• HABARI MPYA

    Monday, July 09, 2018

    SANGA AWAAMBIA VIONGOZI WA MATAWI JANGWANI; “MANJI AMEOMBA MIEZI MITATU AREJEE YANGA”

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KAIMU Mwenyekiti wa Yanga SC ya Dar es Salaam, Clement Sanga amesema kwamba Mwenyekiti wa klabu, Yussuf Manji ameomba miezi mitatu kabla ya kurejea kuendelea na majukumu yake klabuni.
    Sanga alisema hayo jana katika kikao chake na viongozi wa matawi ya klabu kilichofanyika makao makuu ya klabu, Jangwani, Dar es Salaam.
    Kwa mujibu wa habari ambazo Bin Zubeiry Sports – Online imezipata kutoka kwenye kikao hicho, Sanga aliitisha kikao hicho kujadili pamoja na wanachama hali halisi ndani ya klabu kwa sasa.

    Ni kweli Yussuf Manji ameomba miezi mitatu kabla ya kurejea kuendelea na majukumu yake klabuni?

    Juni 10, mwaka huu katika Bwalo la Maafisa wa Jeshi la Polisi, Oysterbay, Dar es Salaam, wanachama wa Yanga SC waligomea ombi la Mei mwaka jana la Mwenyekiti wao, Manji kujiuzulu na kusema bado wanamtambua kama kiongozi wao mkuu.
    Pamoja na hayo, wanachama hao waliunda Kamati ya watu tisa chini ya Rais wa zamani wa klabu, Tarimba Abbas na wanachama wa Yanga Kusimamia Shughuli mbalimbali za klabu hiyo kufuatia kile kinachoonekana kuelemewa kwa uongozi uliopo madarakani sasa chini ya Kaimu Mwenyekiti, Sanga.
    Mwenyekiti Mteule wa Kamati hiyo ni Tarimba Abbas, Makamu wake, Saidy Meckysadik na Wajumbe wa Kamati hiyo ni Abdallah Bin Kleb, Hussein Nyika, Samuel Lukumay, Lucas Mashauri, Yusuphed Mhandeni, Hamad Islam, Makaga Yanga, Ridhiwani Kikwete, Majjid Suleiman na Hussein Ndama.
    Idadi ya Wajumbe wa Kamati ya Utendaji kutoka uongozi wa Manji uliochaguliwa Juni mwaka 2016 imepungua mno baada ya kujiuzulu kwa Mwenyekiti mwenyewe, Omary Said Amir, Salum Mkemi, Ayoub Nyenzi na Hashim Abdallah.  
    Waliobaki katika Kamati ya Utendaji pamoja na Sanga ni Wajumbe watatu, Siza Augustino Lymo, Tobias Lingalangala na Hussein Nyika.
    Na katika Kamati iliyoteuliwa Juni 10, tayari Mjumbe mmoja, Abdallah Bin Kleb amekataa uteuzi wake akisema kwamba anakabiliwa na matatizo ya kiafya na pia amebanwa na majukumu yake mengine ya biashara zake.
    Pamoja na Tarimba kusema mwezi huu kwamba wanafanya shughuli zao kimya kimya, lakini haionyeshi kama kuna ushirikiano wowote baina ya Kamati ya Utendaji iliyopelea na Kamati iliyoteliwa na wanachama Juni 10.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SANGA AWAAMBIA VIONGOZI WA MATAWI JANGWANI; “MANJI AMEOMBA MIEZI MITATU AREJEE YANGA” Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top