaribia ananunua jezi na mipira kwenda kugawa kwenye timu za mtaani ili kujipendekeza apigiwe kura?
  Wiki hii Spika Ndugai alisema asilimia 80 ya Wabunge wa Bunge la 11 ni wenye umri wa kuanzia miaka 40 kuendelea na Mbinge mdogo kuliko wote ni Halima Bulembo mwenye umri wa miaka 27 na kwamba ndilo Bunge lenye wasomi zaidi kihistoria, likiwa na Wabunge wenye Shahada za Uzamivu (PhD) 29, kati ya hizo 27 zikiwa zinamilikiwa na wabunge wa CCM, moja mbunge wa CHADEMA na moja mbunge wa CUF.
  Hii inajieleza kwamba sasa tuna Bunge lenye Wabunge weledi kutokana na sifa zao za umri na elimu ambao wanaweza kuwa wananua umuhimu wa kusaidia michezo na michezo katika majimbo yao.
  Kwa sababu tatizo sugu katika nchi hii ni ajira kwa vijana, ambao wengi wao ndiyo wanakimbilia kujiajiri kwenye michezo – na Wabunge wetu weledi wa Bunge la 11 wanalijua fika hilo.
  Wakati umefika sasa Wabunge wetu wajikite kwenye kusaidia michezo na wanamichezo katika majimbo yao ili kuibua akina Mwakinyo wengine wengi sambamba na nyota wa michezo mingine, ikiwemo Riadha. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: KATIKA MAMILIONI YA MFUKO WA JIMBO, WABUNGE WANATUMIA KIASI GANI KUSAIDIA MICHEZO NA WANAMICHEZO? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top