• HABARI MPYA

    Sunday, June 10, 2018

    WANACHAMA YANGA WAMREJESHA MANJI MADARAKANI, TARIMBA APEWA JUKUMU LA KUSAJILI WACHEZAJI WAPYA

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    WANACHAMA wa klabu ya Yanga kwa kauli moja wamekubaliana kumrejesha madarakani, Mwenyekiti wao Yussuf Mehboob Manji katika mkutano Mkuu wa mwaka uliofanyika Bwalo la Maafisa wa Jeshi la Polisi, Oysterbay, Dar es Salaam leo.
    Pamoja na kumrejesha Maji aliyejiuzulu Mei mwaka jana, wanachama hao wameunda Kamati ya watu tisa chini ya Rais wa zamani wa klabu, Tarimba Abbas na Makamu wake, Saidy Meckysadik, kusimamia usajili na mambo mengine muhimu ya klabu kwa sasa.
    Wajumbe wa Kamati hiyo ni Abdallah Bin Kleb, Hussein Nyika, Samuel Lukumay, Lucas Mashauri, Yusuphed Mhandeni, Hamad Islam, Makaga Yanga, Ridhiwani Kikwete, Majjid Suleiman na Hussein Ndama.
    Akizungumza na Waandishi wa Habari baada ya mkutano huo, Kaimu Katibu Mkuu, Charles Boniface Mkwasa amesema kwamba agizo la Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harison Mwakyembe kufanyika kwa uchaguzi wa kuziba nafasi za viongozi waliojiuzulu ndani ya miezi miwili pia linafanyiwa kazi.

    Wanachama wa Yanga kwa kauli moja wamekubaliana kumrejesha madarakani, Mwenyekiti wao Yussuf Manji 

    Mkwasa pia amesema kwamba wameridhia mwongozo wa mabadiliko ya uendeshwaji wa klabu kwa kuingia kwenye soko la hisa na kwamba mchakato wa zoezi hilo unashughulikiwa na Wakili maarufu, Alex Mgongolwa. 
    Mapema akifungua mkutano huo, Waziri Mwakyembe pamoja na kuipongeza Yanga kwa klabu yenye mafanikio makubwa nchini, pia aliwapa miezi wawe wamefanya uchaguzi ili kuziba mapengo ya viongozi walioondoka.
    Waziri Mwakyembe amesema Yanga inahitaji kuwa na uongozi imara utakaosajili wachezaji wazuri wa kuirejeshea heshima klabu kwa kufanya vizuri kwenye mashindano. “Mkifanikiwa Yanga, nimefanikiwa mimi kama Serikali...mnatakiwa kupata kundi la wanachama ambao mtasaidiana kuvuka katika kipindi hiki cha mpito,”amesema.
    Aidha, Mwakyembe amewataka wale wanaopinga mabadiliko ya mfumo wa uendeshwa wa klabu hiyo kufika kwenye mkutano kutoa ya moyoni na wakishindwa wamfuate ofisini kwake.
    Pamoja na Waziri Mwakyembe, Mkutano huo pia ulihudhuriwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Huruma Mkuchika ambao walianza kwa kikao cha faragha na uongozi wa Yanga chini ya Kaimu Mwenyekiti, Clement Sanga.
    Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Mkurugenzi wa Michezo, Yusuph Singo, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya, Jaji John Mkwawa na Wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya klabu pamoja na Katibu Mkuu, Charles Boniface Mkwasa.
    Manji aliingia Yanga mwaka 2006 kama mdhamini kupitia kampuni yake ya Lotto Kitita, lakini baadaye akawa mfadhili Mkuu wa klabu kabla ya kuwa Mwenyekiti.
    Katika kipindi chake cha kuwa mfadhili na Mwenyekiti wa Yanga, Manji aliifanyia mengi klabu– kubwa ni kuirejeshea hadhi na heshima klabu hiyo.
    Alipoingia mwaka 2006 aliikuta klabu ipo dhoofu kiuchumi na haiwezi kushindana na mahasimu wao, Simba katika kuwania wachezaji bora ambao ndiyo mtaji wa kushinda mataji.
    Wakati huo Yanga ilikuwa inasajili wachezaji ambao ama walikuwa wameachwa na timu zao, waliojipeleka wenyewe kwa mapenzi yao au waliopatikana kwa njia ya mchujo wa majaribio.
    Lakini mara baada ya Manji kuingia Yanga, klabu hiyo ikaanza kusifika kwa kusajili wachezaji wa kigeni na wale nyota wa hapa nyumbani, ikiwa ni pamoja na kubomoa ngome ya mahasimu, Simba SC.
    Mwaka 2009 fedha za Manji zilimtoa kipa kipenzi cha wana Simba Msimbazi, Juma Kaseja na desturi hiyo ikaendelea baadaye wakichukuliwa beki Kelvin Yondan na mshambuliaji Mganda Emmanuel Okwi.
    Yanga iliipiku Simba ‘kimafia’ katika kumsajili beki anayeweza kucheza kama kiungo pia, Mbuyu Twite kutoka APR ya Rwanda, tu kwa jeuri ya fedha.
    Aliyekuwa Mwenyekiti wa Simba, Alhaj Ismail Aden Rage alianza kuonekana akimsainisha Mbuyu mjini Kigali, lakini baadaye Mwenyekiti wa Usajili wa timu ya Jangwani, Abdallah Bin Kleb akaingia kwa ‘gia kubwa’ na kubadilisha mambo, Mbuyu akatua Jangwani.
    Wanachama wa Yanga wakiwa katika mkutano Mkuu wa mwaka wa klabu yao Bwalo la Maafisa wa Polisi, Oysterbay leo 
    Wanachama wa Yanga wakiwa katika mkutano Mkuu wa mwaka wa klabu yao Bwalo la Maafisa wa Polisi, Oysterbay leo

    Wanachama wa Yanga wakiwa katika mkutano Mkuu wa mwaka wa klabu yao Bwalo la Maafisa wa Polisi, Oysterbay leo

    Na ni katika kipindi hicho imeshuhudiwa Manji amewazima kabisa Simba na Yanga ikitawala soka ya Tanzania na kuzidi kujiongezea mashabiki na wapenzi.
    Lakini migogoro haikukosekana pia wakati wa utawala wa Manji, ambayo wakati fulani iliiathiri timu mfano ule wa kutaka kumng’oa aliyekuwa Mwenyekiti, Wakili Lloyd Nchunga ulioiponza klabu ifungwe 5-0 na mahasimu, Simba Mei 6, mwaka 2012.
    Mapema mwaka jana, Manji alikuja na mpango wa kutaka kujikodisha klabu kupitia kampuni aliyoisajili kwa jina la Yanga Yetu, lakini ukapata upinzani mkali na kuamua kuachana nao.  
    Kabla ya kufikia maamuzi haya, Manji alipitia kwenye misukosuko na Serikali kuanzia Januari hadi Aprili, kwanza akikamatwa na kuwekwa ndani kwa tuhuma za kujihusisha na matumizi ya dawa za kulevya na baadaye akidaiwa kumiliki pasipoti mbili.
    Kwa sasa klabu inakabiliwa na hali ngumu kiuchumi kiasi cha kuambulia ushindi wa mechi moja kati ya 14 zilizopita, nyingine saba wakifungwa na sita kutoa sare. Na wana Yanga wako tayari Manji arejee kwa sharti lolote kuinusuru klabu.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: WANACHAMA YANGA WAMREJESHA MANJI MADARAKANI, TARIMBA APEWA JUKUMU LA KUSAJILI WACHEZAJI WAPYA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top