• HABARI MPYA

    Monday, July 09, 2018

    TARIMBA ‘KULIPUA BOMU’ YANGA SC KESHO…NI BAADA YA KUCHOSHWA NA MAMBO YA SANGA

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    PAMOJA na kujiuzuulu Uenyekiti wa Kamati Maalum ya Kusimamia shughuli za Uendeshwaji wa klabu ya Yanga, Tarimba Abbas kesho anatarajiwa kukutana na Waandishi wa Habari kuzungumzia nafasi yake na mustakabali wa klabu.
    Tarimba ameiambia Bin Zubeiry Sports – Online leo kwamba amejiuzulu Uenyekiti wa Kamati na kesho atazungumza na Waandishi wa Habari katika mkutano utakaofanyika mchana katika ukumbi ambao utajulikana mapema kesho asubuhi.
    Japokuwa Tarimba hakusema anataka kuzungumzia nini, lakini Bin Zubeiry Sports – Online inafahamu ametofautiana na Kaimu Mwenyekiti wa klabu hiyo, Clement Sanga kiasi cha kufikia uamuzi wa kujiuzulu.
    Juni 10, mwaka huu katika Bwalo la Maafisa wa Jeshi la Polisi, Oysterbay, Dar es Salaam, wanachama wa Yanga SC waliunda Kamati ya watu tisa chini ya Rais wa zamani wa klabu, Tarimba Abbas na wanachama wa Yanga Kusimamia Shughuli mbalimbali za klabu hiyo kufuatia kile kinachoonekana kuelemewa kwa uongozi uliopo madarakani sasa chini ya Kaimu Mwenyekiti, Sanga.

    Tarimba Abbas (kulia) kesho anatarajiwa kukutana na Waandishi wa Habari kuzungumzia mustakabali wa klabu chini ya Mwenyekiti, Clement Sanga 

    Mwenyekiti Mteule wa Kamati hiyo ni Tarimba Abbas, Makamu wake, Saidy Meckysadik na Wajumbe wa Kamati hiyo ni Abdallah Bin Kleb, Hussein Nyika, Samuel Lukumay, Lucas Mashauri, Yusuphed Mhandeni, Hamad Islam, Makaga Yanga, Ridhiwani Kikwete, Majjid Suleiman na Hussein Ndama.
    Na hiyo ni kutokana na kupwaya kwa Kamati ya Utendaji kutoka uongozi uliochaguliwa Juni mwaka 2016 imepungua mno baada ya kujiuzulu kwa Mwenyekiti mwenyewe, Yussuf Manji na Wajumbe wa Omary Said Amir, Salum Mkemi, Ayoub Nyenzi na Hashim Abdallah.  
    Waliobaki katika Kamati ya Utendaji pamoja na Sanga ni Wajumbe wanne, Siza Augustino Lymo, Tobias Lingalangala, Samuel Lukumay na Hussein Nyika.
    Na katika Kamati iliyoteuliwa Juni 10, tayari Mjumbe mmoja, Abdallah Bin Kleb amekataa uteuzi wake akisema kwamba anakabiliwa na matatizo ya kiafya na pia amebanwa na majukumu yake mengine ya biashara zake.
    Bin Kleb aliibuka kuukana uteuzi huo wakati kuna taarifa kwamba Sanga amegoma kufanya kazi na Kamati hiyo na anataka aendelee na watu aliokuwa nao akina Siza, Lukumay, Lingalangala na Nyika.
    Inadaiwa jana Sanga alikutana na viongozi wa Matawi na kuiponda Kamati ya Tarimba huku akisema kwamba Mwenyekiti wa klabu, Yussuf Manji ameomba miezi mitatu kabla ya kurejea kuendelea na majukumu yake klabuni.
    Juni 10, mwaka huu katika Bwalo la Maafisa wa Jeshi la Polisi, Oysterbay, Dar es Salaam, wanachama wa Yanga SC pamoja na kuunda Kamati ya Tarimba, pia waligomea ombi la Mei mwaka jana la Mwenyekiti wao, Manji kujiuzulu na kusema bado wanamtambua kama kiongozi wao mkuu.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TARIMBA ‘KULIPUA BOMU’ YANGA SC KESHO…NI BAADA YA KUCHOSHWA NA MAMBO YA SANGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top