• HABARI MPYA

  Thursday, August 09, 2018

  AMRI SAID ‘STAM’ AELEZEA MIKAKATI YAKE MBAO FC LIGI KUU MSIMU UJAO

  Na Mwandishi Wetu, MWANZA
  KOCHA wa Mbao FC, Amri Said ‘Stam’ amesema kwamba lengo lake ni kuifanya Mbao FC imalize ndani ya timu 10 za juu kwenye msimu ujao wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
  Akizungumza mjini hapa, Amri amesema kwamba  kwa misimu yote miwili iliyopita, Mbao FC ilikuwa inapigania kuepuka kushuka daraja dakika za mwishoni, lakini msimu huu anataka kubadilisha mambo.
  “Kuzungunzia ubingwa au kumaliza ndani ya tatu bora, huko parefu, mpira wa Tanzania una mambo mengi sana, lakini kujihakikishia kumaliza ndani ya timu 10 za juu hilo ndilo langu,”amesema.
  Amri amesema maandalizi yake kuelekea msimu mpya wa Ligi Kuu yanaendelea vizuri na vijana wake wana hamu kubwa ya kucheza.

  Amri Said ‘Stam’ amesema lengo lake ni kuifanya Mbao FC imalize ndani ya timu 10 za juu 

  “Najivunia kuwa na aina ya vijana wenye kiu, wenye njaa ya mafanikio ambao wanataka kucheza kuonekana na kuonyesha uwezo wao ili wapate mafanikio,”amesema Amri.
  Beki huyo wa zamani wa Simba SC, amejiunga na Mbao FC mwezi Juni akitokea Lipuli FC ya Iringa, akichukua nafasi ya Fulgence Novatus ambaye naye alirithi mikoba ya Mrundi, Ettienne Ndayiragijje aliyehamia KMC ya Dar es Salaam.
  Ligi Kuu inatarajiwa kuanza Agosti 22 kwa mechi za ufunguzi kati ya Alliance na Mbao FC Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza, Ruvu Shooting na Ndanda FC ya Mtwara Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani, na Coastal Union na Lipuli FC ya Iringa Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga. 
  Mechi nyingine ni kati ya Singida United na Biashara United Uwanja wa Namfua, Singida, Kagera Sugar na Mwadui FC Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba zote Saa 10:00 jioni na Simba SC na Tanzania Prisons Saa 1:00 usiku Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam. 
  Mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu utakamilishwa Agosti 23 kwa mechi kati ya JKT Ruvu na KMC Saa 8:00 mchana Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Stand United na African Lyon Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga, Mtibwa Sugar na Yanga SC Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro na Azam FC dhidi ya Mbeya City Saa 1:00 usiku.
  Ligi Kuu itafikia tamati Mei 19, mwakani (2019) ikiwa na jumla ya mechi 380 kutoka 240 msimu uliopita baada ya ongezeko la timu nne kutoka 16 za msimu uliopita.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: AMRI SAID ‘STAM’ AELEZEA MIKAKATI YAKE MBAO FC LIGI KUU MSIMU UJAO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top