• HABARI MPYA

    Thursday, July 12, 2018

    KMC YAMSAJILI KIUNGO WA TUSKER YA KENYA ALIYECHEZEA STARS KOMBE LA CHALLENGE

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    TIMU ya Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, KMC imeendelea kujipanga kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baada ya kumsajili kiungo mshambuliaji, Abdul Hillary Hassan kutoka Tusker FC ya Kenya.
    Ofisa Habari wa KMC, Walter Harrison amesema kwamba Hassan amejiunga rasmi na klabu ya KMC FC kwa mkataba wa mwaka mmoja.
    Kiungo mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 23, urefu wa futi 6 na anayetumia miguu yote kwa ufasaha anakuwa mchezaji mpya wa tano kusajiliwa KMC baada ya kipa Juma kaseja na mabeki Aaron Lulambo, Sadallah Lipangile na Ali Ali. 

    Ofisa Habari wa KMC, Walter Harrison (kushoto) akibadilishana mikataba na Abdul Hillary Hassan  

    Na hadi sasa KMC ina wachezaji saba tu wenye mikataba, wakiwemo wawili viungo Abdulhalim Humud na Adam Kingwande waliokuwemno kwenye kikosi kilichopandisha timu kutoka Daraja la Kwanza chini ya kocha Freddy Felix MInziro.
    Tayari Minziro amekwishaondolewa na nafasi yake imechukuliwa na Mrundi Ettienne Ndayiragijje ambaye misimu miwili iliyopita alikuwa Mbao FC ya Mwanza.
    Abdul Hillary Hassan ni mchezaji aliyeibukia katika kituo cha kulea vipaji vya wanasoka cha DYOC (Dar es Saalam Youth Olimpic Centre).
    Msimu wa 2014-2016 alichezea African Lyon ya Dar es Salaam katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara kabla ya kuhamia Tusker FC ya Ligi Kuu ya Kenya mwaka jana, ambayo ilimpa nafasi ya kuitwa kwenye kikosi cha Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars kwa ajili ya michuano ya CECAFA Challenge.
    Hata hivyo, Kilimanjaro Stars iliyokuwa chini ya Kocha Mkuu, Ammy Ninje haikufanya vyema katika michuano hiyo iliyofanyika nchini Kenya baada ya kutolewa hatua ya makundi tu.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KMC YAMSAJILI KIUNGO WA TUSKER YA KENYA ALIYECHEZEA STARS KOMBE LA CHALLENGE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top