• HABARI MPYA

    Thursday, August 09, 2018

    AMUNIKE: HATA NIGERIA ILIPITIA ILIPO TANZANIA, IMANI NA KUJITUMA VITATUPANDISHA KWENYE KILELE CHA MAFANIKIO

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    MAPEMA wiki hii Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limemtambulisha winga wa zamani wa kimataifa wa Nigeria, Emmanuel Amunike kuwa kocha mpya wa timu ya taifa, Taifa Stars ambayo ipo kwenye mbio za kuwania tiketi ya Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwakani nchini Cameroon.
    Na baada ya mchezaji huyo wa zamani wa Barcelona ya Hispania kusaini mkataba wa miaka miwili, Bin Zubeiry Sports – Online ilikutana naye kwa mahojiano maalum katika hoteli ya New Africa mjini Dar es Salaam kuelekea majukumu yake mapya.
    Bin Zubeiry Sports – Online; Habari yako kocha 
    Emmanuel Amunike; Nzuri, karibu
    Bin Zubeiry Sports – Online; Asante…naitwa Mahmoud kutoka tovuti ya Bin Zubeiry Sports - Online 
    Emmanuel Amunike; Sawa, Amunike hapa, kocha wa Tanzania

    Emmanuel Amunike (kulia) katika mahojiano na mwandishi wetu, Mahmoud Zubeiry juzi mjini Dar es Salaam

    Bin Zubeiry Sports – Online; Karibu Tanzania gwiji wa Nigeria  
    Emmanuel Amunike; Asante sana Mwandishi mkubwa
    Bin Zubeiry Sports – Online; Naweza kupata wasaa wa mahojiano nawe
    Emmanuel Amunike; Bila shaka, kwa nini hapana?
    Bin Zubeiry Sports – Online; Asante…Sasa umekuja kufundisha timu ndogo ya Tanzania, ni ipi mipango yako? 
    Emmanuel Amunike; Unasema ni timu ndogo? Sifikirii hivyo, hakuna timu ndogo tena kwenye soka, kinachotakiwa ni kuinua uwezo wa timu
    Bin Zubeiry Sports – Online; Unaanzaje?
    Emmanuel Amunike; Mara moja naanza kuangalia cha kufanya kujenga timu kwa ajili ya majukumu yaliyo mbele yetu. 
    Bin Zubeiry Sports – Online; Kabla ya kuombwa kuifundisha Tanzania, ulikuwa unafahamu chochote kuhusu nchi hii?
    Emmanuel Amunike; Ndiyo, nimeiona soka ya Tanzania. Mechi za mwisho za kufuzu AFCON Nigeria na Tanzania hazikufuzu, tulikuwa kundi moja na Misri na Chad, bahati mbaya timu ya Chad ilijitoa. Niliona mechi waliyocheza na Nigeria, ni timu nzuri, hivyo si kuhusu nimewaona au sijawaona. Kitu cha muhimu lazima tufahamu Afrika soka imekuwa. 
    Bin Zubeiry Sports – Online; Ilikuwa rahisi kwako kukubali ofa ya kufundisha Tanzania?
    Emmanuel Amunike; Si ilikuwa rahisi, ilikuwa ngumu. Kitu cha muhimu ni nilipokutana na Katibu wa TFF (Wilfred Kidau) kwenye mkutano wa CAF (Shirikisho la Soka Afrika) mjini Cairo mwaka jana, tulizungumza mengi na nikagundua wana dhamira ya dhati ya kuinua soka ya Tanzania na hicho ndicho kilichonishawishi kukubali.
    Bin Zubeiry Sports – Online; Hatuna wachezaji wengi wanaocheza nje kama nchi nyingine zina nyota wengi Ulaya na Asia, zaidi vijana wetu wanacheza hapa katika Ligi yetu ndogo. Unaizungumziaje hii?
    Emmanuel Amunike (kulia) enzi zake akiichezea Barcelona nchini Hispania


    Emmanuel Amunike (kulia) akishangilia na mchezaji mwenzake wa Barcelona wakati huo, Ronaldo Lima 

