• HABARI MPYA

  Wednesday, June 13, 2018

  YANGA MWAKA WAO HUU, WATUPWA NJE UHAI CUP BILA KUPOTEZA MECHI, AZAM NA MTIBWA ZAENDA ROBO FAINALI

  Na Mwandishi Wetu, DODOMA
  YANGA SC imetupwa nje ya michuano ya Ligi Kuu ya Taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20, maarufu kama Kombe la Uhai inayoshirikisha vikosi vya pili vya klabu za Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya kulazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 na Mbeya City katika mchezo wa Kundi A leo viwanja vya Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).
  Yanga SC ilitangulia kwa bao la Paul Godfrey Nganyanya dakika ya tatu, kabla ya Grocery Wilfred Mtugo kuisawazishia Mbeya City dakika ya 11. Mechi nyingine ya kundi hilo, Ruvu Shooting imegawana pointi na Mbao FC baada ya sare ya 0-0.
  Matokeo hayo yanamaanisha Yanga B inamaliza mechi zake za Kundi A bila kufungwa wala kushinda, ikitoa sare zote tatu na kumaliza nafasi ya tatu, nyuma ya Mbao FC na Ruvu Shooting zilimaliza na pointi tano kila moja na zote zinakwenda Robo Fainali.
  Paul Godfrey alianza kuifungia Yanga dakika ya tatu, kabla ya Grocery Mtugo kuisawazishia Mbeya City dakika ya 11


  Yanga inaungana na Mbeya City iliyomaliza na pointi moja baada ya awali kufungwa na zote, Ruvu Shooting na Mbao FC kurejea nyumbani.
  Katika Kundi C, wana fainali wa msimu uliopita, Azam FC wamefanikiwa kwenda Nane Bora baada ya ushindi wa 2-1 dhidi ya Mwadui FC, mabao yake yakifungwa na Jamal Abdul Ally dakika ya 19 na Paul Peter Kasunda dakika ya 60 dhidi ya moja la Frank Mbeshi dakika ya 50.
  Nayo na Mtibwa Sugar baada ya sare ya 1-1 na Maji Maji, inamaliza kileleni mwa Kundi C kwa pointi zake tano ikiizidi kwa wastani wa mabao Azam FC na zote zinakwenda Robo Fainali.
  Hatua ya makundi inakamilishwa kesho kwa mechi nne, mbili za Kundi B kati ya mabingwa watetezi, Simba SC na Stand United na Singida United na Njombe Mji FC na mbili za Kundi D kati ya Ndanda FC na Lipuli na Kagera Sugar na Tanzania Prisons.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA MWAKA WAO HUU, WATUPWA NJE UHAI CUP BILA KUPOTEZA MECHI, AZAM NA MTIBWA ZAENDA ROBO FAINALI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top