• HABARI MPYA

    Monday, September 17, 2018

    KAGERE AWA MCHEZAJI BORA WA KWANZA WA MWEZI WA MSIMU LIGI KUU

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Rwanda mwenye asili ya Uganda, Meddie Kagere amekuwa Mchezaji Bora wa kwanza wa mwezi wa Ligi Kuu msimu wa 2018/2019.
    Hiyo ni baada ya mshambuliaji huyo aliyejiunga na Simba SC Julai mwaka huu akitokea Gor Mahia ya Kenya kutangazwa Mchezaji Bora wa Agosti wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
    Kagere aliyewahi kuchezea Rayon Sport ya kwao, Rwanda ameshinda tuzo hiyo baada ya kuisaidia Simba SC kushinda mechi mbili za Ligi Kuu ya Bara dhidi ya timu za Mbeya, Tanzania Prisons akifunga bao moja katika ushindi wa 1-0 na Mbeya City akifunga mabao mawili katika ushindi wa 2-0. 
    Na kwa sababu hiyo, Kagere amewashinda wapinzani wake wawili, Joseph Mahundi wa Azam na Ompar Mponda wa Kagera Sugar alioingia nao fainali ambao kila mmoja alifunga mabao mawili mwezi huo.

    Meddie Kagere amekuwa Mchezaji Bora wa kwanza wa mwezi wa Ligi Kuu msimu wa 2018/2019 

    Kihistoria, Kagere aliibukia Mbale Heroes FC ya kwao, Uganda mwaka 2004 ambako alicheza hadi mwaka 2006 alipohamia Rwanda.
    Klabu yake ya kwanza ilikuwa ni ATRACO FC alikocheza kwa msimu mmoja kabla ya mwaka 2007 kuhamia Kiyovu Sports alikodumu hadi 2008 akahamia Mukura Victory ambako alidumu hadi 2010 alipojiunga na Polisi. 
    Na akiwa Polisi ndipo akashawishiwa kuchukua uraia wa Rwanda ili achezee timu ya taifa ya nchi hyo jambo ambalo alilikubali na tangu mwaka 2011 amekuwa akiichezea Amavubi. Polisi alidumu kwa miaka miwili kabla ya mwaka 2012 kuchukuliwa Esperance Sportive de Zarzis ya Tunisia.
    Alicheza Tunisia kwa mwaka mmoja kabla ya kurejea Rwanda kujiunga tena na Polisi mwaka 2013 ambako alicheza kwa mwaka mmoja na kuhamia Rayon mwaka 2014 ambayo mwaka 2015 ilimuuza KF Tirana ya Albania alikocheza hadi mwaka 2015 akajiunga na Gor Mahia ambako ameondoka Julai kuja Simba SC.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KAGERE AWA MCHEZAJI BORA WA KWANZA WA MWEZI WA MSIMU LIGI KUU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top