• HABARI MPYA

  Thursday, August 02, 2018

  YANGA SC YAAMUA KUMTEMA YOUTHE ROSTAND, KIKOSI CHAINGIA KAMBINI MORO KUJIANDAA NA WAARABU

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  KIPA Mcameroon, Youthe Rostand Juhe hayumo kwenye orodha ya wachezaji waliongia kambini na kikosi cha Yanga leo mjini Morogoro kujiandaa na mchezo ujao dhidi ya USM Alger kwa sababu yupo kwenye mazungumzo na uongozi juu ya kuondoka.
  Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga SC, Hussein Nyika ameiambia Bin Zubeiry Sports – Online leo kwamba wapo kwenye mazungumzo na Rostand ambayo yanaendelea vizuri kwamba aondoke baada ya msimu mmoja wa kuitumikia klabu.
  “Rostand hajakwenda kambini Morogoro kwa sababu tupo kwenye mazungumzo naye ambayo yanaendelea vizuri na ninadhani hadi kufikia kesho tutakuwa tumefikia mwafaka,”amesema.
  Youthe Rostand hajaingia kambini na Yanga leo mjini Morogoro kujiandaa na mchezo ujao dhidi ya USM Alger 

  Nyika amesema kwamba kikosi kimeondoka leo asubuhi mjini Dar es Salaam na leo jioni kinatarajiwa kufanya mazoezi yake ya kwanza kwa ajili ya mchezo wa marudiano dhidi ya USM Alger ya Alger Agosti 19 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Amesema kambi hiyo kwa ujumla ni ya maandalizi ya msimu mpya, lakini kwa kuwa wamebakiza mechi mbili za Kundi D Kombe la Shirikisho pamoja na hiyo ya Agosti 19 dhidi ya USM Alger pia watakwenda Rwanda kucheza na Rayon Sport Agosti 28 – itahusisha na mechi hizo pia.
  Kabla ya hapo, Agosti 12 Yanga SC itakuwa na mchezo maalum wa kirafiki wa kumuaga aliyekuwa Nahodha wake, Nadir Haroub 'Cannavaro' ambaye baada ya kuichezea klabu hiyo tangu mwaka 2006, Cannavaro amestaafu mwishoni mwa msimu uliopita na kuwa Meneja wa timu. 
  Yanga SC iliendelea kufanya vibaya kwenye mechi zake za Kundi D Kombe la Shirikisho la Afrika, baada ya Jumapili iliyopita kuchapwa mabao 3-2 na Gor Mahia ya Kenya Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
  Matokeo haya yanamaanisha Yanga inaendelea kukamata mkia katika kundi D, ikibaki na pointi yake moja iliyovuna kwenye sare ya 0-0 na Rayon Sport ya Rwanda kutokana na kufungwa mechi nyingine tatu, mbili dhidi ya Gor Mahia ukiwemo wa wiki mbili zilizopita waliochapwa 4-0 mjini Nairobi.
  Mechi nyingine ambayo ilikuwa ya kwanza kabisa, Yanga ilichapewa mabao 4-0 na USM Alger mjini Algiers nchini Algeria.
  Yanga wataikaribisha USM Alger Agosti 19 kabla ya kwenda kukamilisha mechi zake za kundi hilo kwa kumenyana na wenyeji, Rayon Sport Agosti 28, mwaka huu mjini Kigali, Rwanda.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA SC YAAMUA KUMTEMA YOUTHE ROSTAND, KIKOSI CHAINGIA KAMBINI MORO KUJIANDAA NA WAARABU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top