• HABARI MPYA

    Monday, July 09, 2018

    KIDAU AMKAANGA MALINZI MAHAKAMANI...ASEMA HAKUKUWA NA KIKAO CHA KUBADILI MTIA SAINI

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KATIBU Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wilfred Kidau ameiambia Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa, kikao cha kamati ya utendaji ya shirikisho hilo cha Juni 5, mwaka 2016 hakikuwa na ajenda ya kubadilisha mtia saini (signatory).
    Kidau amedai hayo leo mahakamani hapo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri, alipokuwa akitoa ushahidi kwenye kesi inayomkabili aliyekuwa Rais wa TFF,  Jamal Malinzi na wenzake.
    Shahidi huyo pia aliionyesha mahakama tofauti zilizopo kwenye muhtasari wa kikao cha kamati hiyo na hati ya kubadilisha watia saini iliyopelekwa Benki ya Stanbic iliyotiwa saini na Malinzi na Katibu Mkuu wake, Celestine Mwesigwa.

    Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidau amedai kikao cha Kamati ya Utendaji Juni 5, mwaka 2016 hakikubadilisha mtia saini 

    Akiongozwa na Wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Leonard Swai, Kidau amedai alianza kazi TFF akiwa Kaimu Katibu Mkuu na pia alikuwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF kwa mwaka 2013 hadi 2017.
    Amedai majukumu ya Katibu Mkuu wa TFF ni kusimamia utendaji kazi wa sekretarieti, kama Katibu Mkuu na ndiyo ofisa mhasibu wa shirikisho hilo anayeidhinisha malipo yote. 
    Akielezea utaratibu wa kutia saini katika vikao vya kamati ya utendaji alidai, baada ya kumaliza kikao muhtasari wake hutiwa saini kikao kinachofuata baada ya wajumbe kuthibitisha yaliyomo katika kikao kilichopita. 
    Kidau amedai Juni 5, mwaka 2016 akiwa Makao Makuu ya TFF, kulikuwa na kikao cha kamati tendaji ambacho kilijadili kuhusu ripoti mbalimbali za utekelezaji wa shughuli za taasisi hiyo.
    “Mara baada ya kikao niliitwa na TAKUKURU na kuulizwa kuhusu muhtasari wa kikao hicho cha Juni 5, kama kulikuwa na ajenda za kubadilisha watia saini, ukweli ni kwamba suala la kubadilisha mtia saini halikuwa moja ya ajenda za kikao hicho.
    “Takukuru waliniuliza hivyo kwa sababu kulikuwa na muhtasari wa kikao husika na nyaraka ya mabadiliko ya watia saini iliyopelekwa Benki ya Stanbic.
    “Niliulizwa juu ya nyaraka hiyo iliyokwenda benki kama iko sawa, niligundua kulikuwa na makosa ambayo ni majina yaliyokuwa kwenye nyaraka iliyopelekwa benki, jina moja liliandikwa mara mbili Khalid Abdallah ambaye ni mjumbe wa kamati ya utendaji anayewakilisha Mkoa wa Tanga na Kilimanjaro,” amedai Kidau. 
    Shahidi mwingine ambaye ni Mjumbe wa Kamati ya Tiba ya Shirikisho la Mpira Afrika (CAF),  Dk. Paul Marealle (57), amedai suala la kubadili mtia saini haikuwa moja ya agenda ya kikao hicho.
    Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni  aliyekuwa Mhasibu wa shirikisho hilo, Nsiande Mwanga, Karani Flora Rauya na Miriam Zayumba.
    Washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka 30 yakiwamo ya kughushi, kuwasilisha nyaraka za kughushi na utakatishaji fedha.
    Kesi imeahirishwa hadi  Julai 19, mwaka huu ambapo Kidau ataendelea kutoa ushahidi.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KIDAU AMKAANGA MALINZI MAHAKAMANI...ASEMA HAKUKUWA NA KIKAO CHA KUBADILI MTIA SAINI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top