    Emmanuel Amunike; Kweli, nafikiri hakuna binadamu anayezaliwa anatembea, ni kweli Tanzania haina wachezaji wengi wanaocheza sehemu hizo, lakini pia naweza kukuambia Nigeria kuna wakati ilikuwa inakabiliwa na hali hiyo. Kulikuwa kuna wachezaji wachache wanacheza Ubelgiji na Uholanzi. Lakini kocha alianza kutumia wachezaji wanaocheza Ligi ya nyumbani, akawapa nafasi tukagundua tuna wachezaji wazuri na baada ya hapo wakaanza kuchukuliwa Ulaya.
    Bin Zubeiry Sports – Online; Inawezekana hiyo na kwa Tanzania pia? 
    Emmanuel Amunike; Ndiyo, na huo ndio mpango wa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (Wallace Karia) na watu katika uongozi wake. Nafikiri ni jambo la kuungana kwa pamoja kusapoti timu yetu na wachezaji wetu tulionao. Timu ya taifa ni ya kujivunia kwa kila nchi, nafikiri ni jukumu la kila mmoja miongoni mwa Watanzania kuisapoti timu yake ya taifa na wachezaji tulionao, naamini tutafanikiwa, ndani ya muda mfupi Tanzania itakuwa na wachezaji wengi wanaocheza Ulaya. 
    Kama kuna wachezaji kutoka Chad wanacheza klabu kubwa Hispania, kwa nini isiwe Tanzania? Lazima tuamini juu ya mpango huu na tujue ni mpango wa muda mrefu, lazima tujue tunapaswa kuwa na mapenzi, wakati mwingine tuwe na njaa ya mafanikio, kwa sababu tunataka kusonga mbele. Lazima tujue wakati mwingine tunapaswa kuwafanya wachezaji watambue majukumu yao ambayo watu wanatarajia kutoka kwao. Hivyo ni suala la pamoja, si la mtu mmoja. Uzalendo, utaifa uwekwe mbele.  
    Bin Zubeiry Sports – Online; Mtihani wako wa kwanza utakuwa ni mechi dhidi ya Uganda Septemba 8 mjini Kampala, baada ya sare ya 1-1 nyumbani na Lesotho Juni 10, mwaka jana kwenye mechi ya kwanza ya kundi L. Unasemaje?
    Emmanuel Amunike; Tunakwenda kucheza na Uganda tukijua nao soka yao imepanda mno, walikuwepo kwenye AFCON iliyopita, tumeona kiwango chao kimekuwa. Hivyo tumeona timu zote Afrika zimekua, kitu cha muhimu ni si tunakwenda kucheza na nani, bali ni kuona namna tunaweza kujitazama kama timu na kukuza kiwango chetu cha mchezo. Namna ya kujihami tunapokuwa hatuna mpira, tunajilinda vipi tunapokuwa tuna mpira na kwa ujumla tunachezaje, hayo ndiyo mambo muhimu. Tukishayafanya yote, tunaweza kusema tuko tayari kwenda Uganda angalau kwenda kucheza vizuri na kupata matokeo mazuri. Lakini cha muhimu kwa sasa ni kuitazama timu yetu wenyewe. 
    Bin Zubeiry Sports – Online; Taifa Stars ilicheza kwa mara ya mwisho Machi 27 dhidi ya DRC (Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo) ikashinda 2-0, uliiona hiyo mechi? 
    Emmanuel Amunike; Niliifuatilia hiyo mechi, lakini sikuiona
    Bin Zubeiry Sports – Online; Unafahamu kuhusu kikosi cha timu yetu ya taifa ya sasa? 
    Emmanuel Amunike; Nimeiona timu yetu, nina baadhi ya mechi zenu, baadhi ya video zenu. Lakini nafikiri suala si kikosi cha sasa, si juu ya namna ya kikosi cha sasa au kipya. Ukitaka kujenga timu unapaswa kuangalia namna gani unaweza kupata wachezaji watakaotuwakilisha vizuri,
    Bin Zubeiry Sports – Online; Kwa sasa una mwezi mmoja kabla ya kukutana na Uganda, utafanyeje kupata kikosi chako?
