• HABARI MPYA

  Monday, July 09, 2018

  SINGIDA UNITED YATUPWA NJE KWA MATUTA KOMBE LA KAGAME…NUSU FAINALI NI SIMBA NA JKU, AZAM NA GOR MAHIA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  SAFARI ya Singida United katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame imefikia tamati katika hatua ya Robo Fainali baada ya kutolewa na JKU Zanzibar kwa penalti 4-3 kufuatia sare ya 0-0 usiku wa leo Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
  Kwa matokeo hayo, JKU itakutana na Simba SC katika Nusu Fainali Jumatano, siku ambayo Azam FC itamenyana na Gor Mahia, mechi zote zikipigwa Uwanja wa Taifa.
  Mapema katika Nusu Fainali ya kwanza, mabingwa watetezi, Azam FC waliichapa mabao 4-2 Rayon Sport ya Rwanda Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
  Pongezi kwake shujaa wa timu hiyo leo, mshambuliaji chipukizi, Shaaban Iddi Chilunda aliyefunga mabao yote manne peke yake katika dakika za 19, 33, 39 na 64 katika michuano yake ya kwanza ya Kombe la Kagame.

  Ikumbukwe Chilunda anacheza kwa mara ya mwisho Azam FC kabla ya kwenda Hispania kuanza kuutumikia mkataba wa mkopo wa miaka miwili Tenerife ya Daraja la Pili Hispania.
  Mabao ya Rayon Sports inayoshiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika ikiwa Kundi D pamoja na vigogo wa Tanzania, Yanga SC yamefungwa na Rwatubyaye Abdul dakika ya 42 na Manishimwe Djabel dakika ya 81.
  Simba na Gor Mahia zilitangulia Nusu Fainali ya michuano hiyo inayofanyika kwa mara ya kwanza baada ya miaka mitatu jana, kufuatia kuzitoa Vipers ya Uganda na AS Ports ya Djibouti.
  Ilianza Gor Mahia kutoka nyuma na kushinda 2-1, baada ya kutanguliwa na Vipers kwa bao la Thadeo Lwanga dakika ya 17, kabla ya kuzinduka na kusawazisha kwa mabao ya Francis Mustafa dakika ya 48 na 75.
  Mchezo wa pili, Mohamed Rashid akatokea benchi dakika ya 59 kwenda kuchukua nafasi ya Adam Salamba na kuifungia Simba bao pekee dakika ya 65 dhidi ya AS Ports.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SINGIDA UNITED YATUPWA NJE KWA MATUTA KOMBE LA KAGAME…NUSU FAINALI NI SIMBA NA JKU, AZAM NA GOR MAHIA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top