• HABARI MPYA

  Saturday, September 08, 2018

  BOCCO AFUNGA MABAO MAWILI SIMBA SC YAICHAPA AFC LEOPARDS YA KENYA 4-2 TAIFA

  Na Sada Salmin, DAR ES SALAAM
  SIMBA SC wameendeleza ubabe mbele ya AFC Leopards ya Kenya baada ya usiku huu kuichapa mabao 4-2 katika mchezo wa kirafiki uliofanyika Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
  Lakini Leopards leo wamejipunguzia adhabu mbele ya mabingwa wa Tanzania, kwani mara ya mwisho walichapwa 4-0 Agosti 8, mwaka 2016 Uwanja wa Taifa pia.
  Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa bora wa Ligi Kuu msimu uliopita, Heri Sasii hadi mapumziko Simba SC walikuwa mbele kwa mabao 2-1. 
  Mshambuliaji na Nahodha, John Raphael Bocco alifunga bao la kwanza dakika ya 13 kwa kichwa akimalizia krosi ya beki wa kulia, Shomari Kapombe kabla ya kiungo Mohammed ‘Mo’ Ibrahim kufunga la pili dakika ya 40 kwa shuti akimalizia mpira wa adhabu uliopigwa na beki wa kushoto, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’.

  Wakati refa Sasii wa Dar es Salaam anajiandaa kupuliza kipyenga kumaliza kipindi cha kwanza, Eugene Mokangola akaifungia AFC Leopards dakika 45 kwa shuti baada ya krosi ya Baker Lukoye.
  Na kipindi cha pili kilipoanza, ilimchukua dakika 12 tu Bocco kufunga tena, akiwaamsha mashabiki wa Simba SC kwa mara ya tatu dakika ya 57 akifunga tena kwa kichwa baada ya krosi ya Tshabalala wa Bongo.
  Mtokea benchi Marcel Kaheza akaenda kuifungia Simba SC bao la nne dakika ya 78 kwa shuti la mpira adhabu baada ya mabeki wa AFC kumchezea rafu mshambuliaji mwenzake mpya Msimbazi, Adam Salamba aliyeingia pia kipindi cha pili.
  AFC Leopards wakafanikiwa kupata bao la pili dakika ya 89 kupitia kwa Ray Omondi ambaye alitumia makosa ya walinzi wa Simba SC.
  AFC Leopards kesho watasogea Uwanja wa Azam Complex, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam kwa mchezo mwingine wa kirafiki dhidi ya Mtibwa Sugar kuanzia Saa 1:00 usiku.
  Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Deo Munishi ‘Dida’, Shomari Kapombe/Asante Kwasi dk76, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Paul Bukaba, Yussuf Mlipili, Jonas Mkude/James Kotei dk61, Mohammed Rashid/Abdul Suleiman dk61, Mohammed ‘Mo’ Ibrahim/Marcel Kaheza dk76, Hassan Dilunga/Said Ndemla dk57, John Bocco/Adam Salamba dk61 na Shiza Kichuya/Rashid Juma dk61.
  AFC Leopards: Jairus Adira/Ezekial Owade dk26, Yussuf Mainge, Maross Abwao/Vincent Oburu dk88, Christopher Oruchum, Michael Kibwage, Said Tsuma/Saad Mussa dk88, Brain Marita/Ray Omondi dk66, Victor Majid, Aziz Okaka, Eugene Mukangola na Baker Lukoye.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: BOCCO AFUNGA MABAO MAWILI SIMBA SC YAICHAPA AFC LEOPARDS YA KENYA 4-2 TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top