• HABARI MPYA

    Sunday, July 08, 2018

    ULIMWENGU AANZA VYEMA LIGI YA SUDAN, AFUNGA MAWILI EL HILAL YAICHAPA 4-0 MERREIKH

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Thomas Emmanuel Ulimwengu jana amefunga mabao mawili timu yake mpya, Al Hilal Omdurman ikiibuka na ushindi wa 4-0 dhidi ya Merreikh El-Fasher katika mchezo wa Ligi Kuu ya Sudan.
    “Ninamshukuru Mungu jana nimefunga mabao mawili katika mchezo wangu wa kwanza wa Ligi Kuu ya Sudan, tumeshinda 4-0,”amesema Ulimwengu akizungumza na Bin Zubeiry Sports – Online kutoka Sudan mapema leo.
    Mbali na Ulimwengu kufunga mabao mawili katika mchezo huo uliofanyika Uwanja wa Al-Hilal, mabao mengine yalifungwa na Walid mawili pia. 
    Mwezi uliopita Emmanuel Ulimwengu alisaini mkataba wa kujiunga na El Hilal ya Sudan baada ya kuachana na AFC Eskilstuna ya Sweden.
    Ulimwengu amerejea uwanjani baada ya kupona maumivu ya goti kufuatia kufanyiwa upasuaji katika hospitali ya Taasisi ya Sayansi ya Michezo mjini Cape Town, Afrika Kusini mwaka jana na kupitia kipindi kirefu cha mazoezi ya kujiweka fiti.
    Thomas Ulimwengu (kushoto) akipongezwa na mwenzake baada ya kuifungia El HIlal mabao mawilu 

    Thomas Ulimwengu (kushoto) akimtoka mchezaji wa El Merreikh  

    Ulimwengu alikwenda kwa watalaamu nchini Italia kufanyishwa mazoezi maalum ya kumuweka fiti haraka arejee uwanjani, ambayo hakika yamemsaidia na sasa anajiunga na vigogo wa Sudan wanaoongoza Ligi ya kwao.
    Maumivu ya goti yamekuwa yakimsakama Ulimwengu tangu alipojiunga na Eskilstuna Januari mwaka jana akitokea Tout Puissant Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kiasi cha kushindwa kucheza. 
    Ulimwengu aliyezaliwa Juni 14, mwaka 1993 aliibukia katika taasisi ya soka Tanzania (TSA) mwaka 2008, kabla ya mwaka 2009 kwenda kuanza kukomazwa Ligi Kuu katika klabu ya Moro United alikokuwa akicheza kwa mkopo hadi mwaka 2010 alipokwenda akademi ya AFC Eskilstuna ya Sweden, alikocheza hadi mwaka 2011  alipochukuliwa na timu ya vijana ya Mazembe.
    Alicheza U-20 ya Mazembe kwa msimu moja kabla ya kupandishwa rasmi timu ya wakubwa mwaka 2012 na moja kwa moja kuwa mchezaji wa kikosi cha kwanza hadi anamaliza Mkataba wake Oktoba mwaka jana.
    Ulimwengu alihamia Ulaya baada ya kushinda mataji makubwa akiwa na  Mazembe kama Ligi ya Mabingwa Afrika, Super Cup ya Afrika na pamoja na kucheza Klabu Bingwa ya Dunia.  
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: ULIMWENGU AANZA VYEMA LIGI YA SUDAN, AFUNGA MAWILI EL HILAL YAICHAPA 4-0 MERREIKH Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top