    Emmanuel Amunike; Tutajadiliana na Shirikisho, tutaona kile ambacho wanacho kwa sasa tutawakusanya na kuona akina nani watatufaa kwa timu ya taifa ndiyo tutakwenda nao Uganda, hivyo ndivyo mambo yanakwenda. 
    Bin Zubeiry Sports – Online; Hakuna mabadiliko makubwa kutoka timu uliyoiona ikicheza na Tanzania miaka miwili iliyopita, unafikiri wachezaji wale wanaweza kuipeleka Taifa Stars AFCON ijayo?  
    Emmanuel Amunike; Kwa nini hapana, wanaweza ikiwa tunaamini juu ya tunachokifanya, tunapaswa kujituma tunaweza kutimiza ndoto, kwa sasa tunaota kwenda AFCON, tufanye kazi na tuwe na mpango wa kutimiza hilo, ikiwa tunaamini kama Watanzania, kama taifa, tunaweza.
    Bin Zubeiry Sports – Online; Tunaweza kuwa na ndoto za siku moja Tanzania kuwa na winga mzuri wa kiwango chako enzi zako?
    Emmanuel Amunike; Hiyo ndiyo ndoto yangu, tena kuwa na mchezaji mmoja mzuri kuliko mimi, siyo kama mimi. Jukumu lango kama kocha ni kukuza uwezo wa mchezaji mmoja mmoja, kuhakikisha nawainua kutoka kiwango chao cha sasa hadi kuwa bora zaidi. Leo mimi ni Mtanzania, ninaishi hapa, nitaishi hapa, nitakula hapa nitahusiana na watu wa hapa, hivyo tunapaswa kumuamini Mungu. Tunaweza kufuzu AFCON, tunatakiwa kufanya kazi kwa mujibu wa mpango wetu, hatua kwa hatua na kuona namna tutakavyokua. 
    Bin Zubeiry Sports – Online; Tanzania inakuwa timu yako ya kwanza kabisa ya wakubwa kufundisha, unaanzia hapa kutafuta uzoefu? 
    Emmanuel Amunike; Kwa maana ya kazi rasmi, lakini nimeanza kupata uzoefu katika timu ya wakubwa ya Nigeria kama kocha Msaidizi wa Nigeria, alipoondoka Sunday Oliseh nilikuwa ninamsaidia Samson Siasia. Lakini ni kweli hii ni mara yangu ya kwanza nitakuwa kazini kama Kocha Mkuu wa timu ya wakubwa ya taifa. Lakini si kuhusu nafasi au chochote, naamini hakuna mtu alizaliwa na uzoefu. Kwenye maisha unapata uzoefu kwa kufanya shughuli ya fani yako
    Bin Zubeiry Sports – Online; Uko tayari kukabiliana na matatizo sugu ya Afrika, yakiwemo ya kifedha na miundombinu?
    Emmanuel Amunike; Mimi si mgeni Afrika, hii si mara ya kwanza, nimekuwa timu za taifa za Nigeria kwanza kama mchezaji na kocha pia, wakati wote kuna changamoto hizo. Nitakabiliana nazo.
    Bin Zubeiry Sports – Online; Ikitokea mishahara ikachelewa kwa miezi miwili, au mitatu, utavumilia na kuendelea kufanya kazi, au utagoma?  
    Emmanuel Amunike; Wakati ukifika ndiyo tutaona cha kufanya, lakini sifikiri kama ninafanya kazi na watu wa aina hiyo, cha muhimu ni kufikiria namna ya kuendeleza soka hapa.
    Bin Zubeiry Sports – Online; Ujumbe wako kwa Watanzania? Wanatakiwa kuamini juu ya timu yao, kuisapoti timu yao, kuwatia moyo wachezaji wao, wanatakiwa kuamini siku moja timu yao itawapa furaha. Huo ndio ujumbe wangu. Siwaambii watu ninakwenda kufanya miujiza, ninachowahakikishia ninakwenda kujaribu na kujituma, kwa sababu ninafahamu kujituma kutakufikisha sehemu, na huo ndio ufunguo wa mafanikio. 
    Emmanuel Amunike; Ninashukuru sana kocha, ninafikiri kwa leo inatosha
    Bin Zubeiry Sports – Online; Asante sana. Karibu tena.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AMUNIKE: HATA NIGERIA ILIPITIA ILIPO TANZANIA, IMANI NA KUJITUMA VITATUPANDISHA KWENYE KILELE CHA MAFANIKIO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top