• HABARI MPYA

  Thursday, July 12, 2018

  SAMATTA AWAHOFIA MABEKI ‘MAGAIDI’ UBELGIJI MSIMU MPYA WA LIGI ZA ULAYA UKIKARIBIA KUANZA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  WAKATI msimu mpya wa Ligi mbalimbali Ulaya unakaribia kuanza, hofu kubwa ya mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta anayechezea KRC Genk ya Ubelgiji ni juu ya mabeki ‘magaidi’.
  Ligi mbalimbali Ulaya na duniani kwa ujumla zinatarajiwa kuanz akuchezwa kuanzia Agosti baada ya kumalizika Mei mwaka huu.
  Na Samatta ametumia ukurasa wake wa Instagram kuelezea hisia zake kuelekea msimu ujao, akisema; “Muda wa kuanza kukimbizana na mabeki unakaribia, ila kuna mibeki mingine ina roho mbaya basi tu hakuna jinsi, muda wa kuanza kupasuka nao unakaribia,”.
  Samatta ambaye ameposti picha akiwa na jezi mpya ya mechi za nyumbani na kuomba maoni ya mashabiki wake juu ya mwonekano wake, amesema kwamba msimu mpya unakaribia kuanza na wakati anafikiria kuanza kuwakimbiza mabeki, pia anafikiria kuumizwa na mabeki hao hao.

  Mshambuliaji wa KRC Genk ya Ubelgiji, Mbwana Samatta anawahofia mabeki ‘magaidi’ 

  Samatta amekuwa na hofu na mabeki katili tangu aumie Novemba 4, mwaka jana akiichezea KRC Genk ikilazimishwa sare ya 0-0 na Lokeren katika mchezo wa Ligi Daraja la Kwanza A Ubelgiji Uwanja wa Luminus Arena mjini Genk na kukaa nje hadi Februari huku ikimchukua hadi Aprili kuanza kuonyesha makali tena.
  Samatta alichanika mishipa midogo ya goti lake la mguu wa kulia akiichezea mechi ya 70 Genk tangu alipojiunga nayo Januari mwaka 2016 akitokea TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na alipopona akacheza mechi 20 zaidi, ingawa nyingi alitokea benchi. 
  Hadi sasa, Samatta, mshambuliaji wa zamani wa Mbagala Market, African Lyon na Simba SC ya Dar es Salaam amefunga mabao 26 katika mechi 90 za mashindano yote tangu ajiunge na Genk Januari mwaka 2016 akitoka kutwaa tuzo ya Mwanasoka Bora Anayecheza Afrika.
  Na mwakani, Samatta pamoja na mashindano ya nyumbani, kwa maana ya Ligi na Kombe la Ubelgiji, pia anatarajiwa kucheza Europa League kwa mara ya pili mfululizo.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SAMATTA AWAHOFIA MABEKI ‘MAGAIDI’ UBELGIJI MSIMU MPYA WA LIGI ZA ULAYA UKIKARIBIA KUANZA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top