• HABARI MPYA

  Sunday, July 08, 2018

  TFF IJITATHMINI MARA MBILI NAMNA INAVYOENDESHA SOKA YA TANZANIA

  MOJA kati ya mambo ambayo yamekuwa yakilalamikiwa kwa kiasi kikubwa kwenye soka ya Tanzania ni uchezeshaji wa marefa.
  Marefa wa Tanzania pamoja na kuwa wa kiwango cha chini, lakini pia wana matatizo mengine makubwa ya ufahamu, utimamu wa mwili, uadilifu, uaminifu na weledi.
  Yote yanasababisha dosari nyingi katika michezo mbalimbali ya mashindano tofauti nchini na si ajabu thamani yao ni ya chini mno kwenye medani ya kimataifa.
  Marefa wa Tanzania hawana nafasi pana hata kwenye michuano ya ukanda huu pekee, inayoandaliwa na Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).

  Hiyo ni kwa sababu CECAFA inaujua udhaifu wao na kwa kuwa haitaki kuyatia doa mashindano yake, imeona bora iyaweke mbali kidogo na marefa wa Tanzania.
  Ilitarajiwa, kwa kiasi kikubwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lingewekeza katika kupambana na mapungufu hayo ya marefa nchini, kwa sababu hao ni watu muhimu mno.
  Ili upate mshindi halali wa mchezo, lazima upate refa mzuri wa kuchezesha mechi kwa haki, uadilifu, uaminifu na kufuata sheria 17 zinazosimamia mchezo wenyewe.
  Mwisho wa siku ili upate bingwa wa halali wa mashindano yako, unahitaji marefa wenye sifa stahiki ili wachezeshe mechi kwa kufuata sheria 17.
  Na pia, ili kuhakikisha hauhatarishi amani viwanjani, unapaswa kuwa na marefa wenye sifa hizo, ili mashabiki wasighadhibishwe kwa maamuzi mabovu na kufanya vurugu viwanjani.
  Vurugu kwa sababu ya uchezeshaji mbovu wa marefa zimetokea sana Tanzania na kuna wakati zilimkera hadi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Joseph Magufuli akataka kuzuia Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam kutumika kwa mechi za soka.
  Hiyo ni baada ya maamuzi ya utata ya refa Martin Saanya kusababisha vurugu Uwanja wa Taifa Jumamosi ya Oktoba 1, mwaka 2016 baada ya Yanga kupata bao la kuongoza dhidi ya mahasimu wake wa jadi, Simba SC lililofungwa na mshambuliaji Mrundi, Amissi Joselyn Tambwe katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
  Tambwe alifunga bao hilo dakika ya 26, akimalizia pasi ndefu ya beki Mbuyu Twite na kugeuka mbele ya beki wa Simba, Novat Lufunga kabla ya kufumua shuti lililomshinda kipa Vincent Angban kutoka Ivory Coast.
  Bao hilo lilizua kizaazaa, wachezaji wa Simba wakimvaa refa Martin Saanya wakidai mfungaji, Tambwe aliushika mpira kabla ya kufunga. Na katika vurugu hizo, Saanya alimtoa kwa kadi nyekundu Nahodha wa Simba SC, Jonas Mkude dakika ya 29 kwa sababu ndiye aliyekuwa mstari wa mbele.
  Mchezo ukasimama kwa takriban dakika tano baada ya mashabiki wa Simba kuanza kufanya vurugu waking’oa viti na kutupa uwanjani. Polisi walitumia milipuko ya gesi za kutoa machozi kuwatuliza mashabiki hao na mchezo ukaendelea hadi Simba SC wakasawazisha dakika ya 87 kwa bao la Shizza Kichuya.
  Lakini baadaye Rais Magufuli akasamehe baada ya TFF kuwaamuru Simba SC kulipa gharama za uharibifu uliotokea. Kuna kitu nataka niwakumbushe viongozi wa soka yetu, aliyekuwa Rais wa FIFA, Sepp Blatter aliwahi kusema miaka ya 1990 soka na vurugu ni chanda na pete, mashabiki wakipata hasira wanafanya fujo.
  Akawataka marefa kuwa makini katika uchezeshaji wao kwa kuhakikisha wanatenda haki ili wasiumize upande wowote kuepusha vurugu uwanjani.
  Wazi ni wajibu wa mamlaka za soka kuhakikisha zinaboresha viwango vya waamuzi kwa namna zote, kiuchezeshaji, uadilifu na uaminifu.
  Lakini katika mastaajabu ya wengi, jana TFF imesema marefa watakaoshiriki Kozi ya Utimamu wa mwili kwa ajili ya kuchezesha mechi za Ligi Kuu, Daraja la kwanza (FDL) na Daraja la Pili (SDL) msimu wa 2018/2019 watajigharamia kwenda vituoni Mwanza na Dar es Salaam.
  Taarifa ya Ofisa Habari wa TFF, Clifford Mario Ndimbo ilisema kwamba kozi hiyo itahusisha waamuzi wote wa Daraja la Kwanza nchini, waliochezesha Ligi ya Mabingwa wa Mikoa(RCL) na waliochezesha mashindano ya U20 ya Uhai Cup.
  "Kila Mwamuzi atatakiwa kujigharamia na ndio maana TFF imeweka vituo viwili ili kupunguza makali ya gharama. Kila Mwamuzi atatakiwa kuja na Passport size 2 kwaajili ya kuingia kwenye data za kiuamuzi na atatakiwa kujaza fomu ya taarifa binafsi,"imesema taarifa.
  Kituo cha Dar es Salaam kitakuwa na mikoa ya Dar es Salaam yenyewe, Pwani, Morogoro, Dodoma, Tanga, Iringa, Njombe, Mbeya, Ruvuma, Songwe, Lindi, Mtwara na Katavi.
  Kituo cha Mwanza kitakuwa na Mwanza yenyewe, Kagera, Geita, Mara, Simiu, Shinyanga, Kigoma, Tabora, Singida, Manyara, Arusha, Kilimanjaro na Rukwa.
  Maana yake refa ambaye hatakuwa na uwezo wa kujigharamia kwenda kwenye hizo kozi hata kama ndiye bora, mwenye kukidhi vigezo vingine vyote vya kitaaluma hataweza kushiriki – na kama hatashiriki hatapangwa kuchezesha ligi yoyote nchini msimu ujao.
  Maana yake marefa wenye uwezo wa kifedha ndiyo watakaochangamkia kozi hizo hata kama wana mapungufu makubwa kitaalama na hawana sifa – yaani hao ndiyo watakaochezesha Ligi za Tanzania msimu ujao.
  TFF inayoshindwa kugharamia kozi za waamuzi ndiyo ambayo inatuhumiwa kiitisha vikao na Wahariri wa Vyombo vya Habari inawapa ‘posho nene’ na inatumia fedha nyingine nyingi katika maumizi ambayo hayana tija kwa mchezo wenyewe.
  Lakini Ligi Kuu ina udhamini wa Vodacom na Azam TV pamoja na makampuni mengine ambayo yamekuwa yakiingia na kutoka – iweje ikosekane bajeti japo isiyohusisha posho, igharamie tu usafiri, malazi na chakula pekee kwa marefa wanaokwenda kushiriki kozi hizo?
  Ipo haja ya TFF kujitathmini mara mbili namna inavyoendesha soka ya Tanzania. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: TFF IJITATHMINI MARA MBILI NAMNA INAVYOENDESHA SOKA YA TANZANIA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top