• HABARI MPYA

  Tuesday, September 11, 2018

  HABIB KIYOMBO KUWAKUTANISHA MEZANI SINGIDA UNITED NA MAMELODI SUNDOWNS

  Na Sada Salmin, DAR ES SALAAM
  KLABU ya Singida United inatarajiwa kufanya mazungumzo na Mamelodi Sundowns ya Afrika juu ya mshambuliaji chipukizi, Habib Hajji Kiyombo. 
  Kiyombo amerejea nchini jana kutoka Afrika Kusini baada ya karibu mwezi mzima wa na mabingwa wa zamani wa Afrika, Mamelodi kwa majaribio.
  Na akizungumza na Bin Zubeiry Sports – Online leo, Mkurugenzi wa Singida United, Sanga Festo amesema kwamba Mamelodi imevutiwa na mchezaji huyo na inamuhitaji ahamishie huduma zake Afrika Kusini.
  Sanga amesema kwamba Kiyombo alipokuwa Afrika Kusini alianzia majaribio yake katika timu ya vijana kwa siku 10 ambako alipoonyesha uwezo akapandishwa kikosi cha kwanza kwa siku 10 nyingine, ambako pia alifanya vizuri.
  Sanga Festo (kulia) akiwa na Habib Kiyombo wakati wanamsajili kijana huyo Juni mwaka huu

  “Wamependezewa na huduma ya mchezaji, wamependezewa na umri alionao, lakini pia kwa kiwango alichonacho, nidhamu na vile ambavyo amevionyesha uwanjani wamefurahishwa sana na Habib Kiyombo. Na kimsingi wametuahidi mchezaji huyu watahitaji kufanya mazungumzo ya kina na sisi, ambayo tunayasubiri,” amesema Sanga.
  Amesema kikubwa ambacho wamefurahia ni kwamba mchezaji Habib Kiyombo hakupata tatizo lolote la kiafya katika kipindi chote alichokuwa Afrika Kusini na amerejea salama tayari kuendelea na majukumu yake Singida United. 
  Mkurugenzi huyo amesema kwamba Kiyombo bado ni kijana mdogo na safari ndefu kisoka na wao kama klabu hawatakuwa tayari kuzima ndoto zake kwa namna yoyote ile, watamruhusu kuondoka mambo yake yakiiva.
  Amesema na hiyo si kwa Kiyombo tu, bali kwa mchezaji yeyote wa Singida United atakayepata timu nje milango iko wazi. Amesema kwa sasa kuna ofa za wachezaji wengine wawili wanatakiwa nje ya nchi na mmoja amekwishakwenda Jamhuri ya Czech watamtaja baadaye.
  “Sisi tunamtakia kila la heri kama viongozi, kama wazalendo, kama wadau wa mpira, tunaamini kabisa, Habib akifanikiwa, taifa limefanikiwa, Habib akifanikiwa Singida United imefanikiwa,”amesema.  
  Habib amejiunga na Singida United Juni mwaka huu akitokea Mbao FC ya Mwanza ambayo ndiyo ilimuibua na kumpambanua kama mkali wa kufunga mabao akijipatia umaarufu zaidi baada ya kufunga dhidi ya vigogo, Simba na Yanga.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: HABIB KIYOMBO KUWAKUTANISHA MEZANI SINGIDA UNITED NA MAMELODI SUNDOWNS Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top