• HABARI MPYA

    Friday, September 07, 2018

    AZAM FC KUCHEZA NA REHA FC JUMAPILI CHAMAZI MECHI YA TATU YA KIRAFIKI WIKI MOJA

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KIKOSI cha Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, kitakuwa na mchezo mwingine wa kujipima nguvu dhidi ya Reha FC utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex Jumapili Saa 3.00 asubuhi.
    Huo utakuwa ni mchezo wa tatu wa kirafiki kwa timu hiyo ya kocha Mholanzi, Hans van der Pluijm ndani ya wiki moja, baada ya awali kupoteza mchezo wa kwanza wa kujipima nguvu dhidi ya Transit Camp (2-1) kabla kutoka suluhu na Arusha United.
    Mchezo huo ni muendelezo wa programu ya benchi la ufundi la timu hiyo la kuwaweka sawa wachezaji ambao hawajapata nafasi ya kucheza kwenye mechi mbili za awali za Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL).
    Kocha Mholanzi wa Azam FC, Hans van der Pluijm timu yake itacheza mechi ya tatu Jumapili ndani ya wiki moja 

    Mbali na lengo hilo, pia ni sehemu ya programu ya kuwaweka kwenye ushindani wachezaji wote waliobakia kikosini kutokana na mapumziko ya ligi kupisha wiki ya mechi za timu za Taifa kufuzu Mataifa ya Afrika mwakani nchini Cameroon.
    Jumla ya wachezaji saba wa Azam FC wapo kwenye timu mbalimbali za Taifa, Nahodha Agrey Moris na Msaidizi wake, Frank Domayo, David Mwantika, Mudathir Yahya na Yahya Zayd, wapo na Tanzania ‘Taifa Stars’, Nickolas Wadada (Uganda ‘The Cranes’) na Tafadzwa Kutinyu (Zimbabwe ‘The Warriors’).
    Mara baada ya mchezo huo wa kirafiki, Azam FC itaendelea na maandalizi yake makali kuelekea mechi tatu zijazo za ligi itakazocheza Kanda ya Ziwa dhidi ya Mwadui (Septemba 14), Biashara UTD (Septemba 19) na Alliance (Septemba 23) kabla ya kurejea jijini Dar es Salaam kukipiga na Lipuli Septemba 27, mwaka huu.
    Hadi sasa Azam FC imeshacheza mechi mbili za ligi na kujikusanyia pointi zote sita katika nafasi ya pili kwenye msimamo ikizidiwa pointi moja na vinara Mbao walifikisha pointi saba lakini wakiwa wamecheza mchezo mmoja zaidi ya matajiri hao kutoka viunga vya Azam Complex.
    Katika mechi hizo mbili, Azam FC imefunga jumla ya mabao matano na kutoruhusu nyavu zake kutikiswa na kuwa timu pekee yenye wastani mkubwa wa kufunga mabao katika ligi hiyo ikiwa na wastani wa mabao 2.5 kwa kila mechi.  
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AZAM FC KUCHEZA NA REHA FC JUMAPILI CHAMAZI MECHI YA TATU YA KIRAFIKI WIKI MOJA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top