• HABARI MPYA

  Wednesday, July 11, 2018

  TENERIFE YAMZUIA SHAABAN IDDI KUCHEZEA AZAM FC KOMBE LA KAGAME, YAHOFIA ATAUMIA

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  KLABU ya CD Tenerife ya Daraja la Kwanza nchini Hispania imemzuia mshambuliaji Shaaban Iddi Chilunda kuendelea kuchezea Azam FC katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame inayoendelea mjini Dar es Salaam ikiwa imefikia hatua ya Nusu Fainali.
  Meneja wa Azam FC, Philipo Alando ameiambia Bin Zubeiry Sports – Online leo kwamba klabu hiyo ya Santa Cruz mjini Tenerife, visiwa vya Canary imetuma barua kuizuia Azam FC kuendelea kumtumia mchezaji huyo kwa sababu tayari wameingia mkataba wa kuuziana kwa mkopo.
  CD Tenerife iliyomnunua kwa mkopo Chilunda wiki iliyopita baada ya kuvutiwa na mchezaji mwingine wa Tanzania, Farid Mussa kutoka akademi ya Azam pia - imesema inahofia mchezaji huyo anaweza kuumia kwenye mashindano ya Kagame.

  Shaaban Iddi (kulia) amezuiwa kucheza michuano ya Kombe la Kagame na klabu yake mpya, CD Tenerife ya Hispania 

  “Tumewaandikia barua CD Tenerife kuwaomba wamruhusu kuchea kumalizia hizi mechi mbili tu, kwa hivyo tunasikilizia majibu yao, nafikiri hadin kufika saa sita mchana tunaweza kuwa majibu kamili kama atacheza au la,”amesema Alando, mshambuliaji wa zamani wa Azam FC.
  Shaaban Iddi ambaye atatimiza miaka 20 Julai 20 mwaka huu tangu azaliwe mwaka 1998, alijiunga na akademi ya Azam FC Jumamosi ya Julak 21, mwaka 2012 kabla ya miaka miwili baadaye kupandishwa kikosi cha kwanza.
  Na tayari katika michuano ya Kombe la Kagame anaelekea kuwa mfungaji bora hadi sasa akiwa amefunga mabao saba, yakiwemo manne ya rekodi katika mchezo wa Robo Fainali dhidi ya Rayon Sport ya Rwanda.
  Kumbukumbu zinaonyesha hakuna mchezaji aliyewahi kufunga mabao manne katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati tangu inaanzishwa mwaka 1974 – maana yake chipukizi wa Tanzania ameweka rekodi mpya.
  Na heshima zaidi kwake amefunga dhidi ya timu ngumu yenye safu imara ya ulinzi, Rayon Sport ambao pia wanashiriki Kombe la Shirikisho Afrika wakiwa Kundi moja na vigogo wa Tanzania, Yanga SC.
  Tayari Chilunda amekwishafunga mabao saba katika michuano ya Kombe la Kagame mwaka huu, pamoja na mawili dhidi ya Kator FC ya Sudan Kusini na moja dhidi ya Vipers FC katika hatua ya makundi.
  Na zaidi ya hayo, anasifiwa kufunga bao zuri zaidi kwenye mashindano haya hadi sasa, ambalo ni dhidi ya Vipers FC ya Uganda akimpiga kanzu kipa kabla ya kutumbukiza mpira nyavuni.
  Mabao saba ndiyo kiwango cha juu hadi sasa cha wafungaji bora wa michuano ya Kagame, idadi ambayo mara ya mwisho ilifikiwa na mshambuliaji Chiukepo Msowoya wa APR mwaka 2010 nchini Rwanda.
  Na kwenye idadi kubwa ya mabao katika mchezo mmoja, mara ya mwisho mchezaji mmoja kufunga mabao mengi ilikuwa mwaka 2013 na huyo ni Mrundi, Amissi Tambwe akiwa na Vital'O ya kwao aliifunga mabao matatu dhidi ya AS Ports ya Djibouti katika ushindi wa 6-0, mchezo wa Robo Fainali.
  Na kabla ya hapo, hat trick nyingine ya Kagame ilifungwa na John Raphael Bocco mwaka 2012 akiwa na Azam FC akiiadhibu timu yake ya sasa, Simba SC kwenye Robo Fainali pia. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: TENERIFE YAMZUIA SHAABAN IDDI KUCHEZEA AZAM FC KOMBE LA KAGAME, YAHOFIA ATAUMIA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top