• HABARI MPYA

    Friday, August 10, 2018

    TASWA, MCT WALAANI KITENDO CHA MWANDISHI WA HABARI KUPIGWA NA POLISI SIMBA DAY TAIFA

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    BARAZA la Habari Tanzania (MCT) na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo nchini (TASWA) vimesikitishwa, kufedheheshwa na kukasirishwa na tukio la ukatili lililofanywa na polisi dhidi ya mwandishi wa habari wa kituo cha Wapo Radio cha Dar es Salaam, Silas Mbise Jumatano Agosti 8, 2018 katika Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.
    Taarifa ya pamoja ya Katibu Mkuu TASWA, Amir Mhando na  Katibu Mtendaji MCT, Kajubi Mukajanga imesema kwamba kwa mujibu wa Mbise tukio hilo lilitokea baada ya mchezo wa Tamasha la “Simba Day” kwenye mechi kati ya timu ya Simba na Asante Kotoko ya Ghana, ambapo kama ulivyo utaratibu mchezo ukimalizika waandishi wa habari wanaenda kuzungumza na makocha katika eneo maalum lililotengwa. 
    Lakini wakati akielekea eneo hilo baadhi ya askari walikuwa wakizuia waandishi kuingia eneo hilo na alipojaribu kuwaelewesha na kujitambulisha ndipo akafanyiwa ukatili huo wa kupigwa na kuumizwa.

    Silas Mbise alishambuliwa na Polisi Jumatano ya Agosti 8, 2018 wakati wa tamasha la Simba Day Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam

    Tukio hili na mengineyo ya kikatili wanayofanyiwa wanahabari wakiwa kazini hayatafumbiwa macho kwani si udhalilishaji wa taaluma ya habari tu bali tunachukulia kuwa ni hujuma kwa tasnia kwa nia ya kudhoofisha uhuru wa kupatikana kwa habari na usambazaji wa habari kwa jamii ikiwa ni nguzo kuu kwenye mfumo wa kidemokrasia, ambao tunajitahidi kuuimarisha nchini. Vyombo vya habari pia ni nguzo muhimu ya kujenga jamii yenye uelewa wa mambo mbalimbali yanayoendelea nchini kama inavyoainishwa kwenye Ibara ya 18 ya Katiba ya nchi yetu.
    Vile vile ifahamike kwamba, Lakini pia kitendo hicho ni kinyume na ibara ya 13(6) (e) ya katiba ya jamhuri ya muungano wa Tanzania inayokataza mtu kuteswa. Hivyo basi, kukaa kimya, hata tukiliwazwa na kuombwa samahani kwa jambo hili, hakutatoa tafsiri nyingine kwa wana taaluma ya habari na jamii kwa ujumla isipokuwa kuliona jambo hili kama ni la kawaida. Waandishi wana kila haki ya kufanya kazi zao bila kusumbuliwa, kupigwa au kutishwa.
    Tunatarajia jeshi la polisi kufanyakazi zake kwa kufuata sheria na weledi wa kazi na kuwa walinzi wa amani na mali za wananchi.
    Mbise kwa hivi sasa yupo katika matibabu kutokana na kipigo hicho. Tunataka polisi wote waliohusika katika kitendo hiki cha kikatili wachukuliwe hatua kali ili wasiendelee kulipa taswira mbaya jeshi zima la polisi.
    Kifungu cha 7 (1) cha Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari, 2016 inatoa haki na wajibu kwa vyombo vya habari kukusanya, kuchakata na kusambaza habari na taarifa mbalimbali kwa wananchi.
    1
    Hivyo ni vyema wadau wetu wakatambua kuwa uandishi wa habari ni taaluma adhimu na nadhifu inayopaswa kuheshimiwa, kuenziwa, kulindwa na kutoingizwa katika migogoro.
    MCT na TASWA inataka wadau wa michezo ikiwa ni pamoja na Polisi, wachezaji, viongozi ana mashabiki mwenye malalamiko kwa mwandishi wa habari binafsi, au chombo chake afuate taratibu za kistaarabu zilizopo, ikiwemo kuwasiliana na uongozi wa chombo cha habari husika na wakishindwa kuafikiana wapeleke malalamiko yao TASWA na Baraza la Habari kwa hatua za zaidi za usuluhishi.
    MCT pia inawataka wanahabari wote wanaopata madhila ya kuzuiawa kufanya kazi zao au vitendo vya kikatili dhidi yao pia kutoa taarifa kwenye Baraza.
    Mbise kwa hivi sasa anafanya yupo katika matibabu kutokana na kipigo hicho tumekubaliana tukio hili lichukuliwe hatua kali zaidi za kisheria.
    TASWA jana ilifanya kikao na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuhusu jambo hili, inaishukuru TFF kwa ushirikiano, lakini pia TASWA itaandaa kikao na wahariri wa habari za michezo kuona namna ya kujadili masuala ya usumbufu wa wanahabari viwanjani kabla ya Ligi Kuu Tanzania Bara haijaanza.
    Baraza la Habari, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania wanawasiliana na wanasheria wao kwa ajili ya kufungua mashtaka dhidi ya wahusika kwa vitendo vya mateso (tourture” alivyofanyiwa ndugu Mbise. Tunawaomba waandishi wa habari wawe watulivu na waziachie mamlaka husika zitekeleze majukumu yake kwa mujibu wa sheria za nchi.
    Wakati huo huo: Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, limeanza kuchunguza tukio la kupigwa kwa mwandishi wa habari wa Kituo cha Wapo Radio, Sillas Mbise aliyepigwa na Polisi juzi.
    Aidha, Jeshi hilo limemtaka mwandishi huyo   kuripoti tukio hilo kituo cha polisi ili hatua zichukuliwe.
    Hatua hiyo imekuja siku mbili baada ya mwandishi huyo kupigwa na polisi katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam wakati wa maadhimisho ya siku ya Klabu ya Simba SC (Simba Day) ambapo hata hivyo haikufahamika mara moja kosa la mwandishi huyo.
    Akizungumza na Waandishi wa habari leo Ijumaa agosti 10, Kamanda wa Polisi Landa Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa amesema jeshi lake limeanza uchunguzi wa tukio hilo kwa kufungua jalada la uchunguzi wa picha ya video inayosambaa ikimuonyesha polisi wakimpiga mwandishi huyo ili kubaini ukweli.
    “Hiyo inaenda sambamba na kumtaka mtendewa wa kosa hilo la kupigwa kutoa taarifa kituo cha polisi kwani mtu yeyote anatakiwa kutoa malamiko yake pale anapoona ametendewa vitendo ambavyo ni kinyume cha sheria,” amesema.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TASWA, MCT WALAANI KITENDO CHA MWANDISHI WA HABARI KUPIGWA NA POLISI SIMBA DAY TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top