• HABARI MPYA

    Tuesday, September 11, 2018

    GWIJI WA SIMBA SC, MTEMI RAMADHANI ACHUKUA FOMU KUGOMBEA UENYEKITI WA KLABU NOVEMBA 3

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KIUNGO wa zamani wa Simba SC, Mtemi Ramadhani amejitokeza kuwania Uenyekiti wa klabu hiyo kama mmoja wagombea wawili tu wa nafasi hiyo, mwingine Swedi Nkwabi.
    Mchezaji huyo wa zamani wa kimataifa wa Tanzania ana uzoefu mkubwa wa uongozi wa soka, baada ya kupitia kwenye nafasi mbalimbali, lakini nyingi za kuteuliwa.
    Ameshika nyadhifa mbalimbali ndani ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) chini ya viongozi tofauti na mara ya mwisho alikuwepo chini ya Rais Leodegar Chillah Tenga, mchezaji mwenzake wa zamani wa Taifa Stars.
    Jana ndiyo ilikuwa siku ya mwisho ya kuchukua fomu na orodha kamili ya wagombea waliojitokeza ni 21 kwa nafasi zote, wawili wa Uenyekiti, wawili wa Ujumbe kwa Wanawake na 17 kwa Wajumbe wa Bodi.

    Mtemi Ramadhani (kushoto) akiwa nyota wa sasa klabu ya Simba, Shiza Kichuya

    Nafasi za Wajumbe wa Wanawake waliojitokeza ni Jasmin Badar Soud na Asha Ramadhani Baraka, wakati Wajumbe wa Bodi ni Hussein Kitta Mlinga, Iddi Noor Kajuna, Dk. Zawadi Ally Kadunda, Mohammed Wandi, Suleiman Haroub Said, Abdallah Rashid Mgomba na Christopher Kabalika Mwansasu.
    Wengine ni Alfred Martin Elia, Mwina Mohammed Kaduguda, Ally Suru, Said Tully, Juma Abbas Pinto, Hamisi Ramadhani Mkoma, Abubakar Zebo, Omar Juma Mazola, Patrick Paul Rweyemamu na Suleiman Omar Suleiman.
    Mwisho wa kurudisha fomu ni Jumamosi wiki hii, Septemba 15 kuanzia Saa 3:00 asubuhi hadi Saa 10:00 jioni makao makuu ya klabu, Mtaa wa Msimbazi, Dar es Salaam.
    Uchaguzi Mkuu wa Simba SC umepangwa kufanyika Novemba 3 mwaka huu katika ukumbi ambao utatajwa baadaye mjini Dar es Salaam Kamati ya Uchaguzi ya klabu hiyo kupitia kwa Mwenyekiti wake, Boniphace Lihamwike. 
    Hiyo ni baada ya uongozi uliopita ulioingia madarakani juni 30, mwaka 2014 chini ya Rais, Evans Elieza Aveva, Makamu wa Rais, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ na Wajumbe Iddi Kajuna, Said Tully, Collins Frisch, Ally Suru na Jasmine Badour kumaliza muda wao.
    Lakini Aveva na Kaburu hawakufanikiwa kumalizia muda wao madarakani, kufuatia kuwekwa rumande katika gereza la Keko tangu Juni 29, mwaka jana kwa tuhuma za kughushi nyaraka, kesi ambayo bado inaendelea katika Mahakama ya Kisutu mjini Dar es Salaam.
    Na Julai 1, mwaka jana, Kamati ya Utendaji iliwateua Salum Abdallah ‘Try Again’ na Iddi Kajuna kukaimu nafasi za Aveva na Kaburu na hao ndiyo waliosimamia mchakato mzima wa mabadiliko ya klabu kuelekea uchaguzi Mkuu ujao.
    Katiba mpya ya Simba SC inaelekea Rais wa klabu awe na elimu ya kiwango cha Shahada ambaye ataongoza Bodi ya Wakurugenzi itakayokuwa na Wajumbe wanane chini yake.
    Na Mwenyekiti huyo atakuwa na mamlaka ya kuteua Wajumbe wengine wanne, kati yao mmoja lazima awe mwanamke ili kukamilisha Bodi ya Ukurugenzi ya watu wanane.
    Hiyo ni baada ya mfanyabiashara Mohamed ‘Mo’ Dewji, Mbunge wa zamani wa Singida Mjini, kukubali kununua asilimia 49 za hisa za klabu ya Simba SC kulingana na maelekezo ya Serikali badala ya asilimia 51 alizotaka yeye awali katika mkutano Desemba 3, mwaka jana, ambao uliazimia kumfanya mwanahisa mkuu wa klabu katika mfumo mpya wa uendeshwaji.
    Mo pekee aliweka dau la Sh Bilioni 20 kuomba asilimia 50 ya hisa, baada ya klabu kutangaza kuuza asilimia 50 ya hisa zake kwa Sh. Bilioni 20 miezi miwili iliyopita, ingawa baadaye Serikali ikaagiza klabu hiyo isiuze zaidi ya asilimia 49 kwa mtu mmoja.
    Wanachama 1320 walihudhuria mkutano huo wa Desemba 3, mwaka jana kutoka Dar es Salaam na mikoa jirani na kwa furaha ya ushindi huo, Mo Dewji alitoa ahadi 10 za kuleta mabadiliko makubwa, ikiwemo ujenzi wa Uwanja wa mazoezi wa nyasi za asili na nyasi bandia pamoja na hosteli ya kisasa ya wachezaji.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: GWIJI WA SIMBA SC, MTEMI RAMADHANI ACHUKUA FOMU KUGOMBEA UENYEKITI WA KLABU NOVEMBA 3 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top