• HABARI MPYA

  Sunday, August 05, 2018

  MTIBWA SUGAR WAZUNGUMZIA KUHAMA KWA BANKA NA DILIUNGA; “HAKUNA MCHEZAJI ALIONDOKA AKAACHA PENGO MTIBWA SUGAR”

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  WASHINDI wa Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), lijulikanalo kama Azam Sports Federation Cup (ASFC), Mtibwa Sugar wamesema kwamba hakuna mchezaji aliyeondoka akaacha pengo katika klabu yao kihistoria.
  Hayo yalikuwa majibu ya Katibu Msaidizi wa Mtibwa Sugar, Abubakar Swabur alipoulizwa na Bin Zubeiry Sports – Online juu ya kuondoka kwa viungo Mohammed Issa ‘Banka’ aliyehamia Yanga SC na Hassan Dilunga aliyejiunga na Simba SC, zote za Dar es Salaam.
  Lakini baada ya viungo hao waliong’ara kwenye kikosi cha Mtibwa Sugar msimu uliopita kuhama, Swabur amesema; “Kihistoria hakuna mchezaji aliyeondoka akaacha pengo la kudumu Mtibwa Sugar, ni kweli Banka na Dilunga walikuwa sehemu ya wachezaji wetu muhimu msimu uliopita, lakini nafasi zao zitazibwa na mtawasahau,”amesema.

  Mohammed Issa ‘Banka’ amejiunga na Yanga SC akitokea Mtibwa Sugar ya Morogoro 

  Hassan Dilunga amejiunga na Simba SC ya Dar es Salaam akitokea Mtibwa Sugar ya Morogoro

  Swabur ameongeza kwamba Mtibwa Sugar ni chuo cha kukuza vipaji vya wanasoka wanaogeuka kuwa lulu katika soka ya Tanzania na baada ya vigogo, Simba na Yanga kuvuna tena msimu huu, wanakaribishwa tena msimu ujao.
  “Wameondoka wachezaji wengi Mtibwa tangu enzi za akina Peter Manyika mkubwa, hadi akina Amir Maftah, Hassan Kessy, Shiza Kichuya, Muzamil Yassin na wengine, lakini Mtibwa Sugar haijawahi kuyumba na haitayumba,”ameongeza.
  Kuhusu maandalizi ya mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya mabingwa wa Ligi Kuu, Simba SC Agosti 18, mwaka huu Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza, Swabur amesema kwamba yanaendelea vizuri na kikosi kwa sasa kipo kambini Manungu, Turiani mkoani Morogoro.
  Amesema kikosi kitahamia Dar es Salaam Agosti 10 kwa ajili ya mechi ya kirafiki ya kujipima nguvu dhidi ya KMC kati ya Agosti 11 na 12 kabla ya safari ya Mwanza tayari kuwavaa Simba SC.       
  Kwa sasa benchi la Ufundi la Mtibwa Sugar linaongozwa na Mkurugenzi wa Ufundi, Salum Mayanga, Kocha Mkuu Zubery Katwila na Kocha Msaidizi, Patrick Mwangata, ambaye pia ni kocha wa makipa wote wachezaji wake wa zamani.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MTIBWA SUGAR WAZUNGUMZIA KUHAMA KWA BANKA NA DILIUNGA; “HAKUNA MCHEZAJI ALIONDOKA AKAACHA PENGO MTIBWA SUGAR” Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top