• HABARI MPYA

  Sunday, August 05, 2018

  SEEDORF NA KLUIVERT MAKOCHA WAPYA TIMU YA TAIFA CAMEROON

  KIUNGO wa zamani wa kimataifa wa Uholanzi, Clarence Seedorf ametambulishwa kuwa kocha mpya wa timu ya taifa ya Cameroon na atakuwa anasaidiwa na mchezaji mwenzake wa zamani, Patrick Kluivert.
  Uteuzi wa wawili hao umetangazwa na Waziri wa Michezo na Elimu wa Cameroon, Pierre Ismael Bidoung Mkpatt katika mkutano wake na Waandishi wa Habari Jumamosi baada ya mazungumzo na kocha wa zamani wa England, Sven-Goran Eriksson kutopata mwafaka.
  Seedorf anakwenda kuchukua nafasi ya Mbelgiji, Hugo Broos, ambaye aliiongoza timu hiyo kutwaa taji Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka jana, lakini akashindwa kuipeleka Kombe la Dunia nchini Urusi.

  Clarence Seedorf ameteuliwa kuwa kocha wa timu ya taifa ya Cameroon 

  Alexandre Belinga amekuwa akikaimu ukocha wa timu tangu wakati huo. Cameroon itatetea Kombe lake la AFCON nyumbani Juni mwakani.Seedorf, mwenye umri wa miaka 42, hicho kinakuwa kibarua chake cha kwanza katika timu ya taifa baada ya uzoefu wa kufundisha klabu AC Milan ya Italia, Shenzhen ya China na Deportivo La Coruna ya Hispania.
  Ameziongoza timu hizo katika jumla ya mechi 52, lakini anafahamika zaidi kwa makali yake alipokuwa anacheza na zaidi alipokuwa anachezea vigogo kama Ajax Amsterdam, Real Madrid na AC Milan, ambazo kila moja alishinda nayo taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya.
  Pia aliichezea jumla ya mechi 87 timu ya taifa ya Uholanzi kati ya mwaka1994 na 2008.
  Mshambuliaji mwingine wa zamani, Kluivert pia amechezea timu kadhaa zikiwemo Ajax, ambako alishinda taji la Ligi ya Mabingwa na Seedorf, Milan na zaidi Barcelona alikodumu kwa misimu sita.
  Alikuwa Kocha Msaidizi wa Louis van Gaal timu ya taifa ya Uholanzi kati ya mwaka 2012 na 2014, kabla ya baadaye kuifundisha kwa muda Curacao.
  Shirikisho la Soka Cameroon halijawahi kutangaza nafasi ya kazi kwa kocha wa timu ya taifa,laini makocha Afrika kwa kawaida wanateuliwa na Serikali.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SEEDORF NA KLUIVERT MAKOCHA WAPYA TIMU YA TAIFA CAMEROON Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top