• HABARI MPYA

  Wednesday, August 08, 2018

  SHAABAN IDDI CHILUNDA APATA MAPOKEZI MAKUBWA CD TENERIFE…APELEKWA HADI UWANJANI

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Shaaban Iddi Chilunda leo amepata mapokezi mazuri katika klabu yake mpya, CD Tenerife ya Daraja la Kwanza nchini Hispania anayojiunga nayo kwa mkopo wa miaka miwili kutoka Azam FC.
  Chilunda amewasili leo na kupokewa na mashabiki kadhaa wa timu hiyo sambamba na kundi kubwa la Waandishi wa Habari waliomfanyia mahojiano makao makuu ya klabu, Santa Cruz de Tenerife, Tenerife, visiwa vya Canary.
  Akizungumzia mapokezi hayo, Chilunda aliyepelekwa hadi Uwanja wa Heliodoro Rodríguez López, unaotumiwa na timu hiyo amesema; “Kwa kweli nimefurahi sana, yamekuwa mapokezi makubwa ambayo sikuyatarajia. Namshukuru sana Mungu, hii inanipa ujumbe kwamba nina deni kubwa hapa. Watu wana matarajio makubwa na mimi. Nitajitahidi kwa uwezo wa Mungu,”amesema.
  Shaaban Iddi Chilunda (kulia) akiwa makao makuu ya CD Tenerife leo
  Shaaban Iddi akionyeshwa Uwanja wa Heliodoro Rodríguez López wa CD Tenerife

  Shaaban Iddi akizungumza na Waandishi wa Habari makao makuu ya klabu, Santa Cruz de Tenerife

  Shaaban Iddi ambaye aliyetimiza miaka 20 Julai 20 mwaka huu tangu azaliwe mwaka 1998, alijiunga na akademi ya Azam FC Jumamosi ya Julak 21, mwaka 2012 kabla ya miaka miwili baadaye kupandishwa kikosi cha kwanza.
  Na msimu huu Chilunda ameweka rekodi ya kufunga mabao mengi zaidi katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame kwa kufunga mabao nane, yakiwemo manne ya rekodi katika mchezo mmoja wa Robo Fainali dhidi ya Rayon Sport ya Rwanda.
  Kumbukumbu zinaonyesha hakuna mchezaji aliyewahi kufunga mabao manne katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati tangu inaanzishwa mwaka 1974 – maana yake chipukizi wa Tanzania ameweka rekodi mpya.
  Na heshima zaidi kwake alifunga dhidi ya timu ngumu yenye safu imara ya ulinzi, Rayon Sport ambao pia wanashiriki Kombe la Shirikisho Afrika wakiwa Kundi moja na vigogo wa Tanzania, Yanga SC.
  Na zaidi ya hayo, anasifiwa kufunga bao zuri zaidi kwenye mashindano haya hadi sasa, ambalo ni dhidi ya Vipers FC ya Uganda akimpiga kanzu kipa kabla ya kutumbukiza mpira nyavuni.
  Mabao saba ndiyo kiwango cha juu hadi sasa cha wafungaji bora wa michuano ya Kagame, idadi ambayo mara ya mwisho ilifikiwa na mshambuliaji Chiukepo Msowoya wa APR mwaka 2010 nchini Rwanda.
  Na kwenye idadi kubwa ya mabao katika mchezo mmoja, mara ya mwisho mchezaji mmoja kufunga mabao mengi ilikuwa mwaka 2013 na huyo ni Mrundi, Amissi Tambwe akiwa na Vital'O ya kwao aliifunga mabao matatu dhidi ya AS Ports ya Djibouti katika ushindi wa 6-0, mchezo wa Robo Fainali.
  Na kabla ya hapo, hat trick nyingine ya Kagame ilifungwa na John Raphael Bocco mwaka 2012 akiwa na Azam FC akiiadhibu timu yake ya sasa, Simba SC kwenye Robo Fainali pia. 
  Chilunda atakuwa mchezaji wa pili Mtanzania katika kikosi cha Tenerife, mwingine Farid Mussa pia kutoka Azam FC aliyejiunga na timu hiyo Faridi Malik Mussa Shah aliyejiunga na timu hiyo mwaka 2016 kutoka Azam FC pia na wote wameibuliwa katika akademi ya Chamazi.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SHAABAN IDDI CHILUNDA APATA MAPOKEZI MAKUBWA CD TENERIFE…APELEKWA HADI UWANJANI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top