• HABARI MPYA

  Tuesday, September 04, 2018

  BODI YA LIGI YAWAFUNGIA MAKAMISAA WA MECHI ZA YANGA NA MTIBWA, AZAM NA MBEYA CITY KWA KUTOA TAARIFA POTOFU

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  KAMATI ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara imemfungia miezi mitatu Kamisaa wa mchezo kati ya Yanga SC na Kagera Sugar uliofanyika Agosti 23 Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam, Juma Chaponda wa Tanga.
  Kikao kilichofanyika Jumamosi mjini mjini Dar es Salaam kimejiridhisha Chaponda hakuwa makini katika kutoa taarifa za mchezo huo ambao Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 2-1.
  Mtendaji Mkuu wa Bodi, Boniphace Wambura alisema jana mjini Dar es Salaam kwamba pamoja na kufungiwa kwa Chaponda, lakini Kamati imempa onyo kali mshika kibendera namba moja, Sylvesrer Mwanga kwa kutokuwa makini kwenye uchezeshaji hususan katika eneo la kuotea.
  Klabu zote, Yanga na Mtibwa Sugar zimepewa onyo kali kwa kushindwa kuwasilisha orodha ya wachezaji wao iliyowatumia kwa mujibu wa sharia kwenye kikao cha kabla ya mechi asubuhi ya siku hiyo.

  Kamisaa na marefa wakiziongoza timu za Yanga na Mtibwa Sugar kuingia uwanjani 

  Naye refa Jimmy Fanuel wa Shinyanga aliyechezesha mechi kati ya Azam FC na Mbeya City, amefungiwa miezi mitatu kwa kushindwa kutafsiri vizuri sheria za soka.
  “Kipa wa Azam FC alimshika mchezaji wa Mbeya City wakati anakwenda kufunga baada ya yeye kuukosa mpira, refa aliamuru penalti, lakini akatoa kadi ya njano badala ya nyekundu kwa hiyo ameadhibiwa kutokana na upungufu huo,” alisema Wambura.
  Kamisaa wa mchezo huo, Victor Mwandike pia amefungiwa mechi tatu kwa kushindwa kutoa taarifa kwa usahihi.
  Aidha, Wambura amesema kwamba klabu ya Mbao FC imetozwa faini ya Sh. 500,000 kufuatia mashabiki wake kuingia uwanjani baada ya mechi kushangilia ushindi wa 1-0 dhidi ya Alliance FC.  
  Mshika kibendera, Jamada Ahamada wa Kagera amefungiwa kwa miezi mitatu kwa kushindwa kutafsiri sheria katika eneo la kuotea katika mchezo baina ya Singida United na Mwadui FC, wakati Kamisaa Juma Msaka wa Mwanza amepewa onyo kwa kutokuwa makini katika utoaji wa taarifa ya mechi.
  Na klabu za Singida United na Mwadui FC zimepewa onyo kwa kutowasilisha orodha ya wachezaji wao iliyowatumia katika kikoa cha kabla ya mechi.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: BODI YA LIGI YAWAFUNGIA MAKAMISAA WA MECHI ZA YANGA NA MTIBWA, AZAM NA MBEYA CITY KWA KUTOA TAARIFA POTOFU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top