• HABARI MPYA

    Friday, August 10, 2018

    MAHAKAMA YAIPA JAMHURI SIKU SABA KUWAONDOA HANS POPPE NA LAUWO KESI YA AKINA AVEVA, KABURU

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imetoa siku saba kwa upande wa jamhuri kukamilisha mchakato wa kubadilisha hati ya mashtaka ili kuwaondoa washtakiwa wawili katika kesi inayomkabili aliyekuwa Rais wa Klabu ya Simba SC, Evans Aveva na Makamu wake, Godfrey Nyange maarufu Kaburu au kuifuta kesi hiyo.
    Washtakiwa wanaotakiwa kuondolewa katika kesi hiyo ni Zacharia Hans Poppe na Frank Lauwo ambao hawajawahi kufika mahakamani hapo.
    Akitoa uamuzi huo leo mahakamani hapo,  Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba amesema bado wanaifuatilia kesi hiyo kwa ukaribu lakini itafika mahali uvumilivu utawashinda na kama jamhuri wameshindwa basi waifute.

    Mahakama imeamuru Zacharia Hans Poppe (kulia) aondolewe kwenye kesi ya viongozi wa Simba SC

    “Ukiangalia afya ya Aveva unaona kabisa ni mgonjwa, anatakiwa kwenda kliniki kwa wiki mara mbili, hivyo basi tunalazimika kuangalia ratiba ya matibabu yake ili tupange kesi,” amesema Hakimu Simba.
    Awali, Wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Leonard Swai ameieleza mahakama hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba kuwa, kesi hiyo imekuja kwa ajili ya kutajwa na tayari wameshaifanyia marekebisho hati ya mashtaka na kwamba wanasubiri kibali cha Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) ili kesi hiyo iendelee kwa mujibu wa sheria.
    Baada ya Wakili huyo kudai hayo, Aveva aliiomba mahakama hiyo kupanga tarehe za karibu za kusikiliza kesi hiyo kwa madai kuwa imechukua muda mrefu huku Wakili wa Jamhuri Shadrack Kimaro na Wakili Takukuru, wamekuwa wakirushiana mpira.
    Kwa upande wake Kaburu ambaye ni mshtakiwa wa pili amedai kuwa ni zaidi ya mwaka mmoja sasa umepita wako mahabusu tangu kesi hiyo ianze kusikilizwa mahakamani hapo huku mawakili hao wakidai faili liko kwa DPP.
    Alidai mshtakiwa wa kwanza, Aveva ana matatizo ya kiafya na kwamba kila wiki anaenda kliniki kwa ajili ya matibabu hivyo basi kuendelea kurushiana mpira ni kuwaumiza na kwamba hadhani kama DPP ameshindwa kushughulikia kesi yao, bali ni ucheweshaji wa makusudi unaofanywa na mawakili hao katika kesi hiyo kutoka kwa DPP na Takukuru.
    Amedai upelelezi umeshakamilika kilichobaki ni kubadilisha hati hiyo ili kesi ianze kusikilizwa, hivyo basi anaiomba mahakama hiyo kupanga tarehe za karibuni ili waweze kuwaona na kuwaonea huruma kuliko kupanga tarehe za mbali za wiki mbili.
    Wakili Swai alidai kuwa, hoja zilizotolewa na washtakiwa hao zina mashiko na kuahidi kushughulikia suala hilo.
    Hakimu Simba alihairisha kesi hiyo hadi Agosti 17 mwaka huu.
    Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka kumi likiwemo la kula njama, matumizi mabaya na kughushi nyaraka ikionyesha Klabu ya Simba inalipa mkopo wa Dola za Marekani 300,000 kwa Aveva kitu ambacho si kweli.
    Wanadaiwa, kuwa  Machi 10 na 16, 2016, Aveva na Nyange waliandaa nyaraka za kuhamisha dola za kimarekani 3000,000 kutoka kwenye akaunti ya klabu ya Simba kwenda kwenye akaunti ya Aveva wakijua kuwa wanachofanya ni kosa.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MAHAKAMA YAIPA JAMHURI SIKU SABA KUWAONDOA HANS POPPE NA LAUWO KESI YA AKINA AVEVA, KABURU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top