• HABARI MPYA

  Tuesday, August 07, 2018

  KOCHA MPYA SIMBA SC, AUSSEMS ASEMA: "KOTOKO WATANIPA TASWIRA YA KIKOSI CHANGU"

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  KOCHA Mkuu wa Simba SC, Mbelgiji Patrick J Aussems amesema kwamba atautumia mchezo wa kesho wa kirafiki dhidi ya Asante Kotoko ya Ghana kupata mwanga wa kikosi chake kabla ya kuanza kwa msimu mpya wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
  Akizungumza na Waandishi wa Habari mjini Dar es Salaam leo katika mkutano uliofanyika Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam, Aussems amesema kwamba baada ya maandalizi mazuri katika kambi ya Uturuki ni wakati mwafaka sasa kukiona kikosi chake katika mechi nzuri ya ushindani dhidi ya timu bora kama Asante Kotoko.
  “Tumejipanga vyema kufanya vizuri ikiwemo mchezo wetu huu wa kesho dhidi ya Asante Kotoko,"amesema Aussems aliyejiunga na Simba SC mapema mwezi huu akichukua nafasi ya Mfaransa, Pierre Lechantre aliyedumu kwa nusu msimu Msimbazi.

  Mbelgiji Patrick J Aussems amesema atautumia mchezo dhidi ya Asante Kotoko kupata mwanga wa kikosi chake

  Kwa upande wake, Nahodha wa Simba SC, Aishi Salum Manula amesema kwamba watahakikisha wanashinda katika mchezo wao huo ili kuwapa raha mashabiki wao.
  Alisema walipokuwa Uturuki walifanya maandalizi ya kutosha na wanatumia nafasi ya kuonyesha kile walichokipata kutoka katika kambi hiyo.
  “Tulipokuwa Uturuki kuna baridi na sasa tumerudi huku kwenye joto, itatusaidia kwa kucheza dakika 90 bila ya kuchoka, " amesema Manula.
  Naye kocha wa Asante Kotoko, Kwesi Fabim amesema kwamba atautumia mchezo huo kutambulisha mchezaji wake mpya.
  “Tumekuja kucheza na Simba na tutatumia nafasi hiyo kwa ajili ya kutambulisha mchezaji wetu mpya na pia kuwa burudani mashabiki wa Simba," amesema.
  Baada ya kambi ya wiki mbili ya kujiandaa na msimu mpya nchini Uturuki, Simba SC imerejea jana mjini Dar es Salaam na kesho itacheza na Kotoko katika mchezo wa kirafaki kupamba tamasha la Simba Day.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: KOCHA MPYA SIMBA SC, AUSSEMS ASEMA: "KOTOKO WATANIPA TASWIRA YA KIKOSI CHANGU" Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top