• HABARI MPYA

  Sunday, August 05, 2018

  KOCHA MOROCCO ASUSA KAZI SINGIDA UNITED SABABU HAJATEKELEZEWA STAHIKI ZAKE

  Na Sada Salmin, DAR ES SALAAM
  KOCHA mpya wa Singida United, Hemed Suleiman ‘Morocco’ hajajiunga na timu hiyo kwa maandalizi ya msimu mpya kwa sababu hajakamilishiwa baadhi ya mambo waliokubaliana.
  Akizungumza na Bin Zubeiry Sports – Online jioni hii kwa simu kutoka Zanzibar, Morocco amesema kwamba hajaungana na timu katika kambi ya Mwanza kujiandaa na msimu mpya kwa sababu kuna mambo hayajakaa sawa.
  “Mimi bwana sijakwenda katika kambi, kwa sababu kuna mambo yangu hayajakaa sawa kati yangu na uongozi. Nawasubiri tu tukamilishiane mambo tuliyokubaliana ndiyo nitakwenda,”amesema.

  Hemed Suleiman ‘Morocco’ hajajiunga na Singida United kwa maandalizi ya msimu mpya kwa sababu hajakamilishiwa stahiki zake 

  Kocha huyo Msaidizi wa zamani wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars amesema yeye hana tatizo na Singida United wakati wowote tu watakapomtimizia stahiki zake atakwenda kujiunga na timu.
  “Na kama watachelewa kunimalizia maana yake maandalizi ya timu kwa ajili ya msimu mpya yataendelea bila mimi na hatari yake ni kwamba timu inaweza kufanya vibaya katika Ligi Kuu, nadhani hilo wanalijua. Kweli kuna programu nimewapa wanaendelea nazo, lakini napaswa kuwepo mimi mwenyewe kuzisimamia,”amesema.
  Morocco ambaye pia amekuwa kocha wa Zanzibar Heroes na klabu mbalimbali, Bara na visiwani ikiwemo Coastal Union ya Tanga, amesema kwamba amekuwa akiukumbusha uongozi wa Singida United juu ya kumalizana ili aingie kazini, lakini wamekuwa wakimpa tu ahadi za ‘kesho, kesho’.   
  Morocco alijiunga na Singida United Mei mwaka huu kuchukua nafasi ya kocha Mholanzi, Hans van der Pluijm aliyehamia Azam FC.
  Na baada ya kuiongoza timu hiyo kwenye michuano ya SportPesa Super Cup nchini Kenya na Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, maarufu kama Kombe la Kagame amesusa hadi apewe stahiki zake.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: KOCHA MOROCCO ASUSA KAZI SINGIDA UNITED SABABU HAJATEKELEZEWA STAHIKI ZAKE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top